Na Shamimu Nyaki-WHUSM.
WAZIRI wa Habari Utamaduni,Sanaa na
Michezo Mhe.Nape Moses Nnauye amezindua studio ya redio ya jamii ya ‘Community
Media Network of Tanzania’ (COMNET)
katika Chuo kuku Huria( OUT ) itakayotumika
kusambaza habari maeneo yenye uhaba wa redio.
Uzinduzi huo umefanyika leo
jijini Dar es Salaam,ambapo Mhe. Waziri amesema kuwa studio hiyo itasaidia idadi kubwa ya wanachi wanaoishi vijijini
kupata habari kutoka Serikalini na kutoa mrejesho wa kile watakachosikia kwa
urahisi.
“Ni Studio muhimu kwa ajili ya
kusambaza demokrasia kwa watu hasa wale
waliopo vijijini kwa vile redio nyingi bado hazijawafikia”Alisema Mhe.Nape.
Aidha amewataka wanafunzi wa taaluma
ya uandishi wa habari na mawasiliano kwa
umma katika chuo hicho kutumia studio hiyo kujifunza zaidi kwa
vitendo na kuzingatia maadili ya uandishi wa habari kwa kuandika habari zenye
ukweli kutoka vyanzo sahihi ili kutoa ujumbe wenye manufaa mazuri kwa jamii.
Kwa upande wake Makamu mkuu wa Chuo
hicho Pro.Elifas Bisanda amesema studio hiyo imeanzishwa kwa ushirikiano na
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni(UNESCO) kwa lengo kutoa elimu kwa jamii ambayo imekuwa
haipati habari kwa urahisi.
Amewataka wanahabari na wananchi kwa
ujumla kufikisha habari katika studio hizo kwa kuwa
inatumia njia ya haraka na rahisi katika kufikisha ujumbe kwa kushirikiana na
redio mbalimbali za jamii.
Naye mwakilishi kutoka Shirika la umoja wa
mataifa linaloshughulikia Elimu,Sayansi,na Utamaduni(UNESCO) Bi. Zulimira
Rodrigues amesema studio ya redio ya ‘Community’
ipo kwa ajili ya kutoa elimu kwa jamii kuhusu maendeleo ya wanawake na vijana
ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.
Mpaka sasa Shirika hilo limefanikiwa
kuanzisha redio za jamii katika baadhi ya mikoa ya Tanzania bara ambayo ni
Mwanza, Arusha na Tanga na katika baadhi ya maeneo ya Unguja na Pemba.
No comments:
Post a Comment