Na Georgina Misama - Maelezo
SERIKALI inatarajia kuzalisha
maji lita milioni 270 kwa siku baada ya kukamilika kwa mradi wa upanuzi wa
Chanzo cha Maji cha Ruvu Chini na upanuzi wa mtambo wa kusafishia maji.
Mradi huo unaotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na
Shirika la Kimarekani la Millenium Challenge Co-operation umegharimu kiasi cha
shilingi bilioni 66.24 na unatarajiwa kukamilika wakati wowote baada ya
kukamilika kwa kazi ya kulaza bomba linalosafirisha maji toka Ruvu chini kuja
Jijini Dar es Salaam.
Akiongea na waandishi wa habari,
leo Jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka
Wizara ya Maji, Bw. Shariff Athumani amesema kwamba mradi wa upanuzi wa mtambo
wa ujenzi wa bomba la Ruvu Chini utapunguza kero ya maji kwa wakazi wote
wanaotumia maji kutoka Ruvu Chini.
Akiyataja maeneo yatakayofaidika na kukamilika kwa mradi huo
ni pamoja na Bagamoyo na vitongoji vyake, Bunju, Mabwepande, Boko, Tegeta Kunduchi
na Mbezi Beach. Maeneo mengine ni pamoja na Mbezi Juu, Salasala, Kawe, Makongo,
Chuo Kikuu, Mikocheni, Msasani, Masaki,
Mwananyamala, Kinondoni, Magomeni,
Sinza, Manzese, Ubungo, Mabibo, Kigogo, Buguruni, Ilala, Kurasini, Bandarini na
maeneo yote ya katikati ya jiji la Dar es Salaam.


No comments:
Post a Comment