Ofisa Mdhamini wa ZSTC Pemba Abdulla Ali Ussi (kulia), akitoa maelezo baada ya Magunia
ya Karafuu Kavu kukamatwa na Kikosi cha KMKM katika Ufukwe wa Bahari ya
Chanjaani Mtambwe ambazo zilikuwa katika harakati za kutaka
kusafirishwa kwa njia ya Magendo. Anaemsikiliza ni Kamanda wa KMKM zone ya Pemba, Silima Hija Hija.
Baadhi
ya Wafanyakazi wa Shirika la ZSTC wakipita mbele ya Rais Mhe. Dkt. Ali
Mohmaed Shein wakiwa wamebeba bango lenye ujumbe wa kupinga magendo ya
zao la karafuu katika maazimisho ya siku ya Wafanyakazi duniani, Mei
Mosi 2015
Magendo ni vitendo viovu vinavyohusisha uingizaji
au usafirishaji wa bidhaa au mazao kwa njia zisizo halali/kisheria kwa lengo la
kukwepa kodi na kukiuka sheria ambapo ni njia haramu ya kufanya biashara.
Sababu kuu za magendo ni tamaa ya utajiri, ujinga na kukosa uzalendo.
Ni dhahiri kuwa magendo yana athari kubwa kwa
maendeleo ya nchi na Wananchi wake, huikosesha serikali mapato ambayo ndio
yanayohitajika katika kuimarisha huduma za jamii kama vile utoaji wa elimu, afya,
maji safi na salama, ujenzi wa miundombinu ya barabara na huduma nyengine
muhimu.
Karafuu ni zao kuu la uchumi wa Zanzibar linalosaidia upatikanaji
wa fedha za kigeni na kuiwezesha Serikali kuimarisha huduma za jamii. Katika
kipindi cha miaka ya 1980 na 2010 zao hili lilikuwa katika changamoto kubwa ya kusafirishwa
kwa magendo. Baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu walikuwa wakisafirisha zao hili
kwa magendo kwenda katika nchi za jirani.
Katika wakati huo
usafirishaji magendo wa zao la karafuu ulikuwa mkubwa kiasi cha kuzifanya nchi
hizo za jirani kuwa wauzaji wakubwa wa zao la karafuu kwa zaidi ya tani 2,000
katika soko la dunia huku ikizingatiwa kuwa katika nchi hizo hakuna mikarafuu
inayolimwa.
Wakati nchi hizo
zikionekana kuuza karafuu kwa kiwango hicho, uzalishaji
wa zao hilo kwa Zanzibar ulishuka kutoka tani 9,952 hadi tani 2673 katika
kipindi cha miaka kumi, sababu moja ikiwa ni karafuu za Zanzibar kusafirishwa
kwa magendo kwenda katika nchi hizo za jirani.
Katika kipindi hicho cha mwaka 2000 hadi 2010, Zanzibar ilipoteza
kiasi cha dola za kimarekani milioni 16, sawa na TZS bilioni 34.7 kutokana na
usafirishaji karafuu kwa magendo.
Kwa mujibu wa sheria ya ZSTC ya mwaka 2011 kifungu cha 9
(a) Wakulima na Wafanyabiashara wa zao hilo la karafuu wanatakiwa kuuza karafuu
zao Serikalini tu kupitia Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) ambayo
ni taasisi pekee iliyopewa mamlaka ya kununua na kuuza karafuu, hivyo kufanya
magendo ya karafuu ni makosa.
Kulikuwa
na sababu nyingi zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya watu ikiwemo suala la bei
ya karafuu kuwa ndogo na kusababisha watu kuamua kuziuza karafuu zao kimagendo
nje ya nchi kwa lengo la kutafuta bei nzuri.
Kwa lengo la kuimarisha, kulinda ubora na kuwahamasisha Wakulima
kuuza karafuu zao Serikalini kupitia vituo vya ununuzi vya ZSTC badala ya
kusafirisha kwa magendo, mikakati mbali mbali ilipangwa na kutekelezwa na
Serikali.
Mwaka 2011 Serikali ilitoa ahadi na kuitekeleza ahadi hiyo ya kuwalipa Wakulima
wa zao la karafuu asilimia 80 (80%) ya bei ya karafuu ya soko la dunia. Karafuu
za daraja la kwanza zinanunuliwa kwa bei ya TZS 14,000 kwa kilo badala ya TZS
5,000 kwa kilo, bei iliyokuwepo mwaka 2010. Ongezeko hili ni sawa na
asilimia 180.
Kadhalika, vituo vipya vya ununuzi na uuzaji wa karafuu vimejengwa,
vituo vya zamani vimekarabatiwa ambapo idadi kamili ya vituo vyote ni 35 Unguja
3 na Pemba 32, huduma zote muhimu zimeimarishwa kwenye vituo hivyo na ulinzi
pia umeimarishwa zaidi katika kudhibiti magendo.
Mkakati mwengnie uliochukuliwa ni kwa Shirika la ZSTC kujipanga
vyema katika suala la upatikanaji wa kifedha kwa wakati na kulipa fedha taslim
kwa Wakulima wa zao la karafuu na kuhakikisha hakuna Mkulima anaekopwa karafuu zake
anapokwendwa kuuza.
Utekelezaji
wa mikakati hiyo imesaidia sana kufanikiwa kudhibiti magendo ya karafuu, hivi
sasa Wananchi wanauza karafuu zao katika vituo vya ununuzi vya ZSTC. Ni jambo
la kuwashukuru na kuwapongeza Wakulima, Wananchi na Vikosi vya Ulinzi na
Usalama kwa kazi nzuri walioifanya ya kushirikiana na Serikali katika kupambana
na magendo ya karafuu.
Pamoja
na mikakati na jitihada hizo zilizochukuliwa na Serikali kudhibiti magendo
ya karafuu kufanikiwa kwa kiwango
kikubwa lakini inaonekana kuwa bado wapo watu wachache wanaendeleza biashara
hiyo haramu. Katika msimu wa mavuno mwaka 2015/2016 gunia 33 za karafuu kavu na
gunia 31 za makonyo zimekamatwa ambazo zilikuwa zinasafirishwa nje.
Lakini kabla Mkulima hajafikiria suala la kuuza karafuu
zake kwa njia ya magendo, anapaswa kwanza ajiuulize masuali yafuatayo;-
Ni nini anachotaka zaidi ilhali karafuu zimeongezwa bei
na bei hiyo ni kubwa zaidi ya huko anakokwenda kuuza kwa magendo?
Pia kwa nini anafanya magendo llhali pamoja na bei nzuri
lakini pia faida ya karafuu ikirudishwa ndani ya nchi ndio hupatikana elimu bora
kwa mwanawe, afya bora kwake, barabara nzuri kwa wote, maji safi kwa kila mtu
na maendeleo kadhaa wa kadhaa?
Inakuwaje mtu anajitia katika magendo ya karafuu ilhali uwezekano
wa kupoteza maisha yake ni mkubwa au uwezekano wa kukamatwa na kufungwa na
kupoteza utumishi wake kwa familia yake na kuitia katika mateso, kwa nini
anafanya hivyo?
Ni kwa sababu gani za msingi watu ambao wanauwezo wa
kupata kiasi kikubwa cha fedha kwa kuuza karafuu zao serikalini waingie katika
tombola ya kukosa kabisa kwa kujaribu kuingia kwenye magendo na kuhatarisha
mali zao kwa kuzama baharini au kufilisiwa na kubaki katika umaskini kwa kukosa
fedha za Serikali na zile ambazo walizitarajia kuzipata kwa kuuza magendo huko
nchi za jirani?
Ni wazi kuwa anachokosa mtu huyo ni uzalendo na uwezo
mzuri wa kufikiri.



No comments:
Post a Comment