TANGAZO


Saturday, October 8, 2016

DC NDEJEMBI AKIFUNGA CHUO CHA UALIMU NKURUMA, MKOKA KWA KUTAPELI WANAFUNZI

Mkuu wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Mhe Deogratius Ndejembi

MKUU wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Deogratius Ndejembi amekifunga Chuo cha Ualimu cha Nkuruma kilichopo Mkoka na kuagiza uongozi wa chuo hicho, kurudisha fedha zote za ada walizolipa wanafunzi ili ziwasaidie kulipia vyuo vingine.

Alitoa agizo hilo, wakati wa mkutano na wanafunzi pamoja na uongozi wa chuo hicho, kuhusu kutafuta suluhu ya mgogoro ambao ulianza Septemba 16, mwaka huu. Chuo hicho kilidahili wanafunzi 77 kwa lengo la kuwafundisha ualimu, walipofika wakaambiwa wanasoma masomo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT).

“Baadaye wakaambiwa wanabadilishiwa masomo sasa wanasoma Maendeleo ya Jamii, hii yote wamefanya kwa kuwa chuo hakina usajili wowote. Ada wamechukua na hakuna kinachoendelea,” alisema Ndejembi.

Ndejembi alifikia hatua ya kukifunga chuo kutokana na wanafunzi kugoma kufanya mitihani ya chuo ya kumaliza mwaka wa masomo kwa madai chuo hakitambuliwi na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).

Alisema kukifungia chuo pekee haitoshi wanatakiwa kurudisha fedha zote za ada walizolipwa na wanafunzi katika mwaka huo wa masomo uliopita ili kuwasaidia kulipa vyuo vingine.

“Kuwarudishia fedha sio mwisho wa jambo hili kwa sababu mmepotezewa muda wenu na haki yenu ,mmeonewa, mmedhulumiwa kwa kusema hivyo namwagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya na timu yake kuwakamata sasa hivi na wafikishwe kwenye vyombo vya kisheria ili haki iweze kutendeka,” alisema.

Amewataja wanaotakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria kuwa ni mmiliki wa chuo, Mathew Nkurlu, Msajili wa Chuo, Yohana Michael, Mhasibu Elieth Ruben, wakufunzi Pendael Petro na Christopher Mabatian.

Ndejembi alitaja sababu za kuagiza wakamatwe viongozi hao wa chuo ni kuwa walihusika kushiriki katika kufanya udanganyifu na kuwatapeli wanafunzi hao huku wakijua kinachoendelea.

Aidha, alisema serikali itawasaidia katika utaratibu wa kupata vyuo vingine kwa wale wenye sifa za kujiunga na vyuo katika kozi ambayo walianza kusoma.

Alisema kama ikitokea chuo hakina fedha za kuwarudishia wanafunzi, majengo yao yatatumika kama dhamana ya ada kwa vyuo ambavyo vitawapokea wanafunzi hao. Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa chuo hicho, Mhoja Matando aliishukuru serikali kwa kuwasaidia kujua hatma ya kutimiza ndoto yao ya kielimu.

No comments:

Post a Comment