Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Mboza Lwandiko akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu hali ya Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya leo Jijini Dar es Salaam.
Na Georgina Misama –
MAELEZO
WIZARA ya Ardhi, Nyumba
naMaendeleo ya Makazi imewataka watanzania kutumia Mabaraza ya Ardhi na Nyumba
ya Wilaya katika kutatua matatizo mbalimbali
yanayohusu Nyumba na Makazi.
Hayo yamesemwa leo na
Kaimu Msajili Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya Bi Amina Rashidi wakati akiongea
na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya habari Maelezo.
“Mabaraza ya Ardhi na
Nyumba ndiyo chombo pekee kilichoundwa kwa ajili ya kutatua matatizo yote yanayohusu
ardhi na nyumba” alisema Amina.
Akitaja baadhi ya
mashauri yanayosikilizwa kwenye Mabaraza hayo Amina alisema mashauri yanayotokana
na milki pandikizi (double allocation) au mashauri ya wananchi wanaopakana kwa mmoja
wao kutaka kujipanulia eneo. Yapo pia mashauri ya wenye nyumba na wapangaji yanayofunguliwa
kwa kukiukwa kwa mikataba.
Aidha, Amina alifafanua
kwamba uendeshaji wa mashauri katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ni wakirafiki nasio
unaofuata taratibu za Mahakama za kawaida. Wajumbe wa Baraza wanatoka miongoni mwa
wanajamii wa eneo ambalo Baraza limeundwa.
Nae Mkuu wa Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi Bi. Mboza Lwandiko alitolea ufafanuzi wa
dhamira ya wizara yake katika kuhakikisha inapambana na ongezeko la mashauri kwa
kuunda Mabaraza mapya yapatayo 20 kila mwaka.
“Katika mwaka wa fedha
2016/2017 Wizara itakamilisha taratibu za kuunda Mabaraza(44) kati ya Mabaraza
mapya 47 yaliyoundwa na tangazo la serikali la mwezi Aprili, 2016” alisema
Mboza.
Tayari takribani mashauri
elfu 43 yamesikilizwa kati ya mashauri elfu 59 yaliyofunguliwa kwa kipindi cha
kuanzia Oktoba 2004 na Septemba 2016.
No comments:
Post a Comment