TANGAZO


Sunday, March 20, 2016

Balozi Seif Iddi akipiga kura uchaguzi wa marudio jimboni kwake Kitope Wilaya ya Kaskazini B Unguja

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  ambae pia ni mgombea wa nafasi ya Uwakilishi wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akisubiri kukabidhiwa karatasi za kupigia kura ili atumie haki yake ya Kidemokrasia kumchagua kiongozi anayemtaka. (Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)
Balozi Seif Ali Iddi Mgombea nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar akipiga kura  kwenye uchaguzi wa marejeo hapo kwenye kituo chake Skuli ya Sekondari Kitope Wilaya ya Kaskazini “B” Mkoa wa Kaskazini Unguja. 
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Mama Asha Suleiman Iddi akijibu maswali ya mwanahabari wa Kituo cha Matangazo cha Cloud FM mara baada ya kumaliza kupiga kura kwenye kituo chake hapo skuli ya sekondari ya Kitope. 

Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
20/03/2016.
KITENDAWILI cha uchaguzi Mkuu wa Zanzibar kilichotegwa kufuatia Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Bwana Jecha Salum Jecha kutangaza kufuta uchaguzi  na matokeo yake yote mnamo Tarehe 28 Oktoba mwaka 2015 siku tatu baada ya uchaguzi  Mkuu  wa Tarehe 25 Oktoba kutokana na sababu Tisa Kuu hatimae kimeteguka.

Kuteguka huko kumekuja baada ya Wazanzibar kupata fursa ya kuitumia  haki yao ya kidemokrasia ya kupiga kura katika uchaguzi wa marejeo kwa kumchagua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Mwakilishi wa Jimbo pamoja na Diwani wa Wadi.

Uchaguzi huo wa marejeo  unaosimamiwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar { ZEC }umetoa nafasi kwa Wananchi wa  Zanzibar kukamilisha kupiga kura kwa nafasi  Tano ambazo zile za awali tayari wameshachagua Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge.

Kwa wapiga kura wa upande wa Tanzania Bara  waliokuwa chini ya usimamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi { NEC } wameshawajibika kupiga kura  kwa nafasi Tatu kwa kuwachagua Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mbunge pamoja  na Diwani.

Viongozi mbali mbali pamoja na maelfu ya wananchi walijitokeza mapema asubuhu kupiga kura ili kutimiza  kiu yao iliyowashika tokea kutangazwa kufutwa kwa uchaguzi pamoja na matokeo yake Oktoba mwaka uliopita.

Misururu mirefu ya Wananchi  iliyowekwa kwa mujibu wa mfumo wa majina ya wapiga kura  yaliyobandikwa vituoni kwa takriban wiki moja kabla ya uchaguzi ilianza mapema alfajiri  mara tuu baada ya kumalizika kwa Ibada ya sala ya Asubuhi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi wao pamoja na wananchi wengine wakapiga kura katika Kituo chao cha Skuli ya Sekondari ya Kitope Jimbo la Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja mnamo saa 2.4 za asubuhi.

Balozi Seif  ni mgombea wa nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi { CCM } katika Jimbo jipya la Mahonda badala ya lililokuwa Jimbo la Kitope kufutwa kufuatia  mfumo mpya wa mabadiliko wa maeneo kutokana na ongezeko la idadi ya watu kwa mujibu wa Sensa ya Idadi ya watu na Makaazi ya mwaka 2012.

Akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kupiga kura Balozi Seif  alisema ameridhika na zoezi zima liloanza mapema asubuhi ambapo wananchi mbali mbali tayari wameshatumia haki yao ya kupiga kura na kurejea nyumbani kuendelea na shughuli zao za kimaisha.

Balozi Seif alisema hali ni shwari, utulivu na isiyo na bvughdha iliyowawezesha wananchi kujitokeza kwa wingi kuitumia haki yao ya Kidemokrasia ya kuwachaguwa viongozi watakaowasiamamia katika harakatri zao za Maendeleo.

Alionyesha matumaini yake kwamba zoezi la upigaji kura lililoanza mapema asubuhi litaendelea na kumalizika kwa amani na utulivu na kuwaomba wananchi walioko majumbani kujitokeza kwenda kupiga kura.

Akizungumzia kasumba za baadhi ya vyombo vya Habari na Mitandao ya Kijamii vinavyodai hali ya Zanzibar ni tete tokea kufutwa kwa uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka uliopita Balozi Seif  alisema nchi zisizo na amani zinaeleweka na kujuilikana kupitia vyombo hivyo hivyo vinavyoe;ezea kasumba hiyo.

Aliwahakikishia wananchi, wageni na watalii kwamba Zanzibar ina amani inayotoa fursa kwa wageni kuendelea kumiminika bila ya hofu kiasi kwamba sekta ya utalii bado haijatetereka kufuatia kasumba za baadhi ya vyombo vya Habari ndani na hata nje ya nchi.

Kupitia mahojiano hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewatoa hofu wananchi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imejitahidi katika kuona hali ya amani inaendelea kutengamaa.

Mmoja kati ya wapiga kura katika kituo cha kupiga kura cha Skuli ya Sekondari ya Kitope ambae alikataa kutaja jina lake alisema ameridhika na maandalizi mazuri yaliyofanywa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa kuwapa fursa wananchi kutekeleza haki yao kupiga kura katika misingi ya utulivu.

Alisema yule mwananchi atakayefikia maamuzi ya kutaka kuilaumu Tume ya Uchaguzi ajijue kwamba ana matatizo mwenyewe kwa kile alichokieleza kwamba fursa ilitolewa mapema kwa wananchi kuhakiki majina yao katika vituo vyao vya kupiga kura wiki nzima kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wenyewe.

Moja kati ya jambo lililoleta faraja kubwa ndani ya zoezi zima la upigaji kura ni ile hali ya amani miongoni mwa wapiga kura katika vituo mbali mbali vya wapiga kura Mjini na Vijijini.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein aliendelea na kiti cha urais wa Zanzibar  kwa miezi Mitano baada ya Tarehe 25 Oktoba mwaka 2015  kufuatia Tume ya Uchaguzi Zanzibar  { ZEC } kutomtangaza mshindi wa kiti cha nafasi ya urais wa Zanzibar kutokana na kasoro nyingi zilizojitokeza kwenye zoezi la upigaji kura.

Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984  kifungu cha 28{1}{a}kilikuwa na nguvu ya kumpa uwezo Rais aliyepo madarakani kuendelea na madaraka ya Urais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la M apinduzi.

No comments:

Post a Comment