TANGAZO


Sunday, October 9, 2016

NEC YAPONGEZWA KWA KUTOA ELIMU YA MPIGA KURA WIKI YA VIJANA MKOANI SIMIYU

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mhe. Jenista Muhagama (katikati) akikata utepe kufungua rasmi maadhimisho ya Wiki ya Vijana leo mkoani Simiyu. Kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Anthony Mavunde, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Antony Mtaka (wa pili kutoka kushoto), Waziri Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu Titus Kamani na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mhe. Abdallah Possi (Mwenye Kofia).
Baadhi ya Wanachi wakifuatilia ufunguzi rasmi wa maadhimisho ya Wiki ya Vijana na Kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere wilayani Bariadi mkoani Simiyu leo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mhe. Jenista Muhagama akipata maelezo kuhusiana na Elimu ya Mpiga Kura alipotembelea Banda la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) leo mkoani Simiyu.
Wananchi wilayani Bariadi mkoani Simiyu wakipata elimu ya Mpiga Kura kwenye banda la Maonesho la NEC leo.
Watumishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakiandaa vipeperushi vya Elimu ya Mpiga Kura tayari kuwagawia viongozi na wananchi wanaotembelea Banda la Maonesho la NEC.

Na Aron Msigwa –NEC ,  Bariadi –Simiyu.
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imepongezwa kwa kuanzisha programu endelevu  za utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura kwa kuwafikia wananchi moja kwa moja katika maeneo yao kote nchini.

Akitoa pongezi hizo mara baada ya kutembelea Banda la Maonesho la Elimu ya Mpiga Kura la NEC wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Vijana yanayofanyika Bariadi mkoani Simiyu,  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mhe. Jenista Muhagama amesema kuwa hatua ya NEC  kutoa elimu ya mpiga kura kupitia maonesho hayo inawasaidia wananchi kujifunza masuala mbalimbali kuhusiana na chaguzi za Tanzania.

“ Nawapongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuanzisha utaratibu huu wa kushiriki maonesho mbalimbali, mnafanya kazi nzuri, endeleeni hivyo hivyo kuwaelimisha wananchi” Amesema Mhe. Jenista.

 Ameeleza kuwa ushiriki wa NEC katika maadhimisho ya Wiki ya Vijana unawapa fursa vijana wengi kupata elimu sahihi kuhusu wajibu wao na majukumu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika kuratibu na kusimamia Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.

Kwa upande wake Afisa Habari wa Idara ya Elimu ya Mpiga Kura ya NEC Bi. Margareth Chambiri amwemweleza Waziri huyo kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeanzisha program endelevu za kutoa elimu ya mpiga kura kwa kuhakikisha kuwa wananchi moja kwa moja katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema NEC inatoa elimu hiyo kwa wananchi ili kuwawezesha kuwa na uelewa sahihi kuhusu utendaji wa Tume na masuala mbalimbali yanayohusu upigaji wa kura, sheria, taratibu na kanuni zinazosimamia uchaguzi, taarifa za wapiga kura na maelekezo ya namna ya kufanya endapo kadi zao za kupigia kura zimepotea au kuharibika, mwananchi kuhama eneo moja kwenda jingine kutokana na sababu mbalimbali.

Baadhi ya wananchi waliolitembelea banda la NEC wameeleza kufurahishwa ufafanuzi  na elimu ya Mpiga kura inayoendelea kutolewa na Maofisa wa Tume hiyo  kupitia majibu ya maswali mbalimbali wanayouliza hususan uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura kwa mujibu wa Sheria ambao utakaowapa fursa ya kuhuisha taarifa zao pia kupewa elimu kuhusu uendeshaji wa chaguzi mbalimbali hapa nchini.

Aidha, wameiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuendelea kutoa elimu ya Mpiga kura katika maeneo  mengine nchini kwa ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kupata elimu sahihi kuhusu utendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

No comments:

Post a Comment