Profesa Florens Luoga
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
JUMUIYA ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam (DUCE) imeaswa kuendelea kushiriki katika shughuli za kijamii kwa wanapanga siku moja kila mwaka ya kutoa huduma za kijamii ili kuwa kitovu cha nidhamu bora na chachu ya maendeleo nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha Dar es salaam upande wa Taaluma Prof. Florens Luoga wakati wa kufungaji wa sherehe za maadhimisho ya miaka 10 ya chuo cha DUCE jana jijini Dar es salaam.
“Nawashukuru sana waliojitokeza kwenda kutoa misaada hospitalini, kushiriki kuchangia damu, kupanda miti na kwenda shule mbalimbali kuhamasisha masuala anuai ya kielimu kwa wanafunzi pamoja na walimu wao ili elimu iwe na tija na ufanisi kwa Watanzania wa sasa na baadaye” alisema Prof. Luoga.
Akitoa hotuba ya kufunga sherehe hizo, Prof. Luoga aliupongeza uongozi wa chuo cha DUCE kwa kuwa sehemu ya jamii ya Watanzania na kusisitiza kuwa ni wajibu wa chuo kikuu chochote duniani kutoa mchango kwa jamii katika elimu na kuwaletea maendeleo wananchi na taifa kwa ujumla.
Prof. Luoga alisisitiza kuwa ushiriki katika shughuli za kijamii utaendelea kusaidia chuo hicho kujitangaza na kujenga mahusiano mema miongoni mwa wanajamii ambao ndiyo chuo kimekuwa kikiwahudumia kwenye utoaji huduma mbalimbali.
Naye Mkuu wa chuo cha DUCE Prof. William Anangisye alisema kuwa zaidi ya kutoa taaluma katika elimu ya juu, wanajukumu pia la kujali suala la maadili kwa wanachuo.
Kwa upande mwingine Prof. Anangisye amesema kuwa chuo chake kinakabiliwa na changamoto mbalimbali katika kutoa taaluma na huduma bora kwa wanachuo ambazo ni pamoja na upungufu wa wahadhiri wa ngazi ya shahada ya uzamili na uzamivu na uwezo mdogo wa mabweni ya kulala ya wanachuo.
Chngamoto nyingine ni uhaba wa vyumba vya kutosha vya madarasa na kumbi za kuendeshea semina wakati wa masomo ikizingatiwa chuo hicho kimerithi majengo na miundo mbinu mingine kutoka kilichokuwa chuo cha ualimu cha Chang’ombe pamoja.
Aidha, katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kwa wiki moja kuanzia Novema 16 hadi 20 mwaka huu, yamefanyika mashindano ya michezo mbalimbali ikiwemo soka, mpira wa pete, kuvuta kamba, kufukuza kuku, kukimbia kwa magunia, riadha na uvaaji wa mavazi yenye staha kwa wanachuo wa kike na wa kiume.
Katika shindano hilo la mavazi yenye staha, mshindi kwa upande wanaume alikuwa John Paul mwanafunzi wa mwaka wa pili na Ruth Mtata mwanafunzi wa mwaka wa kwanza kwa upande wa wanawake.
Washindi hao walisema kuwa wanafurahia maisha yao wakati wote wakiwa chuoni na hata wakiwa nyumbani kwani wao ni walimu na wakiwa katika mavazi yenye heshima ni rahisi kuwafundisha wanachuo wengine na jamii kwa ujumla kuvaa mavazi kulingana na mila na desturi za kitanzania ambapo waliwaasa wanachuo wengine kuvaa nguo ambazo hazitoi maswali kwa wanafunzi wanaowafundisha na jamii kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment