Mkuu wa Kitengo cha Maabara ya Uhandisi Ujenzi ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS)
Mhandisi Stephen Minja akionesha kwa waandishi wa habari vigae vilivyofikishwa
katika maabara hiyo ili kudhibitishwa ubora wake.(Picha zote na Maelezo)
Mkuu wa Kitengo cha Maabara ya Uhandisi Ujenzi ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Mhandisi Stephen Minja akionesha kipande cha Bomba kilichohakikiwa ubora katika maabara hiyo.
Mkuu wa Kitengo cha Maabara ya Uhandisi Ujenzi ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Mhandisi Stephen Minja akionesha kwa waandishi wa habari lami iliyofikishwa katika maabara hiyo ili kudhibitishwa ubora wake kwa mujibu wa sheria ili iweze kutumika katika ujenzi wa barabara hapa nchini.
Mkuu wa Kitengo cha Maabara ya
Uhandisi Ujenzi ya Shirika la Viwango
Tanzania (TBS) Mhandisi Stephen Minja akipima ubora wa Lami kwa kutumia mashine
maalum ili kudhibitisha kama ina ubora unaotakiwa kulingana na viwango
vilivyowekwa.
Mtaalamu wa masuala ya Umeme kutoka shirika la Viwango Tanzania (TBS) Bw. Evance Jeremiah akionesha namna mitambo ya kupima ubora wa vifaa vya umeme inavyofanya kazi.
Frank Mvungi, Maelezo, Dar es Salaam
SERIKALI imewataka wazalishaji na wajasiriamali nchini kuhakikisha kuwa bidhaa wanazozalisha
zinakidhi viwango vya ubora vilivyowekwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS)
ili kuchochea ukuaji wa uchumi.
Kauli hiyo imetolewa Leo Jijini Dar es Salaam na
Mkuu wa Kitengo cha Maabara ya Uhandisi wa Ujenzi ya Shirika la Viwango Nchini, Mhandisi Stephen Minja wakati wa ziara ya
waandishi wa habari kutembelea na kujionea namna maabara za shirika hilo
zinavyotekeleza jukumu lake la kuhakiki viwango vya ubora hapa nchini.
Akifafanua zaidi Minja amesema kuwa mabara za
shirika hilo zipo kwa ajili ya kuhudumia wazalishaji wa bidhaa mbalimbali na
wale wanaoingiza bidhaa kutoka nje ya nchi
lengo ili kuhakiki ubora wa bidhaa zote ili kuepusha athari zinazoweza
kujitokeza kwa watumiaji.
“Maabara yetu ina viwango vya kimataifa na gharama
zake ni nafuu ambazo kila mwananchi anaweza kumudu lengo likiwa ni kutoa huduma
kwa wananchi na kuchangia kuchochea maendeleo
kwa kudhibiti bidhaa hafifu” alisema
Minja.
Aliongeza kuwa maabara hiyo inapima bidhaa za
ujenzi kama nondo, chokaa, vigae, mbao, mabomba
ya maji, simenti, nguzo za umeme,matofali,zege, mchanga na bidhaa zote
zinazotumika katika ujenzi wa barabara ikiwemo lami.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa kitengo cha maabara
ya umeme Mhandisi Anectus Ndunguru
amesema kuwa vifaa vyote vya umeme vinavyozalishwa na kuingizwa nchini lazima
vipimwe ubora wake kuona kama vinakidhi vigezo ili kuepusha majanga.
Alitaja baadhi ya vifaa ambavyo lazima vihakikiwe
ubora wake kuwa ni vifaa vyote vinavyotumika katika kujenga mfumo wa umeme
katika majengo, taa za majumbani, pasi, redio, televisheni, waya .
Akizungumzia athari za kutumia vifaa visvyo na
ubora Ndunguru amesema kuwa athari za matumizi ya vifaa hivyo ni makubwa
ikiwemo kusababisha majanga na kupotea kwa umeme hivyo kuongeza gharama kwa
mtumiaji.
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limekuwa
likisisitiza matumizi ya bidhaa zenye ubora na zilizohakikiwa na kuepuka bidhaa
hafifu ambazo kwa sasa zimedhibitiwa na shirika hilo kwa kiwango kikubwa hali
inayochochea ukuaji wa sekta ya Viwanda hapa nchini.

No comments:
Post a Comment