Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akimsikiliza Meneja wa Kituo cha Kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji, Mhandisi Pakaya Mtamakaya (kushoto) akizungumzia kuhusu uendeshaji wa mitambo ya kuzalisha umeme ya kituoni hapo.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akikagua moja ya mtambo wa kuzalisha umeme kwenye kituo cha uzalishaji umeme cha Kihansi. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), Mhandisi Felchesmi Mramba na kushoto ni Meneja wa Kituo cha kuzalisha umeme cha Kihansi, Mhandisi Pakaya Mtamakaya.
MAMENEJA wa Kanda wa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) wametakiwa kuhakikisha kuwa ifikapo tarehe 15 Januari mwakani kazi ya kuwaunganishia Umeme na Luku waombaji wa muda mrefu iwe imekamilika.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kwenye Kituo cha kuzalisha umeme cha Kihansi wakati alipokutana na Mameneja wote wa Kanda wa Shirika hilo.
Alionya kuwa Meneja yoyote atakaeshindwa kutimiza agizo hilo awe tayari kuacha ama kuachishwa kazi.
"Ikitokea Watanzania wakalalamika kucheleweshewa huduma kufikia tarehe 15 mwezi ujao, muwe tayari kuacha kazi," alisisitiza.
Profesa Muhongo alisema Watanzania wamechoshwa na utendaji duni wa Tanesco na kuagiza wahakikishe wanabadilika kwa kuwatumikia vyema wananchi.
Alisema kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi huku kubwa zaidi ikiwa ni kukatika kwa umeme mara kwa mara na kucheleweshewa huduma ya kuunganishiwa umeme na Luku.
Alisema kwa sasa anazungukia mitambo yote ya uzalishaji umeme nchini kufanya tathmini ili kuelewa hali halisi ya umeme na kuwataka kukomesha mara moja hali ya ukatikaji wa umeme mara kwa mara ambayo imekuwa kero kubwa kwa wananchi.
Vilevile Profesa Muhongo aliwaeleza Mameneja hao kuwa ifikapo siku ya Jumamosi ya tarehe 19 mwezi huu wawe na majibu ya kero mbalimbali za umeme nchini.
Alisema siku hiyo atakutana na Mameneja hao pamoja na watendaji wa taasisi mbalimbali zinazojishughulisha na masuala ya nishati nchini.
"Nimewaeleza hawa Mameneja kuwa siku ya jumamosi nitakuwa na kikao nao pamoja na watendaji wengine. Nataka waje na majibu ya kisayansi," alisema Profesa Muhongo.
Jambo jingine ambalo Waziri huyo anataka kutoka kwa Mameneja hao ni mkakati waliouandaa kuhakikisha bei ya umeme nchini inashuka.
"Watanzania wanauliza vipi tutafaidika na gesi yetu? Nataka mje na mkakati wa kupunguza bei ya umeme," alisema Muhongo.
Aidha, alizungumzia suala la kuongeza makusanyo ya mapato ya huduma ya umeme ambapo aliwaagiza Mameneja hao kuongeza mara mbili ya malengo ya ukusanyaji mapato waliyokuwa wamewekewa hapo awali.
Waziri Muhongo tayari amekwishatembelea vituo vya kuzalisha umeme vya Hale, Pangani, Nyumba ya Mungu, Mtera na Kihansi.

No comments:
Post a Comment