TANGAZO


Tuesday, March 22, 2016

UNFPA yakabidhi vifaa tiba Vyuo na Taasisi za Afya nchini.


Mwakilishi wa Shirika la UNFPA nchini Natalia Kanem (aliyesimama) akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo ya kutumia simu kwa ajili ya kufundisha wakunga na wauguzi njia ya uzazi salama, waliokaa kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali) Dkt. Otilia Gowele, Msajili wa Baraza la Uuguzi Lena Mfalila na Geeta Lal kutoka makao makuu ya UNFPA. (Picha zote na Lilian Lundo-Maelezo)


Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Dkt. Otilia Gowele akitoa hotuba ya ufunguzi wa mafunzo kuhusu uzazi salama kwa njia ya simu kwa wawakilishi wa Vyuo vya Afya nchini pamoja na Taasisi zinazoshughulikia afya ya mama na mtoto,  waliokaa meza kuu kutoka kulia ni Nayanesh Bhandutia kutoka makao makuu ya UNFPA, Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo ya Wauguzi na Wakunga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto  Ndementria Vermand, Mwakilishi wa Shirika la UNFPA nchini  Natalia Kanem, Msajili wa Baraza la Uuguzi Lena Mfalila na Geeta Lal kutoka Makao Makuu ya UNFPA.


Wawakilishi kutoka Vyuo vya Afya na Taasisi zinazojihusisha na uzazi salama nchini  wakifuatilia mafunzo ya uzazi salama kwa kutumia teknolojia mpya ya simu.


Geeta Lal kutoka Makao Makuu ya UNFPA akitoa maelekezo kwa washiriki (hawapo pichani) kuhusu mafunzo ya uzazi salama ambayo yanapatikana ndani ya simu hiyo.


Mkuu wa Chuo cha Uuguzi Newala Tecla Ungele (wa kwanza kulia) akipokea seti ya simu ya kufundishia uzazi salama kutoka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Otilia Gowelle , wa kwanza kushoto ni Mwakilishi wa Shirika la UNFPA nchini Natalia Kane.


Mwalimu wa Uuguzi Asha Ally Khamis (wa pili kulia) kutoka Chuo cha Afya Mbweni Zanzibar akipokea simu ya kufundishia uzazi salama kutoka kwa Natalia Kanem, wa kwanza kushoto ni Mwakilishi wa Shirika la UNFPA nchini na Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Dkt. Otilia Gowelle, kulia ni Nayanesh Bhandutia kutoka makao makuu ya UNFPA.


Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Otilia Gowelle akipokea simu ya kufundishia uzazi salama kutoka kwa Mwakilishi wa Shirika la UNFPA Natalia Kanem (katikati) huku wakishuhudiwa na Geeta Lal kutoka makao makuu ya UNFPA.


Washiriki wa mafunzo ya uzazi salama wakifuatilia kwa makini mafunzo kwa vitendo, kutoka kushoto ni Mkufunzi Chuo Kikuu cha Muhimbili  Dkt. Thecla Kohi, Mratibu wa Mafunzo ya Wauguzi na Wakunga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Vumilia Mmari na Annamagreth Mukwenda kutoka taasisi ya MCSP (Maternal and Child Survival Program)


Washiriki wa mafunzo ya uzazi salama kwa kutumia simu wakifuatilia jambo kwa umakini kutoka kwa mwezeshaji (hayupo pichani) wa mafunzo hayo.



Na Lilian Lundo-MAELEZO
Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNFPA) limekabidhi simu za kufundishia huduma ya uzazi salama kwa vyuo vya Afya pamoja na taasisi zinajihusisha na masuala ya afya ya mama na mtoto ili kuboresha huduma kwa akina mama wajawazito na watoto wanaozaliwa.

Makabidhiano hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam Machi 21, 2016 baina ya shirika la UNFPA na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Akikabidhi vifaa hivyo Mwakilishi wa Shirika la UNFPA nchini Natalia Kanem alisema wanashirikiana na Serikali ya Tanzania katika kukuza na kuboresha elimu juu ya uzazi salama na kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.

“Dhumuni la matumizi ya simu za kufundishia uzazi salama ni kutoa elimu kwa wauguzi na wakunga walioko vijijini na maeneo ambayo hayafikiki kwa urahisi ili kuwasaidia kupata elimu ya uzazi salama na kupunguza vifo vya mama na mtoto,” alisema Natalia.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Otilia Gowele ambaye alimwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali alisema kuwa simu hizo zitarahisisha ufundishaji kwa wauguzi na wakunga kwani zitawawezesha kujifunza masuala yote yanayohusu uzazi salama bila kuondoka kwenye vituo vyao vya kazi.

Dkt. Gowele aliongeza kwa kusema kuwa, simu hizo zitakuwa na mafunzo ya uuguzi ambayo yako katika mitaala ya vyuo vya uuguzi na mtumiaji wa simu hiyo anaweza kuuliza swali lolote linalohusu uzazi salama akapata majibu kwa njia ya sauti, picha na maandishi.
Aidha, simu hizo zinachajiwa kwa kutumia umeme wa mwanga jua, umeme wa wakawaida na inatumia betri pia, hivyo inaweza kutumika hata maeneo ambayo bado hayajafikiwa na umeme.

Kwa upande wake Mtaalamu wa Afya ya Mama na Mtoto wa UNFPA Felister Bwana alisema kuwa, simu hizo zimegawiwa kama majaribio kwa baadhi ya vyuo vya Afya na na taasisi zinazojihusisha na uzazi salama, endapo teknolojia hiyo italeta mafanikio yanayotarajiwa simu hizo zitagawanywa kwa vyuo vyote vya uuguzi na hospitali nchini.

Vyuo na taasisi ambavyo vimepokea vifaa hivyo ni pamoja na Chuo cha Afya Kilosa, Bugando, Newala, Nachingwea, Bagamoyo, Geita, Kahama, Maswa, Sengerema, KCMC, Zanzibar, Ifakara pamoja na taasisi ya TAMA na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Kwa mujibu ya sensa ya mwaka 2010, jumla ya vifo 454 vimekuwa vikitokea  katika kila vizazi hai 100,000 kwa mwaka, idadi hiyo imepungua na kufikia vifo 432 kwa kila vizazi hai 100,000 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012.

No comments:

Post a Comment