TANGAZO


Sunday, January 10, 2016

Balozi Seif Iddi aweka jiwe la msingi Soko la Matunda, Ofisi za Baraza la Mji Wete Pemba

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwasili katika katika Soko la Matunda la Mji wa Wete kuweka jiwe la msingi la ujenzi wake ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1864.
Mkurugenzi wa Baraza la Mji wa Wete Kisiwani Pemba Nd. Amageni Othman mwenye suti ya rangi ya kisamli akimtembeza Balozi Seif sehemu mbali za majengo la Soko la Mji wa Wete baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wake.
Mshauri Muelekezi wa Kampuni ya Smal Investment of Town Council inayosimamia ujenzi wa soko la Mji wa Wete  Mhandisi Joseph John Marandu akimpatia maelezo Balozi Seif jinsi ya ujenzi unavyoendelea mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi huo.
Muonekano wa baadhi ya Majengo ya Soko Kuu la Matunda la Mji wa Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba yakiendelea na harakati a ujenzi.
Muonekano wa baadhi ya Majengo ya Soko Kuu la Matunda la Mji wa Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba yakiendelea na harakati a ujenzi.
Baadhi ya Wananchi wa Mji wa Wete wakionesha furaha yao wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa soko la Mji wa Wete ambapo Mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Balozi Seif. (Picha zote na Hassan Issa–OMPR – ZNZ)

Na Othman Khamis Ame
OMPR – ZNZ
10/1/2016.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa onyo kwa Uongozi wa Baraza la Mji wa Wete kisiwani Pemba kutoongeza wafanya biashara wapya hadi wale wazamani wote watakapopatiwa nafasi za kufanya biashara mara baada ya kumalizika kwa ujenzi wa soko jipya la Mji huo.

Alisema wapo watendaji ndani ya Taasisi za umma waliozoea kutumia madaraka yao kwa kuuza nafasi za biashara kwa wafanyabiashara wapya wenye uwezo mkubwa na kuwaacha wale wa asili kwa sababu tu ya kupenyezewa kitu kidogo.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa onyo hilo mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Soko Kuu la Matunda na Ofisi ya Baraza la Mji wa Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar za Januri  1964 kutimia miaka 52 sasa.

Alisema Serikali iliyopo ni ya wengi wa wananchi wanyonge, hivyo kamwe haitokubali kumvumilia mtendaji ye yote  asiyezingatia sheria na agizo hilo na kuamua kutumia wadhifa wake kwa kuwanyanyasa wafanyabiashara wa kipato cha chini.

Alieleza kwamba Taifa limekusudia kuwa na masoko makubwa ya kisasa katika Miji yote ya Unguja na Pemba ili kusaidia kupunguza tatizo la ajira kwa wananchi pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma bora katika masoko hayo.

“Kumalizika kwa ujenzi wa soko la Wete kutaongeza nafasi za kufanyia biashara kama vile maduka, nafasi za kuuzia mboga mboga na matunda mambo ambayo yatapelekea kutoa nafasi kwa wananchi walio wengi kujiajiri wenyewe “. Alisema Balozi Seif.

Alisema hatua hiyo ya Serikali pia italiwezesha Baraza la Mji wa Wete kukusanya mapato mengi kutokana na ongezeko  kubwa la wafanya biashara kasi ambayo italipa nguvu za ziada kutoka huduma bora kwa wakaazi wake pamoja na wageni watakao hitaji huduma za kibiashara katika eneo hilo.

Mkamau wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa Benki ya Wananchi wa Zanzibar (PBZ) kufikiria kuweka huduma zao mara utakapokamilika ujenzi wa soko hilo ili kuwawezesha wananchi kupata huduma za fedha kwa urahisi.

“Soko hili la Wete litakapokamilika ujenzi wake litakuwa miongoni mwa masoko ya kisasa lenya wafanyabiashara wengi zaidi ambao watafanya kazi katika mazingira bora “. Alisema Balozi Seif.

Akizungumzia suala la ukusanyaji wa mapato ambalo Masoko ni miongoni mwa vianzio vikubwa vya mapato vya Mabaraza ya Miji na Halmashauri za Wilaya, Ballozi Seif alishauri wakati umefika kwa watendaji wa taasisi hizo kuanzisha mfumo wa kisasa wa ukusanyaji mapato kwa kutumia mtandao wa Kompyuta.

Alisema mfumo huu wa kisasa  unaotumia mashine za Kisasa za kielektoniki umeonekana kuleta mafanikio ya haraka na kuachana na ule zamani wa kukusanya mapato kwa kupitia vibanda na risiti mkononi ukiwa ukipitwa na wakati.

Alifahamisha kwamba ukusanyaji  wa mapato unaotumika hivi sasa katika masoko mbali mbali nchini bado unaendelea kutoa mwanya kwa mapato mengi kuingia kwenye mifuko ya wajanja.

Akigusia suala la usafi wa mazingira katika masoko ya mabaraza ya Miji na Halmashauri za Wilaya Balozi Seif alipendekeza kuanzishwa kwa utaratibu maalum wa kusafisha masoko hayo.

Alisema si vibaya kwa Afisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ kuanzisha mashindano ya usafi wa masoko kila mwaka na mshindi kusawadiwa zawadi nono inayostahiki.

Balozi Seif alieleza kwamba utaratibu huo unaweza kusaidia sana Masoko hayo katika utunzaji wa mazingira katika kiwango kinachokubalika jambo ambalo pia litatoa fursa kwa wafanyabiashara wanaotumia muda wao mkubwa sehemu hizo kuishi katika mazingira rafiki.

“Masoko mengi yanapokuwa mapya hufuata taratibu zote za utunzaji wa usafi wa  mazingira lakini hali hiyo hatimae hupotea baada ya kipindi kifupi na watu kusahau kwamba uzorotaji wa usafi katika maeneo hayo huhatarisha maisha ya Wananchi “. Alifafanua Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishukuru Benkiu ya Dunia {(WB) kwa kukubali kugharamia ujenzi wa soko la Mji wa Wete na kuiomba Kampuni iliyopewa kazi za ujenzi huo kuhakikisha inakamilisha mradi huo kwa wakati ili Wananchi wanufaike nahuduma bora zinazotarajiwa kupatikana katika soko hilo.

Akisoma risala Mkurugenzi wa Baraza la Mji wa Wete Nd. Mgeni Othman alisema ujenzi wa soko la Mji wa Wete ulioanza Tarehe 4 Aprili mwaka 2015 na kukamilika rasmi tarehe 3 April mwaka huu unatarajiwa kuwafaidisha wakaazi 31,872 wa shehia 8 zilizouzunguuka Mji huo.

Nd. Othman alisema soko kuu la Matunda Mjini Wete litakuwa na milango 35 ya Biashara, Vikuta 80 vya uuzaji wa matunda, Banda la abiri, Ofisi 15 za wafanyakazi wa baraza la Mji,kituo cha Dala dala pamoja na vyoo.

Mkurugenzi huyo wa Baraza la Mji wa Wete alieleza kwamba zipo changamoto zilizojitokeza ndani ya ujenzi wa majengo ya soko hilo zilizopelekea kushindwa kujengwa kwa jingo la biashara ya uuzaji wa kuku kutokana na sehemu ya eneo hilo kuvamiwa kwa ujenzi wa nyumba mbili za makaazi ya watu.

Nd. Othman aliitaja changamoto nyengine iliyochangia ufinyu wa eneo la Barala la Mji wa Wete ni  kituo cha mafuta  ambacho hakimo ndani ya umiliki wa Baraza hilo la Mji wa Wete.

Akitoa Taarifa ya ujenzi wa Soko Kuu la Matunda la Mji wa Wete Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum Zanzibar Nd. Joseph Meza alisema Miji ya Bopwe, Limbani pamoja na Kizimbani hivi sasa inahitaji kuwa na masoko yake.

Nd. Meza alisema hali hiyo kwa sasa inatokana na kukuwa na Mitaa ndani ya Mji wa Wete pamoja na ongezeko la watu linalohitaji huduma hizo muhimu kwa maisha ya kila siku ya wanaadamu.

Ujenzi wa Soko Kuu la Matunda na Ofisi ya Baraza la Mji wa Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba unafanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Mkandarasi wa Kampuni ya Small Investment of Town Council 
(STC) kwa mkopo wa sh. Bilioni 1,597,383,432.40/- zilizotolewa na Benki ya Dunia (WB).

No comments:

Post a Comment