Kufuatia utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa
kupanda miti kutunza Mazingira na Kuhifadhi Vyanzo vya Maji, Serikali kupitia
Ofisi ya Makamu wa Raisi Muungano na Mazingira, imetekeleza ahadi yake ya
kugawa miche ya miti ya matunda Mkoani Simiyu katika Majimbo ya ya Uchaguzi ya Busega,
Bariadi, Itilima, Kisesa, Meatu, Maswa Mashariki na Maswa Magharibi.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Raisi (Mazingira), Mhe. Luhaga
Mpina, amechangia miti ya matunda ya maembe na machungwa ipatayo Elfu Kumi
(10,000) huku, Halmashauri na Wabunge wa Mkoa huo ,wamechangia idadi ya miche
inayozidi Elfu Kumi na Tatu (13,000).
Kwa kuanzia idadi ya miche ya miti ya matunda
ipatayo Elfu Kumi na Tatu Mia Sita Sitini na Sita,(13,666) imeshapelekwa Mkoani
simiyu ikiwa ni miti ya maembe Elfu Kumi na Tatu na Mia Tano Sitini na Sita
(13,566) na Michungwa Mia Moja (100).
Awali, Mhe. Mpina akitoa ahadi hiyo alisema, Mkoa
wa Simiyu hauna miti ya matunda ya kutosha hivyo Mkakati wa upandaji miti ya
matunda utasaidia chakula kwa familia, fedha kwa kuuza matunda na malighafi kwa
viwanda nchini na kusema kuwa miti ni Mali na miti ni uchumi.
Aidha, Ofisi ya Makamu wa Rais inamshukuru Mhe. Daudi
Njalu Silanga (Mb). wa Itilima, kwa kujitolea usafiri wa kusafirisha miche hiyo
kutoka Chuo cha Kilimo cha Sokoine kilichopo Mkoani Morogoro.
Idadi ya miche elfu ishirini na saba (27,000)
inatarajiwa kugawanywa katika majimbo hayo, ikiwa ni pamoja na michango ya
wabunge wa majimbo hayo.
Kupitia Mkakati huo wa Kitaifa wa kupanda miti na
kuhifadhi vyanzo vya Maji, Serikali pia imewataka wananchi kushiriki kikamilifu
katika kutunza mazingira na hususan wananchi wa Simiyu kuitunza miti hiyo ya
muda mfupi, ili kuiepusha nchi na hali ya jangwa na ukame.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO
SERIKALINI OFISI YA MAKAMU WA RAIS


No comments:
Post a Comment