Na Daudi
Manongi-Maelezo, Dodoma
SERIKALI kupitia Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema kuwa inategemea
kusambaza vifuko maalum vya kujifungulia
vyenye vifaa vya kujifungulia kwa
wanawake 500,000 ambavyo vitasambazwa
nchi nzima kulingana na uhitaji.
Hayo yamesemwa na
Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Mhe.Dk Khamis Kigwangalla wakati akijibu swali
la Mbunge wa Viti Maalum Mhe.Munira Mustafa Khatibu leo Bungeni Mjini Dodoma.
“Sera ya Afya ya
mwaka 2007 inaeleza kuwa Huduma za kina Mama wajawazito katika vituo vya ngazi
zote zinapaswa kutolewa bila malipo”, Alisisitiza Mhe. Kigwangala.
Aidha amesema kuwa
Serikali haijawahi kuweka tozo na gharama za vifaa vya kujifungulia na upasuaji
na hivyo huduma hizo zitaendelea kutolewa katika ngazi zote katika vituo vya
umma vya kutolea huduma kwa gharama za Serikali.
Aidha kwa upande
mwingine Mhe. Kigwangala ametoa rai kwa Wabunge kusaidia kusimamia utekelezaji wa Sera walizokubaliana
katika katika maeneo yao husika ili kuhakikisha huduma hizi za kina mama
zinapatikana kwa Gharama za Serikali kama ilivyopangwa.
“Ili azma ya Serikali
ya Kuhakikisha akina mama wajawazito wanapata huduma nzuri na lengo la
kupunguza vifo vya mama na watoto inafanikiwa ni lazima usimamizi uwe wa karibu
sana”, Aliongeza Mhe. Kigwangalla.
Aidha jumla ya kina
mama 1,900,000 hujifungua kila mwaka nchini na kumekuwa na changamoto katika
upatikanaji wa vifaa ambapo kwa sasa Serikali imeliwekea mkazo suala hilo ili
kuhakikisha kina mama hao wanajifungua salama.


No comments:
Post a Comment