TANGAZO


Monday, September 28, 2015

Kippi Warioba ataja vipaumbele sita Jimbo la Kawe

Mwenyekiti wa Jimbo la Kawe kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Athuman Athuman (kushoto), akikabidhi ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015 kwa  Mgombea Ubunge wa Jimbo hilo, Kippi Warioba, katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu, uliofanyika katika eneo la Mlalakuwa, Kata ya Makongo jijini Dar es Salaam jana. 
Mgombea Ubunge Jimbo la Kawe kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kippi Warioba (wa pili kulia), akiwaaga wanaCCM baada ya kumaliza kuhutubia  mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu, katika eneo la Mlalakuwa, Kata ya Makongo jijini Dar es Salaam jana.

Na Mwandishi wetu
MGOMBEA Ubunge kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika jimbo la Kawe jijini Dar es Salaam, Kippi Warioba ametaja vipaumbele Sita atakavyovitekeleza pindi atakapopewa ridhaa ya kuwaongoza wananchi wa jimbo hilo.

Vipaumbele hivyo ni pamoja na kuboresha huduma ya afya, miundombinu, Maji, Michezo, migogoro ya ardhi, ajira na biashara.

Aliyasema hayo katika viwanja vya Mlalakuwa jijini jana, wakati akiwahutubia wananchi wa jimbo hilo.

Alisema pindi atakapochaguliwa atasimamia maendeleo ya kweli ya jimbo la Kawe kwa kuboresha mfuko wa Jimbo wa maendeleo wa Kawe.

Alisema atashirikiana na wazazi na walimu kuhakikisha matatizo katika sekta ya elimu ikiwamo uhaba wa vitabu, matundu vya vyoo na uhaba wa walimu yanapatiwa ufumbuzi.

“Sekta ya afya nitasimamia, zahanati hazitafungwa mapema pia suala la elimu nitapambana nalo watoto wenu hawatakaa chini,” alisema Warioba.

Aliongeza kuwa kupitia mfuko wa maendeleo ya Kawe atahakikisha upatikanaji wa vitabu mashuleni kwa kuwashirikisha wafanyabiashara wakubwa walioko katika Jimbo la Kawe.

Alisema pindi atakapochaguliwa kuwaongoza wananchi wa Kawe atakusanya Sh. milioni 5 zitakazosaidia katika sekta ya elimu.

Kihusu migogoro ya ardhi, Warioba alisema kuwa atahakikisha anapambana na tatizo hilo kwa kutenga maeneo ya kufanyia biashara, masoko pamoja na maeneo ya wajasiliamali.

Alisema suala la ajira na biashara atahakikisha kunakuwapo na mazingira mazuri kwa wafanyabishara wadogowadogo wakiwamo mama lishe na madereva bodaboda.

Naye mgombea Udiwani wa Kata ya Makongo kupitia CCM, William Iteba alisema mojawapo ya changamoto zinazoikabili kata ya Makongo ni tatizo la ukosefu wa miundombinu ya kupitishia maji taka.

Alisema pindi atakapochaguliwa kuwa diwani, atahakikisha suala hilo linapatiwa ufumbuzi kwa kutengeneza mifereji ya kisasa ya kupishia maji machafu.

Alisema suala la uhaba wa maji katika kata ya Makongo juu atalipatia ufumbuzi kwa kutafuta njia mbadara wa kuzibua visima vya maji vilivyokufa.

“suala la visima vya maji hapa mlalakuwa limekuwa sugu hivyo mkinipa ridhaa ya kuwaongoza nitahakikisha tatizo hilo nalipatia ufumbuzi,” alisema Iteba.

Alisema mbali na kutatua kero hiyo, pia atahakikisha upatikanaji upatikanaji wa gari la kubebea wagonjwa linapatikana pamoja na kuwapo kwa wodi za wazazi ili waweze kujifungua katika mazingira salama.

No comments:

Post a Comment