TANGAZO


Friday, November 27, 2015

Balozi Seif Idd awataka waandishi wa habari kuwa makini katika kutoa habari za Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa ufafanuzi juu ya taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya Habari kuhusu kurejewa kwa uchaguzi  Mkuu wa Zanzibar. Alichokirejena tena ni kwamba CCM imethibitisha kuwa iko tayari endapo uchaguzi huo utapangwa tena na si vyenginevyo. (Picha na Hassan Issa–OMPR – ZNZ)

Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
27/11/2015.
WANAHABARI  wanapaswa kuwa makini zaidi katika utoaji wa habari zao hasa kipindi hiki ambacho  Zanzibar  inaendelea kutafuta  njia mwafaka wa hatma yake, ya baadaye kufuatia Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kufuta  Uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba mwaka huu baada ya kubaini hitilafu kadhaa katika zoezi zima la uchaguzi.

Nasaha hizo zimetolewa na Makamu wa Pili wa  Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar  alipotoa ufafanuzi wa kina juu ya taarifa zilizotolewa na  baadhi ya vyombo vya Habari vikieleza kuwa Viongozi wanaokutana kujadili suala hilo wamekubaliana kurudiwa kwa uchaguzi huo.

Alisema kalamu za waandishi wa habari kwa sasa ni vyema zikawaelekeza na kuwaongoza wananchi kujihusisha na harakati zao za kimaisha badala ya kuwaendeleza katika wimbi la mizozano na mifarakano inayoweza kuamsha  hamasa.

Balozi Seif akiongea na Redio ya Kiswahili ya Kimataifa ya Ufaransa (RFI) juzi alichokisema kuwaeleza wanahabari hao ni kwamba Chama cha Mapinduzi (CCM) pekee ndicho kilichotamka na kuthibitisha kuwa kiko tayari kurejea uchaguzi huo endapo utapangwa upya.

“Nilichokieleza juzi ni kwamba  CCM peeke ndiyo tuliothibitisha  na kukubali kurejea uchaguzi endepo utapangwa tena na hili tunaloendelea nalo la vikao na wenzetu bado tunajadiliana na maamuzi ya pamoja yatatolewa kwa waandishi hapo baadaye “. Alisema Balozi Seif.

Alisema hadi sasa hakuna chombo chochote cha habari  ndani na nje ya  nchi kilichoitwa au kupewa habari za mazungumzo yanayoendelea kati ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein na Katibu Mkuu wa  Chama cha Wananchi (CUF), ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif  Sharif  Hamadi kwa kuwashirikisha Marais wastaafu wa Zanzibar.

Balozi Seif Iddi, alisema utaratibu maalum utaandaliwa wa kutolewa taarifa rasmi kwa vyombo vyote vya habari ili ziwafikie wananchi wote mara baada ya kukamilika kwa mazungumzo  hayo na makubaliano yatakayofikiwa baina  ya pande hizo mbili.

Aliwathibitishia wananchi na wageni kwamba hali ya Zanzibar bado iko shwari na salama na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  na ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania  kupitia vyombo vyake vya Dola vitasimamia ipasavyo hali hiyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Iddi, aliwaomba wananchi wabakie kuwa watulivu, wastahamilivu  na kuendeleza umoja na mshikamano utakaosaidia kulivua Taifa hili katika shari inayoweza kuepukwa.

No comments:

Post a Comment