Mtaalamu wa Sheria za Madini na Mafuta, Dkt. Adelardus Kilangi
Na Jacquiline Mrisho
– Maelezo
MTAALAMU mbobevu wa Sheria za Madini na Mafuta nchini,
Dkt. Adelardus Kilangi ametoa rai kwa wanasheria watakaoteuliwa kwa ajili ya
kurekebisha Sheria za Madini kuanza kufanya kwanza uchunguzi katika Sheria za Kimataifa za Madini ili waweze
kuishauri vizuri serikali.
Rai hiyo imetolewa leo na mtaalam
huyo katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hii kuhusu maoni juu ya
ripoti ya uchunguzi wa mchanga wa madini iliyowasilishwa na baadhi ya wachumi
pamoja na wanasheria walioteuliwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Dkt. Kilangi amesema kuwa ripoti
iliyowasilishwa imeonesha madhaifu yaliyopo katika sekta ya madini ambayo madhaifu
hayo yamegawanyika katika maeneo ya mfumo wa Sheria pamoja na mfumo wa
usimamizi ambapo tatizo kubwa limekuwa ni kukosa uzalendo kwa viongozi waliopewa
dhamana ya kufanya maamuzi ya nchi.
“Katika eneo la mfumo wa Sheria,
kwanza nampongeza Rais Magufuli kwa kuwataka wanasheria na wataalamu wengine kufanya
mapitio ya Sheria hizo kwa sababu tukitaka kuleta mabadiliko lazima tuanzie
kwenye Sheria hivyo kwa kutengeneza Sheria nzuri zenye manufaa kwa umma ni
lazima tuanzie katika ngazi za kimataifa kwani kuna vipengele vinavyoathiri
sekta yetu ya madini,”alisema Dkt. Kilangi.
Mtaalamu huyo ameongeza kuwa ni
lazima kufahamu kwanza mfumo wa Sheria za kimataifa kwa sababu nchi zilizoendelea zimetengeneza kwa makusudi
Sheria kandamizi kwa nchi zinazoendelea.
Amefafanua kuwa, kabla ya kuanza
kuchunguza Sheria zetu za ndani wanasheria lazima wafahamu jinsi mifumo hiyo
mitatu inavyofanya kazi na inavyoathiri sekta yetu ya madini, yaani sheria za
kimataifa ikiwemo ya Sheria za Kimapokeo/kimila za kimataifa (Customary
International Law), Mikataba inayoingiwa na mataifa mbalimbali (Multilateral
Framework) pamoja na mikataba inayosainiwa kati ya nchi mbili (Bilateral
Framework).Baada ya hapo ndio waje kwenye sheria zetu za ndani na hatimaye
mikataba kati ya serikali na wawekezaji.
Katika mapendekezo mengine, Dkt.
Kilangi alisema kuwa wasomi wanasheria na wataalamu wengine kama wachumi
wanatakiwa wapambane kisomi, wapewe hoja za kupambana na mfumo gandamizi uliopo
katika Sheria za kimataifa uliotengenezwa na mataifa makubwa, na kutafuta mbinu
za kupanga upya Sheria za madini nchini kwa kuongozwa na mapungufu
yaliyojitokeza katika ripoti mbili za mchanga wa madini, tafiti mbalimbali
pamoja na mitazamo kutoka nchi zingine juu ya mambo wanayoyaangalia katika
kubadilisha sheria zinazofanana na hizo.
Aidha, amependekeza wanasheria
kufanya marejeo haya kwa kuangalia pia
falsafa ya uchumi inayopaswa kutuongoza kwa kuangalia ufahamu wetu kama taifa
kuhusu njia kuu za uchumi na nyenzo kuu
za uzalishaji (Political Economy Analysis) ambapo wataweza kufahamu nani anamiliki
njia kuu za uchumi, nani anamiliki rasilimali, nani anatoa mtaji, nani anafanya
kazi, nani anazalisha na , faida
inapatikana kiasi gani, na nani anaipata faida hiyo, hali itakayopelekea
muwekezaji kuingia ubia mzuri na Serikali. Haya yote yafanywe kwenye muktadha
wa sekta ya madini.
Pia Dkt. Kilangi alisisitiza kuwa
katika mchakato huo wa kurekebisha sheria za madini ni vizuri kushirikisha
wananchi wa kawaida ili kupata maoni yao, kwani nao tayari wameshafahamu athari
za mikataba iliyopo sasa, na kwa kweli haya madini ni yao. Kwa hiyo kuhusishwa
kwao ni muhimu alisisitiza.
No comments:
Post a Comment