Na
Ally Daud-MAELEZO
DAWA muhimu za
binadamu zinapatikana kwa wingi katika Bohari kuu ya dawa MSD kwa masaa 24
zikiwemo dawa za kutibu Malaria, Kifua kikuu, Ukoma ,ARV , dawa za kutuliza
maumivu pamoja na Anti- biotic ili kutimiza na kutekeleza sera ya mpango wa
Afya wa awamu ya tano.
Hayo yamesemwa na
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu
wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika leo jijini Dar es
salaam ili kuzungumzia hali ya upatikanaji wa dawa na chanjo nchini.
“Dawa zote muhimu kwa
binadamu zinapatikana kwenye bohari kuu ya dawa kwa masaa 24 kinyume na watu na Taasisi zisizo za kiserikali kusambaza
maneno kuwa MSD imeishiwa dawa kitendo ambacho sio cha kweli dawa zipo na
zinasambazwa kwenye vituo vyote vya afya” Alisema Mhe. Ummy.
Aidha Ummy amesema
kuwa ili kutekeleza mpango wa sera ya afya ya Serikali ya tano ,jumla ya
shilingi bilioni 251 zimetengwa ili kuweza kuhakikisha dawa za binadamu
zinapatikana kila wakati pindi zinapohitajika kutoka MSD ili kutoa huduma bora
kwa watanzania.
Aliongeza kuwa
Serikali imetenga Bilioni 85 kwa ajili ya kulipa deni linalodaiwa na MSD ili
kuhakikisha Bohari hiyo inajiendesha vizuri na kutokaukiwa dawa pindi
zinapohitajika katika vituo vya afya na kutoa huduma za matibabu kwa muda
muafaka kwa watanzania.
Mbali na hayo Waziri
huyo amesema kuwa tatizo la chanjo kwa sasa limepata ufumbuzi kwani zimeagizwa
chanjo za watoto za kifua kikuu dozi milioni 2,
chanjo za Pepopunda dozi milioni 1.2
na chanjo za Polio ambazo ni dozi 2 ili kuimarisha hali ya matibabu nchini.
“Tulikuwa na tatizo
la chanjo kama wiki nne zilizopita lakini tumejitahidi na tumeweza kuleta
chanjo zote muhimu pamoja na kuagiza chanjo za surua ambazo zinatarajiwa kuja
hivi karibuni ili kuhakikisha chanjo zinapatikana kwa wingi nchini” alisisitiza
Waziri huyo.
Aidha amesisitiza
kuwa wanahitaji kununua na kufanya uzalishaji wa dawa katika viwanda vya ndani
ili kuweza kuchangia uchumi wa viwanda vya ndani ili tufikie uchumi wa kati.
Waziri Ummy aliwataka
Wakurugenzi wa Vituo vya Afya pamoja na Waratibu wa Afya wa Wilaya kuagiza dawa
MSD mapema bila ya kusubiri ziishe
kabisa kwenye vituo vyao ili kuweza kuondoa usumbufu kwa wagonjwa.
No comments:
Post a Comment