Na
Jacquiline Mrisho- MAELEZO
MAMLAKA ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka wananchi wenye malalamiko yanayohusu huduma
zitolewazo na makampuni ya simu kutosita kupeleka malalamiko yao kwenye makampuni
husika.
Meneja Mawasiliano wa
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Bw. Innocent Mungy ameyasema hayo leo
jijini Dar es salaam katika mahojiano maalumu alipokua akijibu swali kuhusu
malalamiko ya wananchi juu ya huduma zinazotolewa na makampuni mbalimbali ya
simu hapa nchini.
Amesema mteja ana wajibu
wa kujua matumizi na gharama za huduma za mitandao anazotumia pia ana haki ya
kutoa malalamiko kwa kampuni husika ili aweze kupatiwa majibu na endapo hatasikilizwa
anaruhusiwa kuwasiliana malalamiko yake Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania.
Bw. Mungy ameongeza
kuwa,wananchi wanaweza kufikisha malalamiko yao TCRA kwa kupiga simu au kutuma
ujumbe mfupi kwenda namba 0784558270 au barua pepe; malalamiko@tcra.go.tz
na malalamiko hayo yatafanyiwa kazi haraka.
Aidha, amefafanua
kwamba,TCRA haipangi bei elekezi kwa makampuni hayo hivyo gharama za
mawasiliano ziko kwenye mifumo mbalimbali kutegemeana na gharama za uendeshaji
wa huduma kwenye kampuni husika.
“Mwananchi halazimishwi kutumia huduma ya
mtandao mmoja wa simu ana uhuru wa kuchagua na kutumia mtandao wowote wenye
unafuu kwake” Amesisitiza.
Amewaomba wananchi waelewe
kwamba soko la makampuni ya simu limekuwa na ushindani mkubwa jambo
linaloyalazimisha makampuni yanayotoa huduma kubuni ofa mbalimbali kwa lengo la
kuvutia wateja.
“Sasa hivi soko la
makampuni ya simu limekuwa na ushindani mkubwa nchini, jambo linalofanywa na
makampuni hayo ni kuweka ofa mbalimbali ambazo hizo huwasaidia wananchi kupunguza
gharama za matumizi ya simu”.
No comments:
Post a Comment