Naibu Waziri, Wizara ya Fedha na Mipango, Ashatu Kijaji akijibu hoja mbalimbali za Wabunge Bungeni mjini Dodoma, 12 Mei, 2016.
Naibu Waziri, Wizara ya Fedha na Mipango, Ashatu Kijaji akijibu hoja mbalimbali za Wabunge Bungeni mjini Dodoma, 12 Mei, 2016.
NAIBU Waziri,
Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, ameliambia Bunge Mjini Dodoma,
leo tarehe 12 Mei, 2016, kwamba serikali inaandaa sera ya Taifa ya huduma ndogo
za fedha ya mwaka 2016, itakayosimamia na kutatua changamoto zinazoikabili
sekta hiyo.
Alisema kuwa sera
hiyo itawasilishwa mbele ya Baraza la Mawaziri hivi karibuni kabla ya kupelekwa
bungeni hatimaye itapatikana sheria ya kusimamia taasisi ndogo za
fedha-microfinance Act, 2016.
"Serikali
inatambua changamoto ya taasisi binafsi za fedha zinazosumbua wananchi, hivyo
sheria hiyo ikitungwa itasaidia kuondoa matatizo hayo" alisisitiza Dkt.
Kijaji.
Naibu Waziri huyo
wa Fedha na Mipango alikuwa akijibu swali lililoulizwa na Mhe. Rahisa Abdalah
Musa (Viti maalumu), aliyetaka kujua serikali ilikuwa na mpango gani wa
kudhibiti utitiri wa taasisi za fedha pamoja na mabenki ili yalete tija kwa
Taifa kwa kuwakopesha wananchi.
Akijibu swali la
msingi na maswali ya nyongeza yaliyoulizwa na Mhe. Faida Mohamed Bakar (Viti
maalumu) aliyetaka kujua mikakati ya serikali ya kuanzisha benki ya
wafanyabiashara wakubwa na wadogo ili kuwawezesha kupata huduma bora, Dkt.
Ashatu Kijaji alisema kuwa serikali haina mpango wowote wa kufanya hivyo.
Alisema kuwa badala
yake serikali inafanya jitihada za kuimarisha benki zake zilizopo ikiwemo Benki
ya maendeleo ya Kilimo (TADB) na Benki ya Rasilimali (TIB) ili kukidhi mahitaji
ya wafanyabiashara wa kada mbalimbali.
"Serikali
imeiboresha kimuundo, Benki ya Rasilimali (TIB) kwa kuunda kampuni tatu
zinazofanyakazi kwa kujitegemea lakini kwa ushirikiano wa karibu"
alisisitiza Dkt. Kijaji
Alizitaja kampuni
hizo kuwa ni TIB Benki ya Maendeleo itakayotoa mikopo ya muda wa kati na mrefu
kwa wafanyabiashara wakubwa na wa kati, TIB Benki ya Biashara itakayowahudumia
wafanyabiashara wakubwa, wa kati na wadogo na TIB Rasilimali itakayohusika na
masuala ya ushauri kwenye Soko la Hisa na Mitaji la Dar es salaam.
"Pamoja na
mambo mengine, kampuni hii inawajibika kuwashauri wafanyabiashara, hususan wa
sekta ndogo ya fedha kupata mitaji kupitia Soko la Hisa la Dar es salaam"
aliongeza Dkt. Kijaji
Dkt. Kijaji alisema
kuwa pamoja na juhudi za serikali za kuboresha benki hizo, ikiwemo Benki ya Posta,
Serikali kupitia Benki Kuu (BOT) inaendelea kuweka mazingira wezeshi ikiwemo
kutunga sheria, kanuni na taratibu za kusaidia nguvu za wananchi na sekta
binafsi kuanzisha benki au taasisi za fedha katika maeneo yao.
"Ni matarajio
yetu kuwa wananchi wanatumia fursa ya mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo
nchini kuwekeza wao wenyewe au kuzishawishi benki za biashara kuanzisha huduma
za kibenki katika maeneo yao" alisema Dkt. Kijaji.
Kuhusu ombi la
mbunge huyo kuitaka serikali iingilie kati masuara ya riba zinazotozwa na
taasisi za fedha na kuwaumiza wananchi, Dkt. Kijaji alisema kuwa serikali
haiwezi kudhibiti wala kuingilia jambo hilo.
Alisema kuwa
Serikali ilijitoa katika uendeshaji wa moja kwa moja wa shughuli za kifedha
tangu mwaka 1991 ili kuruhusu ushindani huru na kuboresha huduma katika sekta
ya fedha hivyo viwango vya riba na mikopo vinavyotozwa na benki hizo na taasisi
nyingine za fedha zinapangwa kutokana na nguvu ya soko.
Dkt Kijaji alieleza
kuwa katika upangaji wa viwango vya tozo na riba mbalimbali benki na taasisi za
fedha huzingatia gharanma za upatikanaji wa fedha, halikadhalika gharama za
uendeshaji na sifa alizonazo mkopaji"Alisisitiza Dkt Kijaji
Imetolewa na:
Benny
Mwaipaja
Kaimu
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara
ya Fedha na Mipango
DODOMA
12/5/2016
No comments:
Post a Comment