Baadhi
ya Mawakili wa Serikali waliohudhuria semina hiyo wakisikiliza kwa makini
mafunzo hayo yaliyofanyika leo Mjini Dodoma.
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
SERIKALI imezitaka taasisi zake zote kufuata
sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 na taratibu zake kwa manunuzi
mbalimbali ya vifaa vya ofisi ili kuhakikisha fedha iliyotumiwa inalingana na
huduma iliyopatikana.
Hayo yamesemwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi,
Benno Sanga kwenye Mafunzo ya Sheria ya
Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 kwa
Mawakili wote nchini iliyofanyika mjini Dodoma.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, yamelenga kuwapa mawakili ujuzi katika utoaji
mzuri wa ushauri wa kisheria kwa Taasisi za Serikali.
Wakili Mwandamizi Sanga alisema kuwa msingi mkubwa
wa sheria hiyo ni ushindanishwaji wa wazabuni unaoweza kuiletea Serikali
thamani ya fedha.
“Kila taasisi ya serikali lazima ifuate sheria ya
manunuzi kwa manunuzi mbalimbali ya vifaa vya ofisi,sheria hii imeweka
utaratibu wa kuhakikisha fedha iliyotumiwa inalingana na huduma
inayopatikana”,alisema Sanga.
Akitoa mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa
Mikataba (Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali) Bi.Monica Otaru alisema
mafunzo hayo yatawasaidia mawakili kufanya upekuzi wa mikataba kwa makini na
uhakika zaidi.
“Pamoja na kuwa kazi ya kupekua mikataba ni sehemu
ndogo ya kazi zetu lakini inachukua muda mwingi, hivyo mafunzo haya yatawaandaa
Mawakili wa Serikali walioko katika Ofisi za Kanda kuweza kufanya upekuzi wa
mikataba kwa umakini na uhakika zaidi”,alisema Bi. Otaru.
Aidha, Bi. Otaru amezitaja baadhi ya changamoto
zinazosababisha kazi ya uhakiki wa mikataba kutofanyika kwa usahihi zikiwemo za
mikataba kukosa maelezo na maoni kamili ya taasisi husika.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni gharama za
kusafirisha mikataba kutoka taasisi husika,ugumu wa njia za mawasiliano pamoja
na kutoshirikishwa kwa taasisi husika katika mchakato wa manunuzi na uandaaji
wa mikataba.
Naye Wakili wa Serikali Mwandamizi Divisheni ya
Mikataba, Said Kalunde ameelezea juu ya mambo muhimu ya kuzingatia katika
kufanya upekuzi wa mikataba ya ununuzi
ikiwemo ujazaji wa fomu mbalimbali zinazotumika katika uhakiki wa
mikataba kwa mujibu wa Sheria hiyo ya manunuzi.
“Ni muhimu sana kwa wakili kujiridhisha kama
taratibu za ujazaji wa fomu zimefuatwa na fomu zimejazwa kwa usahihi,endapo
wakili hatojiridhisha kwa kuhakiki fomu hizo huenda akapatwa na matatizo makubwa
ya kiutendaji, alisema Kalunde.
Mafunzo hayo yametolewa kwa mawakili wa serikali divisheni
ya mikataba ili kuwajengea uwezo wa kutekeleza jukumu la kuhakiki mikataba
inayotokana na wazabuni.
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeundwa
chini ya kifungu cha 59 cha Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni mshauri wa masuala ya kisheria kwa Serikali ya
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya kifungu cha 59(3) cha Katiba ya mwaka
1977.



No comments:
Post a Comment