TANGAZO


Thursday, March 24, 2016

Wakuu wa mitihani Kenya wafutwa kazi

Nkaissery  
Waziri Nkaissery amesema watakaopatikana na hatia wataadhibiwa
Serikali imewafuta kazi maafisa wakuu wa Baraza la Mitihani Kenya (KNEC) kutokana na visa vya udanganyifu vilivyoripotiwa wakati wa mitihani ya kitaifa mwaka jana.
Bw Kivilu pamoja na maafisa wengine saba wa baraza hilo wametakiwa kuandikisha taarifa kwa polisi mara moja.
Tangazo la kufutwa kwa wakuu hao limetolewa kwenye kikao cha wanahabari kilichoandaliwa na Waziri wa usalama na masuala ya ndani Meja Jenerali Joseph Nkaissery na Waziri wa Elimu Fred Matiang’i.
Matiang'i Bw Matiang'i
Bw Nkaissery amesema hatua zitachukuliwa dhidi ya waliohusika katika uadanganyifu huo.
Watahiniwa waliopatikana na makosa ya udanganyifu mtihani wa kidato cha nne mwaka 2015 waliongezeka asilimia 70 kutoka mwaka uliotangulia.
Katika mtihani wa mwaka 2015, watahiniwa 5,101 waligunduliwa kuwa walitumia udanganyifu katika mtihani.
Mwaka 2014, ni watahiniwa 2,975 pekee waliokuwa wametumia hila katika mtihani huo wakati huo visa vikiwa vimepungua kutoka visa 3,812 mwaka 2013.
Aliyekuwa naibu chansela wa chuo kikuu cha Nairobi Prof George Magoha ameteuliwa kuwa mwenyekiti mpya wa bodi hiyo na ataanza kufanya kazi mara moja.
Muda mfupi baada ya tangazo la kufutwa kwa wakuu hao kutolewa, Wakenya kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa wakieleza hisia zao na kitambulisha mada #KNEC kimeanza kuvuma.

No comments:

Post a Comment