TANGAZO


Saturday, December 3, 2016

PROF. OLE GABRIEL: SIRI YA MAFANIKIO KATIKA TAASISI NI KUFIKIRI KIMKAKATI NA USIMAMIZI BORA

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akiongea na Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST) alipowatembelea akiwa mmoja wa wanachuo wa mwanzao waliohitimu katika chuo hicho ambapo awali kilijulikana na kama Taasisi ya Sayansi na Teknolojia (MIST). Prof. Ole Gabriel amewahimiza viongozi hao wawe msatari wa mbele katika kusimamia taaluma na kuwajengea uwezo wanafunzi wao wajitambue na wawe na utamaduni bora wa kufikiri kimkakati na usimamizi ili waweze kuendana na ulimwengu wa sasa. (Picha zote na Eleuteri Mangi, WHUSM, Mbeya)
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akitembelea moja ya karakana wakati wa ziara yake hivi karibuni katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST).  
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akiteta jambo na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST) Prof. Joseph Msambichaka mara baada ya kikao na Menejiment ya chuo hicho wakati wa ziara yake hivi karibuni Mkoani Mbeya. 
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST), Prof. Joseph Msambichaka (katikati), akimkabidhi Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) moja ya madaftari yake aliyotumia wakati akisoma chuni hapo kikijulikana kama Taasisi ya Sayansi na Teknolojia (MIST).
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akifurahia zawadi ya moja ya madaftari aliyotumia akiwa mwanafunzi katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia (MIST), ambapo kwa sasa ni Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST). 
Moja ya vyombo vya usafiri alivyotumia Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa mwanafunzi katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia (MIST), ambapo kwa sasa ni Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST).  
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyevaa tai nyekundu) akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya mkutano wake na Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST) hivi karibuni mkoani Mbeya.

Na Eleuteri Mangi-WHUSM, Mbeya
VIONGOZI wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST) wametakiwa kuwa imara katika kusimamia taaluma chuoni hapo na kuwajengea uwezo wanafunzi wa kujitambua na kuwa utamaduni bora wa kufikiri kimkakati na usimamizi ili waweze kuendana na kasi ya ulimwengu wa sasa wa sayansi na teknolojia.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel amsema hayo, alipokuwa akiongea na wajumbe wa Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST) hivi karibuni alipokuwa katika ziara ya kikazi mkoani Mbeya.

Prof. Ole Gabriel amewaambia wajumbe hao kuwa siri kubwa ya mafanikio ni pamoja na kutimiza amri ya sita za kufikiri kimkakati na usimamizi ikiwemo kujenga utendaji bora, kudumisha utendaji bora, kuelewa kazi za msingi wako, kujua mshindani wako katika kazi unayofanya, kukabiliana na kasi ya Teknolojia pamoja na kuwa wazi juu ya malengo uliyojiwekea wakati wote.

Ili chuo hicho kifikie malengo yake, Prof. Ole Gabriel amewaambia wajumbe wa Menejimenti ya Chuo hicho kuwa ni vema wawe na utamaduni wa kufanya tafiti mbalimbali na usimamizi hatua ambayo itakifanya chuo hicho kuwa bora miongoni mwa vyuo vikuu nchini kwa kutoa wananfunzi wenye ubora unaohitajika kwenye soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Zaidi ya hayo, viongozi hao wameshauriwa pia kujenga utamaduni wa kuwa miongoni mwa watu wenye fikra kubwa ambao wanania ya kutengeneza mambo yatokeee na wasiwe watu wa wastani wenye nia lakini wanaangalia mambo yatokee wala wasiwe watu wenye akili za kawaida wenye nia lakini wanashangaa kwanini mambo yanatokea.

Aidha, Prof. Ole Gabriel amezitaja sifa za mtu anayefikiri kimkakati na usimamizi kuwa ni pamoja na daima kuona fursa nje ya matatizo, kuwa na mkakati wa majadiliano, kuripoti matatizo na ufumbuzi mbadala, pamoja na kufanya maamuzi kwa haraka na kwa usahihi.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST) Prof. Joseph Msambichaka kwa niaba ya Menejimenti amemshukuru Katibu Mkuu Prof. Ole Gabriel kuwajali na kuwathamini ikizingatiwa ni miongoni mwa wanachuo wa mwanzao waliohitimu katika chuo hicho ambapo awali kilijulikana na kama Taasisi ya Sayansi na Teknolojia (MIST).

Akitoa taarifa fupi ya chuo, Prof. Msambichaka amesema kuwa chuo kwa sasa kina jumla ya wanachuo 3,852 ambapo idadi ya wanachuo wa wanaume 3,236 na idadi ya wanawake ni 616 ambao wanasoma katika sehemu nne za chuo hicho.

Sehemu hizo ni Taasisi ya Sayansi na Teknolojia, Taasisi ya Uhandisi na Teknolojia, Shule ya Mafunzo ya Biashara pamoja na Chuo cha Sayansi na Ualimu wa Ufundi.

No comments:

Post a Comment