TANGAZO


Monday, May 2, 2016

DAR ES SALAAM WALIVYOSHEREHEKEA MEI DEI, RC MAKONDA AWA MGENI RASMI, AHUTUBIA WAFANYAKAZI

Bendi ya Polisi ikiongoza maandamano ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (May Day), mkoani Dar es Salaam jana, ambapo Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda alikuwa mgeni rasmi Uwanja wa Uhuru jijini. (Picha zote na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com) 
Wafanyakazi wa Mashirika, Taasisi za Serikali na Kampuni binafsi wakiwa katika maandamano ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (May Day), mkoani Dar es Salaam jana,  
Bendia ya Magereza 'Wanamkote Ngoma wakitumbuiza wakati wa maadhimisho hayo. 
Wafanyakazi wa Bandari (TPA), wakiingia uwanjani na mabango yao kwa ajili ya kupita mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Walimu wa Wilaya ya Ilala, wakipita na mabango yao mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati wa maadhimisho ya Mei Dei jijini jana. 
Wafanyakazi wa Tume ya Utumishi, wakipita na mabango yao mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati wa maadhimisho ya Mei Dei jijini jana.  
Wafanyakazi wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, wakipita na mabango yao mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati wa maadhimisho ya Mei Dei jijini jana.   
Wafanyakazi wa Hospitali ya Aga Khan, wakipita na mabango yao mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati wa maadhimisho ya Mei Dei jijini jana.   
Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (katikati), akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema (wa pili kulia) pamoja na viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi, akiyapokea maandamano hayo ya maadhimisho ya Mei Dei jijini jana.   
Wafanyakazi wa Kiwanda cha Dawa cha Shelys, wakipita na mabango yao mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati wa maadhimisho ya Mei Dei jijini jana.   
Baadhi ya wafanyakazi wa taasisi na mashirika mbalimbali wakipita mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati wa maadhimisho ya Mei Dei jijini jana.   
Wafanyakazi wa SSRA, wakipita na mabango yao mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati wa maadhimisho ya Mei Dei jijini jana.   
Wafanyakazi wa Mfuko wa PPF, wakipita na mabango yao mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati wa maadhimisho ya Mei Dei jijini jana.   
Walimu na baadhi ya wafanyakazi Chama cha Wafanyakazi wa Talgwu, Manispaa ya Ilala wakipita mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati wa maadhimisho ya Mei Dei jijini jana.   
Wafanyakazi wa Kampuni za Ranchi za Taifa (Narco), wakipita na mabango yao mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati wa maadhimisho ya Mei Dei jijini jana.   
Wanafunzi wa Elimu ya Juu, wakipita na mabango yao mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati wa maadhimisho ya Mei Dei jijini jana.   
Wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), wakipita na mabango yao mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati wa maadhimisho ya Mei Dei jijini jana.   
Wanafunzi, wahadhiri pamoja na wafanyakazi wengine wa Chuo Kikuu cha Ardhi, wakipita na mabango yao mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati wa maadhimisho ya Mei Dei jijini jana.   
Baadhi ya wanafunzi na wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Ardhi, wakipita mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati wa maadhimisho ya Mei Dei jijini jana. 


Wanafunzi, wafanyakazi wengine wa Chuo Kikuu Huria, wakipita na mabango yao mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati wa maadhimisho ya Mei Dei jijini jana.   
Wafanyakazi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), wakipita na mabango yao mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati wa maadhimisho ya Mei Dei jijini jana. 
Wafanyakazi wa Benki ya Posta Tanzania (TPB), wakipita na mabango yao mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati wa maadhimisho ya Mei Dei jijini jana. 
Magari ya Kampuni na Mashirika mbalimbali yakipita na mabango mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati wa maadhimisho ya Mei Dei jijini jana. 
Wafanyakazi wa Azam, wakipita na mabango yao mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati wa maadhimisho ya Mei Dei jijini jana. 

Wafanyakazi wa Radio Uhuru, wakipita na gari lao, mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati wa maadhimisho ya Mei Dei jijini jana. 
Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (wa tatu kushoto), akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema (wa nne) pamoja na viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi, akiimba wimbo wa wafanyakazi wakati wa maadhimisho hayo ya Mei Dei jijini jana. 
Mmoja wa viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi, akisoma risala ya wafanyakazi wakati wa maadhimisho hayo ya Mei Dei jijini jana.  
Wafanyakazi wa Mashirika, Taasisi za Serikali na Kampuni binafsi wakiwa wamekaa kwenye jukwaa kusubiri hotuba ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda mara baada ya kumalizika kwa maandamano yao ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (May Day), mkoani Dar es Salaam jana,  
Baadhi ya wafanyakazi wa Mashirika, Taasisi za Serikali wakiwa na furaha kwenye jukwaa wakati wakisubiri hotuba ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda mara baada ya kumalizika kwa maandamano yao ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (May Day), mkoani Dar es Salaam jana. 
Baadhi ya wafanyakazi wa Mashirika, Taasisi za Serikali wakiwa wamepozi kwenye jukwaa wakati wakisubiri hotuba ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda mara baada ya kumalizika kwa maandamano yao ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (May Day), mkoani Dar es Salaam jana.  
Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akitoa hotuba yake mara baada ya kumalizika kwa maandamano ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (May Day), mkoani Dar es Salaam jana.  
Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akimkabidhi hundi ya fedha kiasi cha sh. milioni mbili mmoja wa wafanyakazi bora wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (May Day), mkoani Dar es Salaam jana. 
Waimbaji wa Bendia ya Magereza 'Wanamkote Ngoma wakitumbuiza wakati wa maadhimisho hayo. 

HOTUBA YA MHE. MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM KATIKA SHEREHE ZA MEI MOSI – 2016

Ndugu Viongozi wa TUCTA,
Ndugu Viongozi wa TRAWU,
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya,
Ndugu Viongozi wa Vyama mbalimbali vya Wafanyakazi,
Wastahiki Mameya na Wakurugenzi wa Halmashauri,
Ndugu Wafanyakazi wote walioshiriki sherehe hizi.

Awali ya yote nawashukuruni sana kwa kunipa heshima ya kuwa Mgeni Rasmi siku hii ya leo; Nami niungane nanyi kuonyesha

furaha yangu kwa maandamano makubwa na ya kutia fora pamoja wingi wa watu waliohudhuria sherehe hizi za siku ya Wafanyakazi Duniani.
 
Ndugu Wafanyakazi,
Kwa niaba ya Serikali nawapongeza Wafanyakazi wote kwa mchango wenu mkubwa katika kujenga uchumi wa nchi yetu. Ni ukweli usiopingika kwamba mishahara haitoshi na sehemu nyingine mazingira ni magumu.  Lakini, mnaendelea kuchapa kazi. Kuchelewa kwa Serikali kuongeza mishahara kusichukuliwe kwamba Serikali nia yake ni kuwadhalilisha Wafanyakazi hapana.

 Hilo haliwezekani. Uhusiano kati ya Serikali na Wafanyakazi ni sawa na samaki na maji. 

Serikali na Wafanyakazi, ni wabia katika kuujenga uchumi wa nchi hii.  Lakini tusiwasahau wenzetu walioko vijijini ambao ni asilimia 80 ya Watanzania wote.  Hawa wanatuzalishia chakula, wanatuzalishia mali ghafi za Viwandani,  wanatupatia fedha za kigeni kutokana na mazao yao.  Ni wabia muhimu sana katika kukuza uchumi wa nchi.  Kwa hiyo inapofika kugawana pato la Taifa hawa nao ni sehemu yetu.

Kwa hiyo tunapoitumia siku ya leo kudai haki zetu, tuitumie pia kila mmoja wetu kipekee, kujiuliza swali la Uwajibikaji.  Mimi nijiulize je, nawajibika katika nafasi yangu?

Na wewe jiulize, je unawajibika katika nafasi yako?  Unatakiwa ufanye kazi yenye tija kwa saa nane.  Kama unatumia pungufu ya saa hizo kwa kupiga soga, kuchati kwenye Whatsap, facebook au unawanyanyasa wananchi wanaohitaji huduma, unapoteza jalada la mtu ili akupe rushwa n.k. matendo haya yote unalipwa mshahara hata kama ni mdogo, mshahara huo si halali.  Unaihujumu nchi, na huu ni mfano mzuri wa ufisadi ambao Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kupiga vita.

Ndugu Wafanyakazi,
Serikali ya Awamu ya Tano kwa upande wake itaendelea kusimamia haki na kuupiga vita ufisadi, hivyo Wafanyakazi nao wajisafishe,   tubadilike sote.  Nchi hii itajaa neema kama kila mmoja atajituma, atakuwa muadilifu na sana sana akiwa na uzalendo kwa nchi yake. Kuongea na kukosoa hakuna ubaya, lakini kuna baadhi ya Wafanyakazi ni waongeaji sana, wakosoaji sana, na nadharia nyingi.

Natoa wito kwa Wafanyakazi wote tuamue kuwa watu wa vitendo, tena vyenye tija kwa mtu binafsi na kwa Taifa letu.  Natamani sana kuiona Mei Mosi inayosherehekewa kwa furaha na siyo ya manung’uniko.  Hilo linawezekana.  Kila moja akitimiza wajibu wake. Aidha, katika zoezi la kuwabaini watumishi hewa bado Mkoa wetu haujapata takwimu sahihi za watumishi hewa kutokana na takwimu hizo kubadilika siku hadi siku. Natambua kwamba kwa mazingira ya Mkoa wa dar es Salaam wapo watumishi wanaofanya kazi kwa ajira ya Serikali na pia katika Makampuni na Mashirika binafsi na wengine wakiendelea na shughuli zao za biashara wakati wakipokea mshahara wa Serikali bila kufanya kazi, natoa wito kwa wale wote wanaopokea mishahara isivyo halali wajisalimishe kwa sababu mkono wa sharia utachukua mkondo wake.

Ndugu Wafanyakazi,
Nimepokea kilio chenu ambacho kila mwaka tunapoadhimisha Sherehe hizi hutolewa, nacho ni kuhusu madai ya nyongeza za mishahara sambamba na kupunguziwa kodi ya mapato inayokatwa kwenye mishahara ya wafanyakazi. Naahidi suala hili lilifikishwa kwenye mamlaka zinazohusika na matokeo ya kodi hiyo imekuwa ikipungua mwaka hadi mwaka na hadi sasa kiwango kipo kuanzia asilimia 10-30.   Kuhusu nyongeza ya mishahara naomba tuvute subira Serikali kwa Watumishi wa Serikali kupitia Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma inalifanyia kazi suala hili pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu.   Kupitia Bunge linaloendelea na kikao chake huko Dodoma kwa sasa tuna hakika taarifa ya Serikali itatolewa na Waheshimiwa Mawaziri wenye dhamana na suala hili.

Ndugu Wafanyakazi,
Ipo changamoto ya uwasilishaji wa makato ya michango ya watumishi katika Mifuko ya Jamii. Ni kweli baadhi ya Taasisi na Halmashauri za Manispaa za Mkoa wa Dar es Salaam huchelewesha kupeleka michango katika Mifuko ya Hifadhi za Jamii. 
Naziagiza Taasisi zote zilizopo Mkoani kwangu kuhakikisha zinatekeleza wajibu wake wa kuwasilisha makato ya Wafanyakazi kwenye Mifuko husika.

Nawaomba Viongozi wa vyama vya Wafanyakazi katika kila Tawi la Chama cha Wafanyakazi kusimamia suala hili kwa karibu na kunipatia taarifa ili Ofisi yangu ichukue hatua stahiki kwa wale ambao hawatatekeleza agizo hili.

Ndugu Wafanyakazi,
Kuhusu mazingira magumu ya kufundishia hususan kwa Walimu, naziagiza Halmashauri za Manispaa za Dar es Salaam kuboresha mazingira ya Shule zake za Msingi na Sekondari, kwa kuhakikisha vimekuwepo vitendea kazi vya kutosha mfano meza za Walimu, viti, madawati na  vifaa vya maabara. Sambamba na upatikanaji wa vitabu vya ziada na kiada ambavyo kwa Mkoa wetu uwiano uliopo kwa sasa kwa upande wa shule za msingi ni 1:3 wakati uwiano kwa shule za sekondari ni 1:2 mpaka 1:1 kwa  masomo ya Sayansi lakini kwa masomo ya Sanaa na Biashara uwiano ni zaidi ya 1:5. Tunatarajia uwiano huu utapungua si muda mrefu baada ya mikakati inayofanywa na Mkoa ya kupata vitabu vya Sanaa. Hali hii ya upatikanaji wa vitabu vya ziada na kiada  kwa Shule za Msingi imeongeza  kiwango cha ufaulu kutoka asilimia 75% (mwaka 2014) mpaka asilimia 83:17 (mwaka 2015) ambapo kwa miaka minne sasa Mkoa wetu  ulishika nafasi ya kwanza Kitaifa ukiacha mwaka 2015 ambapo tumeshika nafasi ya pili kitaifa kwa matokeo ya Darasa la Saba (7). 

Nawapongeza sana Walimu kwa jitihada hizi sambamba na Wanafunzi kwa usikivu wao.

Ndugu Wafanyakazi,
Kuhusu elimu ya Sekondari, matokeo ya kidato cha nne yanaonyesha kwamba Mkoa wetu umeshuka kiwango cha ufaulu kutoka asilimia 73% mwaka 2014 mpaka asilimia 68.77 mwaka 2015 ambapo Mkoa ulishika nafasi ya kumi na tano (15) ukilinganisha na ufaulu wa mwaka 2014 ambao Mkoa ulishika nafasi ya nane (8) kitaifa. Kwa matokeo hayo ni dhahiri tunayo changamoto ya kupambana na yale yanayoshusha viwango vya ufaulu kwa wanafunzi hawa na tuwajengee mazingira mazuri ya kujifunza na kufundishia kwa Walimu.

Ndugu Wafanyakazi,
Kwa ujumla Mafanikio yaliyofikiwa na Mkoa katika kutekeleza Mkakati wa Matokeo Makubwa Sasa BRN ni pamoja na Kupandisha ufaulu katika Mitihani yote ya Taifa ya Darasa la Nne, Kidato cha Pili, Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi isipokuwa Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne.

Kuhusu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi bado hakuna hata Wilaya moja iliyofikia lengo la BRN. Hapa lazima tukae kwa pamoja tutafakari kwa nini hatufikii lengo la BRN ingawa Mkoa wetu umekuwa ukishika nafasi ya kwanza kwa ufaulu Kitaifa mfululizo tangu mwaka 2011 hadi 2014.

Mafanikio mengine tuliyoyafikia ndani ya BRN ni shule zote za Msingi na Sekondari kupatiwa Kiongozi cha Mkuu wa Shule ambacho kinawawezesha kuwa na uongozi bora katika shule.  Pia jumla ya Walimu 467 wa shule za Sekondari wamepewa Mafunzo ya kujenga uwezo katika masomo ya Hisabati, English Language, Kiswahili na Biolojia. Walimu 1,688 wa Shule ya Msingi wamepewa mafunzo ya kuwajengea uwezo katika masomo ya Hisabati, English Language na Kiswahili.

Shule za Serikali za Sekondari 135 zote zina maabara na wanafunzi wanajifunza, masomo ya Sayansi kwa nadharia na vitendo.

Ndugu Wafanyakazi
Kuhusu madai ya Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari, madai yaliyohakikiwa na kuwasilishwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa ajili ya kuombewa fedha ni jumla ya kiasi cha Shs.3,528,046,426.20 ambapo zimegawanyika kama ifuatavyo:-



Shule za Msingi:
·        Madai ya Walimu waliostaafu ambao ni 157 ni TSh.350,080,288.06.
·        Madai ya Walimu 1,912 waliopandishwa madaraja ni TShs.1,553,000,415.14.
·        Madai ya walimu yasiyotokana na mishahara (likizo, matibabu, masomo, usumbufu, posho ya kujikimu na uhamisho) ni TSh.1,312,002,182.00.
Shule za sekondari:
·        Madai ya Walimu waliostaafu ambao ni 28  TSh.86,514,196.00. Jumla ya Shs. 3,215,082,885.20
·        Madai ya Walimu 1,009 waliopandishwa madaraja ni TSh.62,027,544.00.
·        Madai ya Walimu yasiyotokana na Mishahara ni TSh.164,421,800.00. Jumla Shs. 312.963,540.00

Kwa kifupi, madai yote haya niliyoyataja yanashughulikiwa na Serikali, tunayo matarajio kuwa yatalipwa kulingana na upatikanaji wa fedha Serikalini.  

Ndugu Wafanyakazi,
Kwa mwaka wa fedha 2015/16 mwezi Desemba hadi Februari, Halmashauri za Manispaa za Mkoa wa Dar es Salaam zilipokea fedha TSh.2,652,289,000.00 kama ruzuku ya uendeshaji wa Shule za Msingi na Sekondari katika Mpango wa Elimu bila malipo ulioanza kutumika Januari 2016. Huu ni muendelezo wa utekelezaji wa ahadi ya Mhe. Rais wakati wa Kampeni ya Uchaguzi Mkuu uliomalizika mwaka jana wa kutoa elimu bure bila malipo.

Kwa ujumla maendeleo yaliyofikiwa na Mkoa wa Dar es Salaam kielimu ni makubwa sasa wakati huu na ni muendelezo tulioachiwa na  Uongozi wa awamu ya Nne.      

Mafanikio tunayoyatathmini sasa ni mwendelezo wa juhudi zilizoanza tangu mwaka 2005. Kwa mfano mwaka 2004 kulikuwa na shule za Sekondari za Serikali 28 tu katika Mkoa wa Dar es Salaam, lakini leo zipo shule za Sekondari za Serikali 137. Wanafunzi waliochanguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule za Serikali za Mkoa wa Dar es Salaam walikuwa 21% ya waliofaulu, lakini kuanzia mwaka 2011 hadi 2015 Wanafunzi walichaguliwa kujiunga na Kidato cha kwanza katika Shule za Serikali kwa asilimia 100%. Hivyo kwa Mkoa wa Dar es Salaam kila mhitimu wa Darasa la Saba anayo fursa ya kusoma Sekondari ili mradi tu afaulu mtihani.

Pamoja na Mafanikio hayo changamoto zilizobaki kwa upande wa Elimu ni pamoja na upungufu wa vyumba vya madarasa 7,514 Shule za Msingi na Sekondari madarasa 803, Matundu ya vyoo 16,610 kwa Shule za Msingi na Sekondari  matundu 3,586 na Madawati 66,301 wa Shule za Msingi na
Sekondari, meza 27,729, viti 25,590 na Makabati 1,735.

Hivyo natumia fursa hii kuwaomba Wadau wetu wakiwemo wafanyakazi wote wenye mapenzi mema kuungana nasi katika kukabiliana na changamoto hizi ambazo ni kikwazo katika utoaji wa Elimu Bora katika Mkoa wetu.

Ndugu Wafanyakazi,
Kwa ujumla nimezipokea changamoto zote kama mlivyoziainisha kwenye risala yenu na nitahakikisha nazifikisha kwenye mamlaka mbalimbali zinazohusika ili zifanyiwe kazi na  nina matumaini Mei Mosi ijayo ya mwaka 2017 iwe yenye neema kwa wafanyakazi, kwani si vizuri kila tunapokutana Wafanyakazi wanalalamika kuhusu maslahi.

Naomba nichukue fursa hii kuwapongeza Wafanyakazi wote kwa michango yao ambayo wamekuwa wakichangia kama Wazazi. Michango hii kwa kiasi kikubwa imeleta mafanikio haya tunayoyaongelea leo katika sekta ya Elimu kwenye Mkoa wetu. 

Naomba jitihada hizi ziendelezwe ili watoto wetu wapate elimu bora kwa manufaa ya taifa letu. Hivi karibuni tutazindua Kampeni Kabambe ya Uchangiaji wa Madawati na vyumba vya madarasa ambayo itarushwa hewani moja kwa moja na luninga ya Channel Ten ambapo wadau mbalimbali tumewaomba kuchangia kupitia namba za simu za Mkononi ambazo zitakuwa zikitangazwa na Kituo hiki cha Televisheni. Naomba wafanyakazi wote mtuunge mkono kwa kuchangia fedha ili kukabiliana na upungufu huu wa madawati na madarasa uliopo katika Shule zetu za Msingi.

Ndugu wafanyakazi,
Jiji la Dar es Salaam kwa sasa linakabiliwa na changamoto kadhaa. Mfano mafuriko kwa wenzetu waliojenga maeneo hatarishi ya mabondeni, msongamano wa magari, barabara mbovu, uchafu, uhaba wa maji, mirefeji ya maji ya mvua kuziba n.k. Serikali inafanya jitihada kuzishughulikia baadhi ya changamoto zilizopo mfano:  Barabara na mifereji ili kupunguza msongamano ambao ni tatizo kubwa. 

Ndugu Wafanyakazi,
Serikali ipo mbioni kulipatia ufumbuzi tatizo la usafiri kwa Wafanyakazi na Inshaallah Mwenyezi Mungu akitujalia mwezi ujao mradi wa mabasi makubwa yaendayo kasi ujulikanao kama Dar es Salaam Rapid Transport (DART) ambao unasimamiwa na Ofisi ya Rais -  TAMISEMI utaanza rasmi.

Lengo la mradi huu ni kuyaondoa mabasi madogo ya dala dala ambayo yanaleta msongamano mkubwa na kuingiza mabasi makubwa yenye kubeba abiria wengi lakini yenye Watumishi walio na nidhamu waendeshapo vyombo hivi.  Ni matarajio ya Serikali mradi huu utakapoanza tutapunguza kero za usafiri katika Jiji  na msongamano wa magari.

Ndugu Wafanyakazi,
Changamoto nyingine tuliyonayo ni ile Uchafuzi wa Mazingira, Usafi ni tabia.  Watu wengi katika Jiji letu hawana tabia ya usafi.

Taka wanazozalisha wanazitupa ovyo na hata kwenye mifereji na husababisha kuziba.  Serikali inalaumiwa, kwa nini na wachafuzi hao wasijilaumu kwa vitendo vyao hivyo visivyo vya kistaarabu?  Naomba wananchi waige mfano wa wenzetu wa Manispaa ya Moshi, wenzetu wameonyesha nia thabiti ya kuchukia uchafu na mji wao ni msafi.  Kwanini sisi tuwe wachafu? Naomba kila mmoja wetu awe mlinzi wa mwenzake katika kuhakikisha Jiji letu linakuwa safi.  Jana tarehe 30/04/2016 tumezindua Kampeni Kabambe ya usafi katika Jiji letu  la Dar es Salaam.  Nina hakika Kwa muda mfupi ujao tunatarajia Jiji letu kuwa mfano wa kuigwa kama lilivyo Jiji la Kigali nchini Rwanda.

Kampeni hii ilishirikisha makundi mbalimbali ya wananchi, wazee kwa vijana, akina mama na akina baba. Wote hawa wamekemea suala la uchafuzi wa Jiji letu. Kampeni hiyo ina kauli mbiu ya “USAFI NI KUPIMO CHA USTAARABU”  Kwa umoja wetu na kila mmoja kuwa Balozi wa Kampeni hii.
Aidha, tunatarajia Kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa Sheria kwa watakaochafua mazingira na zawadi nono zitatolewa kwa watakaowakamata watu wanachafua mazingira kwa makusudi. Natoa wito kwa wananchi kuunga mkono jitihada hizi na kutii Sheria bila Shuruti.

Ndugu Wafanyakazi,
Nitumie nafasi hii pia kuendelea kukumbushana juu ya umuhimu wa kujikinga na maambukizo ya virusi vya UKIMWI kwani bado ni changamoto katika Mkoa wetu, hivyo wote tuchukue tahadhari. Kwa kumalizia, nawapongeza Wafanyakazi wote ambao mtawapa zawadi mbalimbali.  Zawadi hizo ziwape moyo wa kufanya kazi kwa bidii zaidi na tija.

Wale ambao hawatatunukiwa leo nina hakika wametoa mchango mkubwa sana kwenye mafanikio ya hawa wenzao.  Wasife moyo, wachape kazi. Nawashukuru sana na sasa niko tayari kutoa  zawadi hizi.


Ahsanteni kwa kunisikiliza. 

No comments:

Post a Comment