TANGAZO


Friday, April 17, 2015

Balozi Idd ampongeza Raza kwa jitihada zake za kuunga mkono sekta ya Michezo visiwani Zanzibar

Mwanamichezo Maarufu nchini ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini, Moh’d Raza Hassanali, akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kabla ya kukabidhi vifaa vya michezo kwa timu ya Soka ya Ofisi ya Makamu wa Pili. Wa kwanza kulia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Dk. Khalid Salum Moh’d,  wa kwanza kushoto ni Mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya timu ya ofisi hiyo, Pili Tajo Hassan na Mwenyekiti wa timu hiyo, Haroub Gharib Bilal.
Mwanamichezo Maarufu Moh’d Raza akimkabidhi seti ya jezi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif (wa pili kulia), akizungumza wakati akimpongeza mwanamichezo Moh’d Raza kwa juhudi za uongozi wa Kampuni yake ya Hassan and Son’s za kusaidia sekta ya michezo visiwani Zanzibar.
Balozi Seif (wa pili kulia), akiziwashilisha jezi hizo kwa Katibu Mkuu wa Ofisi yake, Dk. Khalid Salum Moh’d, mara baada ya kukabilidhiwa na mwanamichezo maarufu nchini, Moh’d Raza.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Dk. Khalid Salum Moh’d akipokea  soksi na mipira kutoka kwa Balozi Seif iliyotolewa na Moh’d Raza kwa ajili ya Tmu ya Soka ya Wizara yake. (Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)

Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
16/4/2015.
MWANAMICHEZO maarufu nchini ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini, Moh’d Raza Hassanali amesema Kampuni yake ya Hassan and Son’s  inakusudia kuanzisha mpango maalum wa kuzisaidia timu za Maskuli Unguja na Pemba ili ile ari na vugu vugu la michezo lirejee kama zamani.

Raza alisema hayo wakati wa hafla fupi ya kumkabidhi Seti za jezi, soksi na mipira Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa ajili ya Timu ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Hafla hiyo fupi iliyofanyika Ofisini kwa Balozi Seif Vuga Mjini Zanzibar pia ilihudhuriwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Khalid Salum Moh’d pamoja  na  Viongozi wa Timu ya Wizara hiyo.

Raza alisema wakati umefika kwa washirika wa michezo Nchini kuunga mkono mpango huo wa kurejesha mashindano ya mara kwa mara katika maskuli ya Zanzibar kwa lengo la kuwaandaa vijana kuwa na timu imara zitakazokuwa na uwezo wa Kimataifa.

Akipokea msaada huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alimpongeza Mwanamichezo huyo Maarufu wa Zanzibar Moh’d Raza kwa jitihada zake za kuunga mkono sekta ya Michezo hapa Nchini.
Alisema kitendo cha Mwanamichezo huyo ni miongoni mwa uzalendo aliouonyesha ambao unastahiki kuigwa na washirika pamoja na wanamichezo wengine.

Balozi Seif alisema juhudi za Mwanamichezo huyo zilipelekea kuteuliwa kuwa mshauri wa Rais anayesimamia michezo pamoja na kuwa Mwenyekiti wa Saidia Zanzibar Ishinde { SAZI } katika awamu zilizopita.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambalo limo ndani ya Ilani ya chama cha Mapinduzi ni kukuza  michezo hapa Nchini.

Alishauri Taasisi zinazosimamia michezo Nchini  kwa kushirikiana na Ofisi yake ziandae utaratibu wa kuanzisha Ligi Maalum za Mawizara ya Serikali na tayari Mwanamichezo Moh’d Raza ameonyesha nia shauku ya kuzisaidia Timu hizo kwa kuzipatia vifaa endapo ligi hiyo itaasisiwa rasmi.

No comments:

Post a Comment