Mhe. Augustine Lyatonga Mrema
Na
Mwandishi Wetu
MWANASIASA mkongwe nchini
Augustine Lyatonga Mrema amesema Rais John Pombe Magufuli ameweka historia ya
mapambano ya uchumi nchini kutokana na namna ambavyo analishughulikia suala la
madini.
Bwana Mrema amesema kuwa
kitendo cha Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Cooperation Profesa John Thornton kusafiri usiku
kucha kuja kuonana na Rais Magufuli na kukubali kuilipa Tanzania fedha zote ilizokoseshwa
na Kampuni Acacia ni kielelezo kuwa sio tu kuwa ujumbe wake umefika lakini
zaidi inadhihirisha kuwa madai yake dhidi ya kampuni hiyo ya uchimbaji madini
ni ya msingi.
“Ni kiongozi gani barani
Afrika aliyethubutu kuishutumu kampuni ya nje kama alivyofanya Rais Magufuli
halafu viongozi wake wakasafiri kuonana na kiongozi huyo kutaka suluhu kama
alivyofanya Mwenyekiti huyo wa Barrick kwa Tanzania?”alihoji Bwana Mrema.
Mwanasiasa huyo aliungana
na wito wa Rais Magufuli wa kuwataka baadhi ya watu wanaowahusisha viongozi
wastaafu na taarifa za Tume za Rais za kuchunguza Makinikia.
“Si vizuri na kwamba si
sheria kwa mtu yeyote kuwatukana au kuwashambulia marais wastaafu kama ilivyo
kwa Rais aliye maradakani na sheria inatoa dhabu kali kwa wanaofanya hivyo”
alieleza bwana Mrema.
Alibainisha kuwa kuwahusisha
na taarifa hizo wakati hazijawataja kunaweza kusababisha kuigawa nchi na kuhatarisha
mshikamano wa Taifa katika kipindi hiki ambacho watanzania wanapaswa kuwa kitu
kimoja kumuunga mkono Rais wao na Serikali kwa hatua mbalimbali anazozichukua
kuimarish uchumi.
“Tumekubali kikatiba
Marais wetu waliopo madarakani na wastaafu walindwe kwa kuwa ndio ni msingi wa
utulivu, amani na mshikamano wetu hivyo hatuna budi kuwaheshimu kwa kutekeleza
hilo tulilokubaliana” alieleza Mrema.
Mwansiasa huyo alieleza kushangazwa
kwake na baadhi ya watu wakiwemo baadhi ya wabunge kumdhihaki Rais na kutozipa
uzito jitihada zake za kutetea maslahi ya nchi na kuhoji mbona wananchi wa nchi
nyingine kama Uingereza na Japan hawawabezi watawala wao akimaanisha Malkia na
Mfalme.
“Baadhi ya wabunge
wanaacha ajenda ya msingi ya kupambana na unyonyaji unaofanywa na makapuni ya
madini badala yake wanaanzisha kampeni dhidi ya Rais”alieleza Bwana Mrema na
kusema kuwa vitendo hivyo ni vya kichochezi, usaliti na ni vya kizandiki kwa Taifa.
Bwana Mrema alifafanua
kuwa kitendo cha baadhi ya wabunge kusema eti “Rais kama angekuwa makini”
asingechukua hatua alizochukua za kuzuia mchanga na kuunda Tume ni kitendo cha
kumdhallisha Rais ambaye alichaguliwa baada ya kuwashinda wagombea wengine
alioshindana nao katika mbio za uchaguzi wa nafasi hiyo.
“Huyo Rais ‘makini’ ni
yupi zaidi ya yule aliyewashinda wengine wote. Rais amekuja na mpango
anautekeleza, tumuunge mkono…sisi ndio tuliomchagua” Alisisitiza bwana Mrema.
Anabainisha kuwa
haiwezekani mtu mkubwa na mashuhuri kama Profesa John Thornton atoke Canada kuja kuonana na Rais wetu tena akiwa na
Balozi wa nchi yake iwe ni jambo la kupuuzwa.
Bwana Mrema alisema wako
waliotaka Rais ataifishe mali za makampuni zinazotuhutumiwa kuiibia Tanzania lakini
Rais Magufuli ametambua kuwa huu si wakati tena wa kutaifisha mali bali ni wa
kutumia sheria zilizopo kupata haki na ndivyo anachofanya.
Mrema ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Chama cha TLP alilikumbusha Jeshi la Polisi wajibu wake wa
kumlinda Rais dhidi ya kejeli za baadhi ya watu wakiwemo wabunge na kulitaka jeshi
hilo kutofanya ajizi kuwakamata watu wanaofanya vitendo hivyo dhidi ya Rais na
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
“Sheria ziko wazi kuhusu
jambo hilo. Hata mimi mwenyewe niliwahi kushitakiwa mahakamani kwa kesi kama
hiyo lakini nikashinda kwa kuwa waendesha mashitaka walishindwa kuthibitisha pasipo
shaka kuwa nilifanya kosa hilo” alifafanua Mrema na kujinasibu kuwa akiwa mtu
safi aliyelelewa vyema na Taifa lake kamwe hathubutu kumtusi au kumdhihaki kiongozi
wa nchi yake.
Tangu Rais Magufuli aunde
Tume za Kuchukunguza Mchanga wa madini kumwekuwepo na baadhi ya watu wanaopinga
hatua hiyo kwa madai kuwa inaweza kuitia Tanzania katika mgogoro wa kisheria na
kampuni ya Acacia.
Hata hivyo, baada ya ripoti
ya Kamati ya Pili ya Uchunguzi kuwasilisha taarifa yake kwa Rais Magufuli hivi
karibuni ambayo ilizidi kuonesha namna Kampuni hiyo ilivyoikosesha Serikali
trilioni za shilingi, Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Cooperation Profesa John Thornton alikuja nchini kwa
mashauriano na Rais.
Katika mazungumzo hayo muafaka
ulifikiwa kuwa iundwe Tume ya mashauriano kati ya kampuni hiyo na Serikali huku
kiongozi huyo wa Barrick akiahidi kurejeha fedha zote ambazo itabainika kuwa
kampuni ya Acacia ilipaswa kuilipa Tanzania.


No comments:
Post a Comment