TANGAZO


Monday, May 25, 2015

HOTUBA YA WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO MHESHIMIWA SOPHIA M. SIMBA (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2015/16

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mhe. Sophia Simba

A: UTANGULIZI

1. Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii iliyoichambua bajeti ya Wizara yangu, naomba kutoa hoja kwamba sasa Bunge lako tukufu likubali kupokea na kupitisha makadirio ya Matumizi ya Kawaida na ya Maendeleo ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa mwaka 2015/16.

2. Mheshimiwa Spika, niruhusu nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema na utukufu kwa kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu nikiwa na afya njema na hivyo kuweza kushiriki mkutano huu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

3. Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kuwapongeza kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wao mahiri na maelekezo yao ambayo yamewezesha kushamiri kwa usawa wa jinsia na uzingatiaji wa haki za mtoto katika jamii ya Watanzania. Mwenyezi Mungu awajalie afya njema ili waendelee kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

4. Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza Mhe Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa uendeshaji bora wa shughuli za Bunge. Tunaendelea kumuomba Mwenyezi Mungu awajalie afya njema ili muweze kusimamia na kuratibu shughuli za Bunge kwa ufanisi.

5. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee napenda kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii ikiongozwa na Mwenyekiti mahiri Mheshimiwa Said Mohamed Mtanda na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Albert Obama Ntabaliba, kwa kuchambua na kujadili bajeti ya Wizara yangu. Ushauri na maelekezo ya Kamati hiyo yamewezesha Wizara yangu kuandaa bajeti kwa ufanisi.

6. Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua fursa hii kuwapongeza wabunge waliochaguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao ni Dkt. Grace Khwaya Puja na Innocent Rwabushaija Sebba kuwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

7. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa salamu za pole kwako, Bunge lako Tukufu, familia na wananchi wa Jimbo la Mbinga Magharibi kwa kifo cha aliyekuwa Mbunge wao na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii Mheshimiwa Kapteni Mstaafu John Damiani Komba. Bunge hili litamkumbuka daima kwa michango yake. Aidha, kwa masikitiko makubwa natumia fursa hii kuwapa pole wale wote waliopatwa na majanga ya ajali na mafuriko pamoja na kufiwa na ndugu, jamaa na wapendwa wao katika matukio mbalimbali yaliyotokea hapa nchini. Nitangulize dua zangu kwa Mwenyezi Mungu awapokee na kuwalaza mahali pema peponi. Amina.

B: MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA ILANI YA UCHAGUZI YA CCM KWA KIPINDI CHA MWAKA 2005 HADI 2015

I.       Ajira na Uwezeshaji wa Wananchi

Mheshimiwa Spika, Udahili wa washiriki katika Elimu ya Wananchi na ufundi stadi kupitia vyuo vyetu vya maendeleo ya wananchi umeongezeka kutoka washiriki 25,486 mwaka 2005 hadi kufikia washiriki 40,692 mwaka 2015 na idadi ya wasichana waliopata mafunzo ya “Mama course” iliongezeka kutoka 60 mwaka 2005 hadi kufikia wasichana 449 mwaka 2014. Wizara yangu ilibuni “mama course” mwaka 2000 kwa lengo la kuwapa wasichana waliopata mimba wakiwa shuleni fursa ya kujiendeleza kielimu kupitia mafunzo ya elimu ya wananchi baada ya kupoteza fursa hiyo katika mifumo rasmi kutokana na kanuni na taratibu za uendeshaji wa Elimu ya Msingi na Sekondari Tanzania. Aidha, kwa mwaka, jumla ya washiriki 36,838 walihitimu katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, kati yao, 22,939 ni wanaume na 13,899 ni wanawake. Wahitimu 33,319 sawa na asilimia 90.44 ya wahitimu kutoka katika vyuo vya Maendeleo ya wananchi wamejiajiri na wahitimu 3,047 sawa na asilimia 8.27 ya wahitimu wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi wameajiriwa katika makampuni ya watu binafsi na Taasisi mbalimbali za Serikali.

II.      Uendelezaji wa Makundi Mbalimbali

Maendeleo ya Watoto
8. Mheshimiwa Spika, Wizara iliwasilisha taarifa ya 3, 4 na 5 za Nchi yetu kuhusu utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto. Aidha, Wizara inaandaa taarifa ya 2 na 3 ya utekelezaji wa Mkataba wa Afrika Kuhusu Haki na Ustawi wa Mtoto ambayo itawasilishwa katika Kamati ya Umoja wa Afrika ya Haki na Ustawi wa Mtoto.

9. Mheshimiwa Spika, Wizara imeandaa na kuanza kutekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa Miaka Mitano wa Ushiriki wa Watoto. Mpango huo utatoa fursa kwa wazazi na walezi kujifunza njia bora za mawasiliano na mahusiano mazuri kati yao na watoto. Aidha, Mpango Kazi huu utabainisha namna ya kuwashirikisha watoto katika majadiliano na hata kunufaika na michango yao kimawazo, kiushauri na katika utekelezaji wa maamuzi mbalimbali ya kutatua matatizo yao.

Maendeleo ya Wanawake

10. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuwahamasisha wanawake kujiendeleza kielimu na kujenga uelewa wao katika kuweka nguvu za kutetea haki zao na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kimaendeleo. Aidha, wanawake wamejengewa uwezo wa ujasiriamali, utaalam wa biashara, jinsi ya kupata mitaji zaidi, masoko pamoja na kutoa mikopo mbalimbali.

III. Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru

11. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru iliendelea kudahili wanafunzi katika ngazi ya Shahada ya Kwanza kuanzia mwaka 2008/09 katika fani ya uandaaji na usimamizi shirikishi wa miradi, usimamizi wa programu za maendeleo ya jamii, maendeleo ya jinsia na stashahada ya uzamili ya maendeleo ya jamii. Udahili wa wanachuo umeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka, katika mwaka 2012/13, jumla ya wanachuo 139 wakiwemo wanaume 64 na wanawake 75, walidahiliwa. Mwaka 2013/14, jumla ya wanachuo 234 wakiwemo wanaume 88 na wanawake 146 walidahiliwa na katika mwaka 2014/15, jumla ya wanachuo 276, wakiwemo wanawake 189 na wanaume 87 walidahiliwa.

12. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2014/15, Serikali ilikipandisha hadhi Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru kuwa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru kupitia Azimio Na.1 la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la mwezi wa Aprili, 2014, katika Mkutano wake wa 17 Kikao cha 27 Taasisi hii inatarajiwa kuongeza Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii wa Ngazi ya Shahada ya maendeleo ya jamii ambao ni muhimu sana katika kuimarisha utendaji wa shughuli za Maendeleo ya Jamii. Hasa katika ngazi ya Halmashauri ambapo kuna uhaba mkubwa wa watumishi hawa.

IV. Demokrasia na Mamlaka ya Umma

13. Mheshimiwa Spika Wizara yangu kupitia Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ilitunga na kupitisha Kanuni za Maadili ya NGOs. Utekelezaji wa Kanuni za Maadili ya NGOs umelenga kukuza uwazi, uwajibikaji na uwezo wa Mashirika haya kujitathimini na kujikagua katika utekelezaji wa shughuli zao kulingana na katiba au miongozo ya kusajiliwa kwao. Kanuni hizi zimeamsha ari ya wadau wa NGOs kujitafiti na kubaini maeneo ambayo wana uwezo mkubwa wa kusaidia jamii na kuyaendeleza maeneo ambayo wako dhaifu kubuni mikakati ya kujijengea uwezo ili kutekeleza kwa ufanisi majukumu yao katika sekta mbalimbali nchini.

14. Mheshimiwa Spika, hatua nyingine ambazo Wizara yangu imechukua ni pamoja na kuanzishwa kwa Tovuti Maalum ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (http//:www.tnnc.go.tz) ambayo hutumiwa na wadau mbalimbali ikiwemo wanufaika wa miradi ya NGOs kutolea mrejesho kuhusu utendaji wa NGOs katika maeneo yao. Idadi ya wadau ambao wametoa mrejesho kuhusu utendaji wa NGOs hadi kufikia Machi, 2015 ni 30,679. Aidha, Wizara imekuwa ikitembelea na kukagua shughuli/kazi, miradi na program mbalimbali zinazotekelezwa na NGOs nchini kwa lengo la kutathimini utendaji na uendeshaji wa Mashirika hayo, ambapo jumla ya Mashirika 66 yamefikiwa hadi kufikia Machi, 2015.

Pamoja na mafanikio hayo, NGOs zinakabiliwa na changamoto zifuatazo: Baadhi ya Wilaya na Halmashauri za Majiji katika maeneo yao wameshindwa kuunda Kamati za Maadili ya NGOs ili kuwezesha mashirika haya kujidhibiti, kutandaa na kutathmini utendaji wao katika maeneo mbalimbali wanakoendesha miradi ya kusaidia na kukuza uwezo wa jamii


C: HALI HALISI YA SEKTA YA MAENDELEO YA JAMII NA CHANGAMOTO ZILIZOPO

Hali ya Maendeleo ya Jamii nchini

15. Mheshimiwa spika, utekelezaji wa dhana ya Maendeleo ya Jamii ambayo ni dhana shirikishi unajenga na kuimarisha misingi ya watu katika jamii kujitambua kwa kutambua uwezo walionao wa kubaini matatizo yao, kuweka vipaumbele, kubaini fursa na rasilimali walizonazo, kupanga na kutoa maamuzi ya kazi au miradi ya kutekeleza ili kutatua kero na matatizo yao. Kipimo cha mafanikio ya dhana hii ni ongezeko la watu katika jamii kubadilika katika kifikra na kimtazamo na kushiriki kikamilifu katika masuala yanayowaletea maendeleo endelevu. Katika kufanikisha haya, Wataalam wa maendeleo ya Jamii ni muhimu katika kuhamasisha, kuraghabisha, kushauri, kushawishi na kuelimisha wananchi na viongozi wao kwa kuwapatia elimu, maarifa na taarifa mbalimbali ili kuwaongezea uelewa, uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi sahihi ya utekelezaji wa dhana hiyo.

16. Mheshimiwa Spika, Pamoja na umuhimu wa Wataalam wa Maendeleo ya Jamii kama ilivyobainishwa katika Sera ya Maendeleo ya Jamii (1996) inayosisitiza kuwepo kwa Mtaalam wa Maendeleo ya Jamii mmoja kila kata ili kuchochea ari na mwamko wa wananchi katika kujiletea maendeleo yao, Sekta hii bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazosababisha utekelezaji usioridhisha wa dhana ya maendeleo ya jamii nchini. Hadi sasa Wataalam, waliopo katika Halmashauri za Wilaya na Manispaa ni 2,774, kati ya hao walioko Makao Makuu ya Wilaya ni 1,464, kwenye Kata ni 1,310. Kwa sasa kuna jumla ya kata 3,339 nchini na hivyo kufanya upungufu wa Wataalam wa Maendeleo ya Jamii kuwa 2,029 katika Kata.

Aidha, wataalamu hao wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vitendea kazi na vyombo vya usafiri. Changamoto hizi zimesababisha maeneo mengi hasa vijijini kukosa wahamasishaji na waraghibishi na hivyo kubaki nyuma katika suala zima la kujiletea maendeleo. Aidha, wananchi wameendelea kukosa elimu, ujuzi na taarifa mbalimbali zihusuzo maendeleo. Upungufu huo pia umesababisha ufuatiliaji usioridhisha wa shughuli mbalimbali za maendeleo katika Jamii.

17. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hizo, Wizara inaendelea kuwasiliana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma juu ya uwezekano wa kuwaajiri wataalam wa Maendeleo ya jamii moja kwa moja kutoka vyuoni.

Vyuo vya Maendeleo ya Jamii

18. Mheshimiwa Spika, Mwaka 1960 serikali ya kikoloni ilianzisha Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru. Chuo hiki kilianza kwa kutoa mafunzo ya ngazi ya Astashahada. Mwaka 1983 chuo kilianza kutoa mafunzo ya Stashahada ya juu. Hivi sasa Chuo hiki ni Taasisi inyotoa mafunzo ya Shahada za Maendeleo ya Jamii, Jinsia na maendeleo na Mipango na usimamizi shirikishi wa miradi ya maendeleo ya jamii. Halikadhalika, Taasisi inatoa Stashahada ya Uzamili katika masuala ya maendeleo ya jamii. Aidha, Vyuo vya Maendeleo ya Jamii Buhare, Rungemba na Misungwi vinatoa wataalam wengi zaidi wenye viwango tofauti vya taaluma, ili kukidhi mahitaji ya maendeleo ya jamii ngazi ya cheti na diploma. ya wataalamu wa Maendeleo ya Jamii katika Vijiji, Kata na Halmashauri.

19. Mheshimiwa Spika, Vyuo hivi vinakabiliwa na uhaba wa majengo, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, vyombo vya usafiri, na upungufu wa watumishi hasa wakufunzi. Licha ya changamoto hizi, udahili umeongezeka kutoka wanachuo 940 mwaka 2005/06 hadi kufikia 3,634 mwaka 2014/15 kama inavyoonekana katika Hali ya Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.

20. Mheshimiwa Spika, Vyuo hivi vilianzishwa kati ya miaka ya 1970 na 1980 kwa kurithi majengo yaliyokuwa yakitumika na taasisi mbalimbali kama vile Vyuo vya Maendeleo Vijijini (Rural Training Centre’s), Shule za Kati (Middle Schools), Vituo vya Mafunzo ya Ushirika na Vituo vya Mafunzo ya wakulima (Farmers Training Centres). Majengo haya yalijengwa kati ya mwaka 1950 hadi 1963. Kutokana na umri wa majengo haya, kwa sasa ni machakavu na hayaendani na mahitaji ya kutolea mafunzo kwa sasa. Madhumuni ya kuanzishwa kwa vyuo vya Maendeleo ya Wananchi ni kujenga uwezo wa wananchi wa kujitegemea kwa kuinua hali za maisha yao na ya Taifa kwa ujumla.Tangu kuanzishwa kwake vyuo hivi vimekuwa vikitoa mafunzo ya stadi na maarifa ya kuwawezesha wananchi kuajiriwa, kujiajiri na kuajiri wengine. Mafunzo haya huwajengea wananchi uwezo wa kuongeza uzalishaji mali wenye tija na ambao huongeza pato la kaya na hivyo kupunguza umasikini katika familia na Taifa kwa ujumla.

21. Mheshimiwa Spika, Hivi sasa kuna jumla ya vyuo 55 vya Maendeleo ya Wananchi ambavyo vipo katika wilaya mbalimbali nchini na baadhi ya wilaya zina zaidi ya chuo kimoja. Vyuo hivi vinatoa mafunzo na stadi mbalimbali kwa wananchi kama matumizi bora ya pembejeo, kilimo, uashi na useremala pamoja na stadi nyingine za maisha. Vyuo hivi pia vinatoa mafunzo ya Ufundi Stadi kwa kushirikiana na VETA. Kutokana na uchakavu wa majengo na miundombinu ya vyuo hivi, wizara inaendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia, jitihada mbalimbali zimefanywa na Wizara za kujenga majengo mapya, kufanya ukarabati wa majengo ya zamani na kuboresha mifumo ya maji na umeme.

Changamoto na namna ya kuzitatua

22. Mheshimiwa Spika, Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo: mahitaji makubwa ya rasilimali fedha na watumishi, ubovu na uchakavu wa majengo na miundombinu, ukosefu wa vifaa vya mafunzo, vyombo vya usafiri na maeneo ya vyuo kuvamiwa na wananchi kwa shughuli za kilimo na ujenzi wa makazi.

23. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hizi, Wizara imeendelea kuboresha mazingira ya utoaji mafunzo Vyuoni kwa kuajiri watumishi wa kada mbalimbal,i kufanya ukarabati wa majengo na miundombinu na kuvipatia vyuo nyenzo na zana za kufanyia kazi kulingana na rasilimali zilizopo.

Hali ya Maendeleo ya Jinsia nchini
Uwezeshaji wa wanawake

24. Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa usawa wa jinsia nchini unazingatiwa katika mipango na mikakati ya utekelezaji katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa. Kupitia programu na mikakati mbalimbali ya kuleta usawa wa jinsia, mafanikio makubwa yamepatikana kwa mfano: Idadi ya Mawaziri wanawake imeongezeka kutoka Mawaziri wanawake 6 kati ya Mawaziri 25 mwaka 2005 hadi kufikia Mawaziri wanawake 10 kati ya Mawaziri 30 mwaka 2015; Wakuu wa Wilaya wanawake wameongezeka kutoka 20 kati ya Wakuu wa Wilaya 104 mwaka 2005 hadi kufikia Wakuu wa Wilaya wanawake 46 kati ya Wakuu wa Wilaya 133 mwaka 2015; Majaji wanawake wameongezeka kutoka Majaji wanawake 8 kati ya Majaji 50 mwaka 2005 hadi kufikia Majaji wanawake 24 kati ya Majaji 67 mwaka 2015; na Wabunge Wanawake wameongezeka kutoka Wabunge wanawake 62 kati ya Wabunge 288 mwaka 2005 hadi kufikia Wabunge wanawake 127 kati Wabunge 357 mwaka 2015. Aidha, Katika kuhakikisha wanawake wanapata fursa ya elimu, mafunzo na ajira, idadi ya Madirisha ya Taarifa kwa Wanawake yameongezeka kutoka madirisha manne mwaka 2005 hadi kufikia madirisha 12 mwaka 2014. Jumla ya wanawake 14,589 wamefikiwa na watoa huduma wa dirisha kupitia huduma ya mmoja mmoja katika ofisi za Madirisha ya Taarifa kwa Wanawake.

25. Mheshimiwa Spika, katika kuwezesha wanawake kiuchumi, Wizara kupitia Benki ya Wanawake Tanzania imetoa mafunzo ya ujasiriamali na mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 24.86. Mikopo hiyo imewezesha wajasiriamali kujiajiri katika shughuli mbalimbali za biashara na hivyo kuinua vipato vyao kiuchumi na kijamii. Aidha, Benki ya Wanawake imeongeza vituo vya kutolea huduma za kibenki kutoka vituo 18 mwaka 2012/13 hadi kufikia vituo 81 mwaka 2013/14.

26. Mheshimiwa Spika, Idadi ya wanawake wanaopata mikopo kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Kiasi cha fedha kilichokopeshwa kimeongezeka kutoka Sh. 260,000,000 mwaka 2005 hadi kufikia Sh. bilioni 1,900,000,000 mwaka 2014. Mikopo hiyo imewawezesha wanawake kufanya shughuli za ujasiriamali ikiwa ni pamoja na: ufugaji; utengenezaji wa mvinyo; usindikaji wa mazao, mbogamboga, matunda na nafaka; kilimo cha bustani za mboga na mazao mbalimbali; biashara ya kuuza na kununua mazao kama mahindi, mpunga, ufuta, karanga, alizeti na mchele; ufumaji; ususi wa mikeka na vikapu. Aidha, mikopo hiyo imewawezesha kuinua vipato vyao na kuweza kugharamia mahitaji mbalimbali ya msingi kama vile; kulipia gharama za matibabu, kusomesha watoto, kujenga na kukarabati nyumba zao.

Ukatili na ubaguzi wa kijinsia

27. Mheshimiwa Spika, Wizara pia imeendelea kutekeleza Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kuzuia na Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (2001-2015) kwa kuijengea uwezo Kamati ya Kitaifa ya Kuzuia Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto ili iweze kushughulikia masuala ya ukatili, kuratibu Kampeni za Kutokomeza Vitendo vya Ukatili Dhidi ya Wanawake ili kuongeza uelewa wa madhara ya vitendo vya ukatili katika jamii na kuandaa Mwongozo wa Kuzuia na Kudhibiti Ukatili wa Kijinsia kwa Kamati za Vijiji, Mitaa, Kata na Wilaya.

Utekelezaji wa mikataba ya kikanda na kimataifa

28. Mheshimiwa Spika, Katika kutekeleza mikataba na maazimio mbalimbali ya kikanda na kimataifa ambayo nchi imeridhia, Wizara imeendelea kushiriki katika mikutano na kutekeleza mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa ikiwa ni pamoja na kutoa michango na uzoefu wake katika kuboresha na kuimarisha usawa wa jinsia na uwezeshaji wa Wanawake. Mikutano hiyo hutoa fursa kwa washiriki kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya wanawake na haki za wasichana na kutoa mapendekezo ya kiutekelezaji katika kufikia usawa wa jinsia.

Changamoto za Kuleta Maendeleo ya Jinsia

29. Mheshimiwa Spika, Pamoja na mafanikio yaliyopatikana bado zipo changamoto mbalimbali ambazo ni; Mahitaji makubwa ya mikopo ya Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake, mafunzo ya ujasiriamali yanayotolewa kwa wakopaji kutotosheleza kujenga uwezo unaohitajika, marejesho hafifu ya mikopo, mahitaji makubwa ya huduma za Benki ya Wanawake Tanzania hususan kwa wanawake wajasiriamali wa vijijini. Aidha, wanawake wengi kushindwa kushika nafasi za uongozi na maamuzi kutokana na majukumu mengi ya familia. Kuendelea kuwepo kwa mila na desturi ambazo zinahamasisha ndoa za utotoni na hivyo kuendeleza ukandamizaji kwa watoto wa kike na kusababisha mimba za utotoni.

30. Mheshimiwa Spika, Katika kukabiliana na changamoto hizo hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kufuatilia na kutathmini matokeo ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake; kutoa mafunzo kwa wanawake wajasiriamali kuhusu utunzaji wa kumbukumbu za biashara, jinsi ya kutumia mikopo na kulipa, kuweka akiba na kukuza biashara; kutafuta vyanzo vingine vya uwezeshaji wa wanawake kiuchumi na kufungua vituo vya kutolea mikopo vya Benki ya Wanawake Tanzania katika Wilaya zote za Mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam na Dodoma.

Hali ya Maendeleo ya Watoto

31. Mheshimiwa Spika, Takwimu za idadi ya watu na Makazi nchini ya mwaka 2012 inaonyesha kuwa kwa sasa Tanzania inakadiriwa kuwa na watoto 24,377,052 chini ya miaka 18 ambao kati yao 12,201,122 ni wasichana na 12,175,930 ni wavulana sawa na asilimia 50.1 ya Watanzania. Kundi hili linahitaji mipango madhubuti ili kuweza kuwalea na kuwaendeleza katika nyanja za afya, elimu, Lishe bora na ulinzi ili waweze kushiriki katika ujenzi wa Taifa.

32. Mheshimiwa Spika, Katika kuhakikisha kwamba watoto nchini wanapata haki yao ya ulinzi, Wizara imeendelea kuratibu shughuli za Kikosi Kazi cha Taifa cha Kuzuia na Kupambana na Ukatili Dhidi ya watoto ambacho kinasimamia utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Mwitikio na Kuzuia Ukatili Dhidi ya Watoto kuanzia mwaka 2013 hadi 2016 kwa kushirikiana na wadau. 

33. Mheshimiwa Spika, haki ya watoto ya kushiriki ni muhimu kwa kuwa inampa fursa ya kujadili na kutoa maoni kwa uhuru kuhusu mambo yanayowahusu na hivyo kumjengea uwezo wa kujiamini na kujieleza. Kwa kutambua hilo, Wizara imeendelea kuratibu shughuli za Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo vikao vyote vya Baraza Kuu na Kamati kuu vilifanyika. Hadi sasa mabaraza ya watoto katika ngazi ya Mikoa yameongezeka kutoka 12 mwaka 2005 hadi kufikia 22 mwaka 2014 na Wilaya kutoka mabaraza 57 mwaka 2005 hadi mabaraza 93 mwaka 2014.

34. Mheshimiwa Spika, Pamoja na mafanikio niliyoyataja, Wizara imekabiliwa na changamoto mbalimbali katika kusimamia utoaji wa haki za watoto hapa nchini kama ifuatavyo; kuongezeka kwa vitendo vya ukatili Dhidi ya watoto ambapo kuanzia mwaka 2000 hadi 2014 matukio 150 ya ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi yameripotiwa na kusabaisha vifo 74 ambapo asilimia 45 ni watoto. Kushuka kwa kiwango cha ukeketaji kusikoridhisha kwa asilimia 3 kutoka 18 mwaka 1999 hadi 15 mwaka 2014. kuwepo kwa tatizo kubwa la ndoa na mimba za utotoni ambazo zinasababisha matatizo makubwa katika maendeleo ya kielimu na afya kwa wasichana hapa nchini. Takwimu zinaonyesha kwamba wasichana 2 kati ya 5 wanaolewa kabla hawajafikisha umri wa miaka 15. Mikoa inayoongoza kwa ndoa za utotoni ni Mara (43%), Shinyanga (37%) na Tabora (38%). Aidha, takwimu za mwaka 2014 zinaonyesha kuwa asilimia 43 ya wasichana wanazaa kabla hawajafika umri wa miaka 18.

35. Mheshimiwa Spika, Ajira hatarishi kwa watoto ni tatizo jingine ambalo limeanza kushamiri hapa nchini. Inakadiriwa kwamba asilimia 28 ya watoto hapa nchini wenye umri kati ya miaka 5 hadi 17 wanafanyishwa kazi katika mashamba, migodi, viwanda, uvuvi na majumbani. Watoto hawa wanakosa haki yao ya kupata elimu na baadae wanakuja kuwa wategemezi katika taifa lao. Aidha, Idadi ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani imeongezeka kwa kasi hapa nchini hasa katika majiji, miji mikubwa, mipakani na katika mikusanyiko ya watu. Mwaka 2012 (Dogodogo Centre na Ustawi wa Jamii) takwimu zinaonyesha Jiji la Dar es salaam ambalo lina watu zaidi ya million 5 lilikuwa na watoto wanaofanya kazi na kuishi mitaani zaidi ya 5,000.

36. Mheshimiwa Spika, sababu kubwa zinazochangia matatizo haya ni uelewa mdogo wa jamii kuhusu haki za mtoto, mamlaka mbalimbali kushindwa kuchukua hatua zinazostahili kukabiliana na matatizo punde yanapotokea na kuendelezwa kwa mila na desturi zenye madhara katika jamii yetu. Wizara yangu imepanga mambo yafuatayo kukabiliana na changamoto hizi: Kudurusu Sera ya Mtoto ya 2008 kwa kuingiza masuala ya Malezi, makuzi na maendeleo ya Awali ya Mtoto katika kuimarisha misingi ya malezi ya watoto hasa katika umri mdogo; Kuimarisha mikakati ya ulinzi wa mtoto na kuboresha uratibu wa masuala ya watoto. Aidha, jamii itaendelea kuhamasishwa kutoa taarifa za vitendo vya ukatili kwa vyombo vya ulinzi na usalama. Sera hii ikikamilika italeta uwajibikaji shirikishi kwa sekta na wadau wote katika malezi ya watoto.

Hali ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali

37. Mheshimiwa Spika, Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2001 na Sheria ya NGOs Na. 24 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa mwaka 2005 zimechangia kuimarisha hali ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali hapa nchini. Lengo kuu la Sera hii ni kujenga mazingira wezeshi kwa ajili ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kushiriki kikamilifu na kuchagia kwa ufanisi katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Aidha, Sheria ya NGOs ilitungwa ili kuupa utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nguvu ya kisheria.

38. Mheshimiwa Spika, kutokana na utekelezaji wa sera na sheria hiyo, idadi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali imeongezeka kutoka 3000 iliyokadiriwa kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2001 hadi kufikia 7,060 mwezi Machi, 2015. Kati ya mashirika hayo, 277 ni ya kimataifa na mashirika 6,783 ni ya ndani ya nchi yanayofanya kazi katika ngazi ya wilaya, mkoa na taifa. Aidha, Wizara ilifuta usajili wa NGOs 24, kati ya hizo, NGOs 10 ziliomba kuondolewa kwenye rejista ya NGOs baada ya kukamilika kwa miradi na programu zao. Utekelezaji huo upo kwa mujibu wa Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ambayo inampa Msajili wa NGOs mamlaka ya kuyafutia usajili mashirika ambayo yanakiuka masharti ya usajili wao au pale mashirika husika yanapoomba kuondolewa kwenye rejista ya usajili kutokana na sababu mbalimbali.

39. Mheshimiwa Spika, mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika kutoa huduma kwa jamii katika masuala mbalimbali umeendelea kuimarika. Mchango huo unaonekana zaidi katika sekta na maeneo ya elimu, afya, maji, maendeleo ya jinsia, maendeleo shirikishi, mazingira, ustawi wa jamii, kilimo, utawala bora, haki za binadamu, huduma za sheria na ujasiriamali. Mfano, Shirika la CCBRT liliwezesha matibabu ya akina mama 868 wenye tatizo la fistula katika Hospitali za Seliani (Arusha), KCMC (Kilimanjaro) na CCBRT (Makao Makuu Dar es Salaam). Aidha, wanawake hao baada ya kupona walipatiwa ujuzi mbalimbali kupitia mafunzo yatolewayo na Kituo cha Mabinti kilichopo Dar es Salaam ili kuwawezesha wanawake hao kujitegemea kiuchumi.

40. Mheshimiwa Spika, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali pia yameendelea kukuza fursa za ajira kwa kuhimiza na kutekeleza vyema dhana ya kujitolea. Taarifa ya mwaka 2012 ya Wizara kuhusu mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika maendeleo inaonesha kuwa, mashirika haya yaliajiri jumla ya watu 60,700 ambapo kati yao, watu 27,312 wanafanyakazi kwa kujitolea.

41. Mheshimiwa Spika, pamoja na uwepo wa michango mingi na mizuri ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika utekelezaji wa mipango na program mbalimbali za nchi ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo (2025), MKUKUTA I na II, bado kuna changamoto mbalimbali zinazohitaji kufanyiwa kazi. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na Mashirika mengi Yasiyo ya Kiserikali kujikita zaidi mijini badala ya vijijini ambapo kuna wananchi wengi wenye kuhitaji huduma zao na kuendelea kutegemea ufadhili wa nje katika kutekeleza shughuli zao ambapo masharti ya ufadhili huo yanapelekea baadhi ya mashirika haya kukiuka mila, desturi, taratibu na sheria mbalimbali za nchi.

42. Mheshimiwa Spika, katika kutatua changamoto hizo, hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa NGOs kuhusu umuhimu wa taasisi hizi kuwafikia wadau wengi zaidi nchini hususan vijijini. Jitihada hizi zimefanyika kupitia Ofisi za Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, mikutano kati ya wadau wa mashirika haya na Bodi ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini pamoja na Wasajili Wasaidizi wa ngazi ya Wilaya na Mikoa. Aidha, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yameendelea kuhimizwa kutumia fursa ya marekebisho ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2005 kwa kuanzisha miradi ya kujipatia kipato kitakachoyawezesha kuepukana na utegemezi uliokithiri kwa wafadhili wa nje katika kuwahudumia walengwa wao.

D: MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MWAKA 2014/15 NA MALENGO YA MWAKA 2015/16.

Sekta ya Maendeleo ya Jamii

43. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizara yangu iliendelea kusimamia utekelezaji wa majukumu yake kulingana na malengo na shabaha zilizopangwa. Katika bajeti ya mwaka huo, Wizara ilikisia kukusanya jumla ya Sh.1,845,360,000 kutoka vyanzo mbalimbali. Hadi Machi 2015, makusanyo yalifikia Sh. 1,815,145,600 sawa na asilimia 98.4 ya lengo. Aidha, Wizara iliidhinishiwa jumla ya Sh. 29,453,599,000 ambapo kati ya hizo, Matumizi ya Kawaida ni Sh. 20,526,055,000 yakijumuisha Sh. 12,818,434,000 kwa ajili ya mishahara na Sh. 7,707,621,000 kwa ajili ya Matumizi Mengineyo. Bajeti ya Matumizi ya Miradi ya Maendeleo iliyoidhinishwa ni Sh. 8,927,544,000

44. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili, 2015, Wizara ilikuwa imepokea jumla ya Sh. 8,639,231,903 sawa na 67% ya Bajeti ya Mishahara iliyoidhinishwa na matumizi yakiwa Sh.8,639,231,903 sawa na 100% ya fedha za Mishahara zilizotolewa, fedha za Matumizi Mengineyo Sh. 3,260,825,060 ikiwa ni 42% ya fedha za matumizi mengineyo zilizopokelewa na Sh. 3,260,825,000 sawa na 100% ya fedha zilizotolewa zimetumika. Aidha, fedha za ndani za maendeleo Sh.1,700,000,000 zilitolewa sawa na 25% ya fedha zilizoidhinishwa na Sh. 338,634,000 sawa na 17% ya fedha za nje zilitolewa ambapo Sh. 1,450,000,000 sawa na 85% ya fedha za ndani zilizotolewa na Sh.338,634,000 sawa na 100% ya fedha za nje zilizotolewa zilitumika.


45. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inatambua mchango wa Wataalam wa Maendeleo ya jamii katika kusaidia jamii ili ziweze kujiletea maendeleo. Katika mwaka 2015/16, Wizara yangu itaendelea kuwajengea uwezo Maafisa Maendeleo ya Jamii ngazi ya Mkoa na Halmashauri za Wilaya kuhusu mbinu shirikishi jamii, utatuzi wa migogoro ya kijamii na mbinu za ujasiriamali ili kuboresha utendaji kazi wa wataalam hawa waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Vyuo vya Maendeleo ya Jamii

46. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutoa mafunzo ya Taaluma ya Maendeleo ya Jamii katika ngazi ya Astashahada ambapo jumla ya wanachuo 1,885 walidahiliwa katika mwaka 2014/15, ambapo kati yao wanaume 758 na wanawake ni 1,128, Stashahada ni 1,430 wakiwemo wanaume 378 na wanawake1,052 kwa Vyuo nane vya Maendeleo ya Jamii ambavyo ni Buhare, Rungemba, Missungwi, Monduli, Uyole, Ruaha, Mlale na Mabughai. Aidha, Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru wanachuo 276 walidahiliwa katika ngazi ya Shahada ambapo wanaume walikuwa 87 na wanawake 189. Hali kadhalika wanachuo watatu (3) walidahiliwa katika ngazi ya Stashahada ya Uzamili kati yao kulikuwa na mwanume mmoja (1) na wanawake wawili (2).

47. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2015/16, Wizara itaendelea kudahili na kutoa mafunzo kuanzia ngazi ya Astashahada hadi Stashahada ya Uzamili. Mafunzo haya yanahusu misingi ya maendeleo ya jamii, mipango shirikishi, ubunifu na uandishi wa miradi, mbinu za uongozi na utawala, mbinu za kuendesha biashara, uchambuzi na upangaji wa masoko. Lengo la mafunzo hayo ni kutoa elimu, ujuzi na mbinu mbalimbali zitakazowasaidia wataalam wa Maendeleo ya Jamii kutekeleza dhana ya maendeleo ya jamii kwa vitendo katika jamii kwa kuwawezesha watu kutambua uwezo walio nao wa kubaini matatizo na uwezo wao wa kutumia raslimali zilizopo ili kuongeza kipato na kupunguza umaskini. Aidha, Wizara itaendelea kukamilisha jengo la maktaba katika Chuo cha Tengeru, ujenzi wa uzio katika Chuo cha Rungemba na Ruaha, kujenga jengo la utawala, jengo la maktaba, ukumbi wa mikutano, nyumba za watumishi katika Chuo cha Uyole, kukarabati majengo na miundombinu katika Vyuo vya Buhare, Mlale, Ruaha, Mabughai, Missungwi na Monduli ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi

48. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2014/15, Vyuo vitano vya Maendeleo ya Wananchi vya Sofi, Mputa, Kilwa Masoko, Tarime na Mwanhala vilifanyiwa ukarabati mkubwa na mdogo wa madarasa, mabweni, majengo ya utawala, ujenzi wa vyoo, mabwalo ya kulia chakula, miundombinu ya mifumo ya umeme, maji safi na maji taka. Aidha, Vyuo vya Nandembo, Sengerema na Chala vilipewa magari ili yatumike kwa usafiri na kutolea mafunzo kwa vitendo. Katika mwaka wa fedha wa 2015/16, Wizara itaendelea kuboresha maeneo ya kutolea mafunzo kwa kujenga madarasa, nyumba za watumishi na majengo ya utawala katika vyuo vya: Ilula na Newala, kuweka mfumo wa umeme katika vyuo vya Munguri, Ulembwe, Rubondo, Msingi, Malya na Mwanhala na kugharamia upimaji na upatikanaji wa Hati Miliki wa vyuo vya: Ifakara, Ikwiriri, Msingi, Mwanva, Musoma, Arnautoglu, Chilala, Kilwa Masoko, Chisalu na Kisarawe kwa lengo la kupunguza migogoro inayosababishwa na wananchi kuvamia maeneo ya vyuo kwa shughuli za kilimo na ujenzi wa makazi. Wizara itaendelea kujenga na kufanya ukarabati wa majengo na miundombinu kwa awamu kadri fedha zinavyotengwa kwa ajili ya kazi hizi zitakavyopatikana kutoka Hazina.

Maendeleo ya Jinsia

49. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kushiriki na kutekeleza mikataba na maazimio mbalimbali ya kikanda na kimataifa ambayo nchi imeridhia, Wizara ilishiriki katika mkutano wa‘’ African Regional Conference’’ uliofanyika tarehe 17-19 Novemba, 2014 Addis Ababa - Ethiopia. Mkutano huo ulilenga kupitia taarifa ya nchi ya Beijing+20 na kutoa maazimio ya utekelezaji wa maeneo 12 yaliyoanishwa. Taarifa hiyo iliwasilishwa katika kikao cha 59 cha Kamisheni ya Hali ya Wanawake ambacho kilifanyika nchini Marekani Machi, 2015.

Aidha, mkutano huo ulitoa fursa kwa washiriki kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya wanawake na haki za wasichana na kutoa mapendekezo ya kiutekelezaji katika kufikia usawa wa kijinsia. Katika mwaka 2015/16, Wizara itaendelea kushiriki katika utekelezaji wa mikataba ya kikanda na kimataifa ikiwa ni pamoja na kutoa michango na uzoefu wake katika kuboresha na kuimarisha usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake pamoja na kushiriki mikutano mbalimbali.

50. Mheshimiwa Spika, Ili kufikia lengo la kuwepo kwa usawa wa jinsia, uingizwaji wa masuala ya jinsia katika mipango, mikakati, bajeti, sera na programu mbalimbali bado unaendelea kutiliwa mkazo. Katika kipindi cha mwaka 2014/15, Wizara iliendesha mafunzo ya ukusanyaji wa takwimu zilizochambuliwa kijinsia kwa maafisa 50 kutoka Wizara mbalimbali, Taasisi zisizo za serikali na Taasisi za Elimu. Mafunzo hayo yaliwezesha ukusanyaji
wa takwimu zilizochambuliwa kijinsia na hivyo kuweza kukamilisha Taarifa ya Hali ya Jinsia Nchini (Tanzania Country Gender Profile - TCGP). Taarifa hizo zitatumiwa na serikali pamoja na wadau mbalimbali katika kufanya maamuzi, ushawishi, utungaji sera na mipango mbalimbali ya maendeleo kwa kuzingatia usawa wa jinsia. Aidha, Wizara itaendelea kutoa mafunzo kwa ngazi mbalimbali za uongozi ili kujenga uelewa wa pamoja kuhusu uingizwaji wa masuala ya jinsia, uboreshaji wa Taarifa ya Hali ya Jinsia Nchini pamoja na usambazaji wa taarifa hiyo.

51. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia vikao vya robo mwaka vya kikundi cha uingizaji wa masuala ya kijinsia katika Sera za Kitaifa na Kisekta (Gender Mainstreaming Working Group for Macro Policies) imeweza kuandaa Mwongozo wa Uingizaji wa Masuala ya Jinsia katika Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now - BRN). Lengo ni kuwezesha kuwepo kwa matokeo makubwa kwa kuzingatia mahitaji ya makundi yote ya wanawake na wanaume. Mwaka 2015/16, Wizara itaendelea kuratibu uingizwaji wa masuala ya jinsia katika Sera za Kitaifa pamoja na kujenga uwezo kuhusu uingizwaji wa masuala ya kijinsia.

52. Mheshimiwa Spika, Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) ambayo ni mali ya umma inayomilikiwa kwa kiasi kikubwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kufikia mwaka 2014/15, Benki ina wanahisa wadogowadogo wanaokadiriwa kufikia 160 wanaomiliki hisa zisizozidi asilimia 2. Katika mwaka, 2014/15, Benki ilitoa mikopo kwa wajasiriamali wapatao 10,847. Kati ya idadi hiyo wanawake ni 8,135 sawa na asilimia 75 ya wateja wote waliopatiwa mikopo. Thamani ya mikopo iliyotolewa ni kiasi cha Sh. 12,469,650,000. Kati ya kiasi hicho, jumla ya Sh. 8,561,200,000 zilikopeshwa kwa wanawake, sawa na asilimia 69 ya mikopo iliyotolewa. Benki imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya mtaji kwa kutafuta fursa mbalimbali za kupata fedha za kujiendesha na kutanua mtaji wake.

53. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2015/16, benki inatarajia kuendelea kutoa huduma zake katika maeneo mengi zaidi kupitia njia ya wakala wa benki (Agency Banking) na kufungua ofisi za kutolea huduma za mikopo mikoani. Aidha, katika mwaka wa kibenki wa 2014, Benki ya Wanawake imetengeneza faida ya shilingi milioni 141 kabla ya kodi (Profit Before Tax). Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi wa benki wanaona mwaka 2015 ni kipindi mwafaka cha kuanza mchakato rasmi wa kuuza hisa ili kukuza mtaji wa benki na kuiwezesha Benki kujiendesha na kupanua wigo wa huduma pasipo kutegemea mtaji kutoka Serikalini.

54. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2014/15, Mfuko wa Wanawake umetoa jumla ya Sh. 31,000,000 kwa Halmashauri tatu ambazo ni Bunda, Iringa pamoja Mkalama. Aidha, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeadhimisha Siku ya Wanawake Duniani iliyofanyika Mkoani Morogoro katika Uwanja wa Jamuhuri na Mgeni Rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Kaulimbiu ya siku hiyo ilikuwa ‘’Uwezeshaji Wanawake; Tekeleza Wakati ni Sasa’. Aidha, siku ya Maadhimisho shughuli mbalimbali zilifanyika ikiwemo maonyesho ya biashara kutoka Wizara mbalimbali, vikundi vya wanawake Wajasilimali pamoja na wadau wa maendeleo.




Maendeleo ya Watoto

55. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2014/15, Wizara iliandaa Mpango Kazi wa Taifa wa Miaka Mitano wa Ushiriki wa Watoto (2014-2019). Lengo la Mpango Kazi huo likiwa ni kuongeza ushiriki wa watoto katika masuala mbalimbali yanayowahusu. Katika mwaka 2015/16, Wizara itaendelea kusambaza mpango kazi huu katika Halmashauri za Wilaya.

56. Mheshimiwa Spika, Wizara imekamilisha uandaaji wa rasimu ya Sera ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Mtoto pamoja na Mkakati wake wa Utekelezaji. Sera hii ipo katika ngazi za juu za maamuzi kwa ajili ya kupitishwa. Sera imeandaliwa mahsusi ili kuhakikisha uwepo wa mfumo fungamanishi na shirikishi wa utoaji huduma za Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto. Katika mwaka 2015/16, Wizara inataraji kukamilisha mchakato na kutoa nakala 3,000 za sera hiyo pamoja na mkakati wake wa utekelezaji na kusambaza kwa wadau kwa ajili ya utekelezaji.

57. Mheshimiwa Spika, Wizara iliendelea kuratibu utoaji wa taarifa zinazohusu vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kwa kushirikiana na Asasi isiyokuwa ya Kiserkali ya C-SEMA ambapo kati ya mwezi Julai, 2014 na Machi, 2015 jumla ya simu 21,960 zilipigwa kupitia mtandao wa simu namba 116. Taarifa hizo zilishughulikiwa kulingana na aina ya tatizo/suala lililowasilishwa. Katika mwaka 2015/16, Wizara itaendelea kuratibu utoaji wa huduma hii kwa kushirikiana na asasi husika.

58. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2014/15, Wizara iliratibu maandalizi ya taarifa ya kujibu hoja mbalimbali zilizotolewa na Kamati ya Haki za Watoto ya Umoja wa Mataifa kuhusu ripoti ya nchi ya 3, 4 na 5 ziliyowasilishwa katika kamati hiyo mnamo mwezi Januari, 2012 na kuwasilisha majibu ya hoja kwenye kamati hiyo mwaka 2015. Katika mwaka 2015/16, Wizara itaendelea kuyafanyia kazi maoni ya jumla ‘’Concluding Observation’’ yaliyotolewa na Kamati hiyo ya Haki za Watoto ya Umoja wa Mataifa.

59. Mheshimiwa Spika, Mwaka 2014/15, Wizara yangu ilizindua rasmi Zana za Mawasiliano kwa ajili ya kuzuia ukatili dhidi ya watoto yenye lengo la kuelimisha wazazi, watoto, wanahabari na wanajamii jinsi ya kujizuia na kutoa taarifa kuhusu matukio mbalimbali ya ukatili dhidi ya mtoto ambapo nakala 1,000 za zana hizo zilisambazwa kwa wadau wa masuala ya ulinzi na haki za watoto hapa nchini. Katika mwaka wa fedha 2015/16, Wizara itasambaza nakala 2,000 za zana hizo na kuratibu utekelezaji wake.

60. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2014/15, Wizara yangu imeratibu Maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 16 Juni na mwaka huu yameadhimishwa katika ngazi ya Mkoa. Kaulimbiu ya mwaka 2015 ni “Usawa wa Kijinsia na Haki za Watoto katika Familia: Wanaume Wawajibike’’
Kaulimbiu hii inaelekeza umuhimu wa wanaume katika kutambua na kuheshimu usawa wa kijinsia katika jamii zetu. Kuachana na mfumo dume ndani ya jamii kutompa fursa mwanamke/msichana kupata maendeleo ya kiuchumi, kisiasa, kielimu, afya na kiutamaduni.
Aidha, Wizara imeratibu maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo kila mwaka yanaadhimishwa tarehe 15 Mei. Kaulimbiu ya mwaka 2015 ni “Tokomeza Mimba na Ndoa za Utotoni: Kwa Pamoja Tunaweza”. Kaulimbiu hii inatukumbusha sisi wadau wa maendeleo ya watoto pamoja na wananchi jukumu letu katika kuwalinda watoto dhidi ya ndoa na mimba za utotoni, ambazo zina athari kubwa katika maendeleo ya elimu na afya ya mtoto. Aidha, kuachana na kupiga vita mila na desturi zenye athari katika jamii zetu ndio silaha pekee katika kukabiliana na tatizo la mimba na ndoa za utotoni.

Mashirika Yasiyo ya Kiserikali

61. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizara yangu iliendelea kusajili NGOs ikiwa ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2001 pamoja na Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na. 24/2002 iliyorekebishwa mwaka 2005. Hadi kufikia Mwezi Machi, 2015 jumla ya mashirika 7,060 yalipatiwa usajili katika ngazi mbalimbali ili kuyawezesha kutambulika kisheria na kutekeleza malengo yaliyokusudiwa. Katika kipindi cha mwaka 2015/16, Wizara itaendelea na usajili wa Mashirika hayo.

62. Mheshimiwa Spika, mwaka 2014/15, Wizara yangu ilichukua hatua mbalimbali za kuimarisha uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini. Hatua hizi ni pamoja na: kuendelea kuliwezesha Baraza la Taifa la NGOs kutekeleza majukumu yake ya kisheria kwa kupitisha Kanuni za Uendeshaji wake na Kanuni za Chaguzi za Baraza hilo za ngazi mbalimbali. Kanuni hizi zitaliwezesha Baraza na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa ujumla kujiendesha kwa ufanisi zaidi kwa kujidhibiti ili kuimarisha taswira na mchango wao katika jamii.

63. Mheshimiwa Spika, hatua nyingine iliyochukuliwa katika uratibu wa NGOs ni kukuza ubia baina ya Serikali na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa kuingia makubaliano ya kufanya kazi kwa pamoja na NGOs 20 zinazojihusisha na maendeleo ya wanawake na watoto. Aidha, Wizara iliendelea kuhamasisha ubia baina ya mashirika haya na Taasisi nyingine za Serikali zikiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa. Pia, Wizara yangu iliboresha Benki ya Taarifa na Takwimu za NGOs kwa kuingiza masuala ya jinsia. Taarifa na takwimu hizi zinatumiwa na wadau katika kufikia maamuzi mbalimbali ya kimaendeleo. Katika mwaka 2015/16, Wizara itaendelea kuratibu na kufuatilia shughuli za NGOs kwa lengo la kuendelea kujenga mazingira wezeshi ya NGOs katika kushiriki na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Uhamasishaji, Uelimishaji na Ushawishi

64. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizara yangu iliandaa vipindi vya luninga na redio, matangazo kupitia magazeti, vipeperushi na mabango, mikutano ya waandishi wa habari kwa ajili ya kuelimisha umma kuhusu masuala ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake, familia, haki za watoto na uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Aidha, kwa kushirikiana na UNICEF, Wizara yangu imeandaa kipindi maalum cha ‘WALINDE WATOTO’ ambacho kinatangazwa kupitia redio 14 zenye usikivu wa kitaifa na kikanda Tanzania Bara na Zanzibar. Lengo la kipindi ni kuhamasisha wadau wa maendeleo ya mtoto kushiriki kikamilifu katika jitihada za kuzuia na kutokomeza ukatili dhidi ya watoto nchini. Katika mwaka 2015/16 Wizara itaendelea kuhamasisha, kuelimisha na kushawishi umma kuhusu masuala ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake, familia, haki za watoto na uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.

Uratibu wa Sera, Programu na Mipango ya Wizara.

65. Mheshimiwa Spika, Katika mwaka 2014/15, Wizara yangu imeandaa Andiko la Programu ya Maendeleo ya Elimu ya Wananchi lenye awamu mbili za utekelezaji kwa vipindi vya miaka mitano mitano zilizohuishwa na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano awamu ya pili na ya tatu. Aidha, programu hiyo ni sehemu ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Elimu na rasimu yake imewasilishwa na kupitishwa katika vikao vya sekta ya Elimu. Programu inalenga kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, utoaji wa ujuzi na stadi mbalimbali na elimu ya ujasiriamali zitakazowezesha vijana na wananchi kupata fursa za kuongeza vipato vyao kwa kujiajiri au kuajiriwa na hivyo kuchangia katika kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa 2025. Kwa mfano, kuzalisha mafundi mchundo watakaotumika katika fursa iliyopo ya uchumi wa gesi na mafuta katika jamii.

Aidha, Wizara inaandaa maandiko ya Programu ya Kuwezesha Wanawake na Wasichana Kiuchumi, Programu ya Kutokomeza Ndoa za Utotoni na Programu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kama sehemu ya kutekeleza Agenda ya Maendeleo ya Afrika 2063 kwa kuanza kutoa msukumo maalum wa kuwaendeleza wanawake na watoto. Katika mwaka 2015/16, Wizara itaendelea kuratibu utafutaji wa fedha kutoka vyanzo mbalimbali ili kutekeleza programu hizo.

66. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu iliandaa Mwongozo wa Ufuatiliaji na Tathmini utakaotumika kufuatilia utekelezaji wa sera, mikakati, mipango na mikataba ya kikanda na kimataifa iliyoridhiwa. Katika mwaka 2015/16, Wizara itawezesha upatikanaji wa taarifa za msingi kulingana na mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ulioandaliwa. Aidha, itawajengea uwezo Maafisa 25 wa Maendeleo ya Jamii wa Mikoa kuhusu ukusanyaji, uchakataji, uchambuzi na uandaaji wa taarifa za utekelezaji wa sera za Wizara.
67. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia maendeleo ya Sera na Programu za Sekta ya Maendeleo ya Jamii. Katika mwaka 2015/16, Wizara itafanya tathmini kuhusu ufanisi wa Sera ya Taifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili kubaini changamoto na mafanikio yaliyopatikana. Aidha, matokeo ya tathmini yatatumika kurekebisha sera iliyopo ili kuweka mazingira wezeshi kwa NGOs na kuziwezesha kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo kwa wananchi.

Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu

68. Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kutoa huduma za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kwa madhumuni ya kuboresha utendaji kazi kwa kuzingatia misingi ya haki, usawa, uadilifu, utawala bora na uwazi kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi katika kazi. Wizara imeendelea kuweka mkazo katika kudhibiti vitendo vya rushwa na uzembe kazini ili kuwa na watumishi waadilifu na wawajibikaji, wenye ari, moyo na msimamo thabiti katika utekelezaji wa majukumu katika utumishi wa Umma. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2015/16, Wizara itaendelea kutoa huduma za kiutawala na usimamizi wa rasilimaliwatu kwa kuzingatia misingi ya haki, usawa, uadilifu na utawala bora.

69. Mheshimiwa Spika, Ili kuwawezesha watumishi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, Wizara imewawezesha watumishi kuhudhuria mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu ndani na nje ya nchi. Kwa mwaka 2014/15, watumishi 64 wamewezeshwa kupata mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi ndani na nje ya nchi. Katika mwaka 2015/16, Wizara itaendelea kuwajengea uwezo watumishi kwa kuwapatia mafunzo ya kuongeza weledi na ufanisi wa kazi za utumishi wa umma.

70. Mheshimiwa Spika, Mwaka 2014/15, Wizara imeendelea kutoa motisha kwa watumishi kwa kuwapandisha vyeo jumla ya watumishi 156, kuwabadilisha kada watumishi 2 na kuwathibitisha kazini watumishi 38 wa kada mbalimbali. Katika mwaka 2015/16, Wizara inatarajia kuwabadilisha kada watumishi 15, kuwapandisha vyeo watumishi 355 na kati yao watumishi 105 ni wa kada ya ualimu.

71. Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha 2014/15, Wizara yangu imeendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa kufanya ukarabati na uboreshaji wa baadhi ya maeneo ya ofisi ( Makao Makuu) kama vile ujenzi wa eneo la kuegesha magari, ununuzi wa jenereta, uboreshaji wa masijala pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya umeme, simu na Internet. Kwa mwaka wa fedha 2015/16, Wizara itaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa kuendelea kufanya ukarabati mdogomdogo katika jengo la Wizara Makao makuu.

72. Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka 2014/15, Wizara imeajiri watumishi wapya wa kada mbalimbali wapatao 148 na kufanya Wizara kuwa na watumishi 1,122. Nafasi 428 zimekwisha tangazwa na Sekretarieti ya Ajira,
hivyo mchakato utakapo kamilika watumishi hao pia wataajiriwa. Hata hivyo, Wizara bado inakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi hasa wa kada ya ukufunzi katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi na vya Maendeleo ya Jamii. Katika kukabiliana na changamoto hizo, Wizara imepeleka maombi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa ajili ya kupata kibali cha kuajiri watumishi wa kada mbalimbali. Kwa mwaka 2015/16, Wizara itaendelea kuomba kibali cha kuajiri watumishi ili kupunguza pengo lililopo.

73. Mheshimiwa Spika, katika kupambana na janga la UKIMWI na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari na magonjwa ya moyo, mwaka 2014/15 Wizara imewawezesha watumishi 154 kupata mafunzo, ushauri nasaha pamoja na huduma ya upimaji afya kwa hiari. Wizara imeendelea kuhamasisha watumishi kupima afya zao kwa kutumia utaratibu wa kuwaleta wataalamu wa huduma za afya kwa ajili ya ushauri nasaha, upimaji wa hiari na kuwapatia watumishi wanaoishi na virusi vya UKIMWI huduma ya lishe. Kwa kutambua umuhimu wa michezo katika kuimarisha afya za watumishi, kwa mwaka 2014/15, Wizara iliwawezesha watumishi kushiriki katika mashindano ya SHIMIWI. Kwa mwaka wa fedha 2015/16, Wizara itaendelea kuhamasisha upimaji wa afya ikiwa ni pamoja na kutoa huduma stahiki na kuendelea kuhamasisha watumishi kushiriki katika michezo.

74. Mheshimiwa Spika, Kutokana na umuhimu wa kushirikisha watumishi kuboresha utendaji kazi, utekelezaji wa majukumu ya Wizara na kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiutendaji, Wizara imeweza kufanya Mkutano mmoja wa Baraza la Wafanyakazi kwa mwaka 2014/15. Kwa mwaka 2015/16, Wizara itaendelea kuhakikisha Mikutano ya Baraza la Wafanyakazi inafanyika.

E: HITIMISHO

75. Mheshimiwa Spika, Majukumu ya Wizara yangu ni kuhakikisha jamii na wananchi wanabadilika kifikra na kimtizamo ili kuwa na jamii inayoshiriki kikamilifu katika kujiletea maendeleo yao wenyewe na Taifa kwa ujumla. Majukumu haya ni mtambuka, hivyo basi utekelezaji wa Malengo na Mipango ya Wizara kwa mwaka 2015/16, bado utahitaji ushirikiano mkubwa zaidi wa wadau mbalimbali hasa Mikoa na Halmashauri.

F: SHUKRANI

76. Mheshimiwa Spika, Napenda sasa kumshukuru sana Naibu Waziri, Mhe. Dkt. Pindi Hazara Chana (Mb.), kwa ushirikiano mkubwa anaonipa katika kuongoza Wizara hii. Vilevile, napenda kutoa shukrani za dhati kwa: Katibu Mkuu, Bibi Anna Tayari Maembe, Naibu Katibu Mkuu, Bibi Nuru H. M. Millao; Wakurugenzi; Wakuu wa Vitengo; Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Wanawake Tanzania - Bibi Magreth Chacha; Wakuu wa Vyuo; na Wafanyakazi wote wa Wizara yangu wa ngazi zote, kwa jitihada zao katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara ambayo ni pamoja na kuniwezesha mimi kuwasilisha hotuba hii mbele ya Bunge lako tukufu.

77. Mheshimiwa Spika, Napenda kumalizia hotuba yangu kwa kuwashukuru wadau wote tunaofanya nao kazi na kushirikiana kwa namna moja au nyingine. Peke yetu kama Wizara tusingefikia mafanikio niliyoyataja. Naomba kupitia Bunge lako tukufu, kutoa shukrani zangu za dhati kwa wafuatao: Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Asasi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA); Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF); Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP); Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA); Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA); Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (FAWETA); Medical Women Association of Tanzania (MEWATA); White Ribon; Plan International; Save the Children na Mashirika mengine mbalimbali Yasiyo ya Kiserikali pamoja na wale wanaofanya kazi kwa maslahi ya jamii kwa namna moja au nyingine.

78. Mheshimiwa Spika, Napenda pia kuyashukuru Mashirika kutoka nchi rafiki ambayo yameendelea kutusaidia na kufanya kazi na sisi. Mashirika hayo ni pamoja na: GPE; KOICA na UK Education. Aidha, nayashukuru Mashirika ya Umoja wa Mataifa ambayo ni: UNICEF; UNDP; UNFPA na UN WOMEN kwa misaada yao mbalimbali iliyofanikisha utekelezaji wa majukumu mengi ya Wizara yangu.

G: MAKADIRIO YA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2015/16

79. Mheshimiwa Spika, Ili Wizara yangu iweze kutekeleza majukumu na malengo yake kwa mwaka 2015/16, sasa naliomba Bunge lako tukufu liidhinishe matumizi ya shilingi 31,421,641,000. Kati ya fedha hizo,
(a) Shilingi 11,038,075,000 ni kwa ajili ya Mishahara
(b) Shilingi 9,460,146,000 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo
(c) Shilingi 10,923,420,000 ni kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Maendeleo ambapo Shilingi 8,000,000,000 ni fedha za ndani na Shilingi 2,923,420,000 ni fedha za nje.


80. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments:

Post a Comment