Mwenyekiti wa Kamati ya Amani na utulivu Tanzania Sheikh Noman Thabit Jongo akiwaeleza viongozi wa Dini mbalimbali suala la amani na utulivu katika kuelekea katika kuipigia kura ya maoni Katiba Inyopendekezwa na kuwaasa kuwaelimisha waumini wao juu ya ubora wa Katiba Inayopendekezwa kwani imegusa makundi yote katika Jamii.
Mbunge wa WAWI kupitia chama cha wananchi CUF Mh. Hamad Rashid Mohamed akiongea na viongozi wa Dini mbalimbali na kuwaasa kuisoma, kuielewa Katiba Inayopendekezwa na kuacha kupotoshwa kwa kusomewa vipengele vya Katiba hiyo bila kupewa ufafanuzi, wakati wa mkutano ulioratibiwa na Kamati ya Amani na Utulivu Tanzania kushirikisha viongozi wa Dini leo Zanzibar.
Mwenyekiti wa Kamati ya Amani na utulivu Tanzania Sheikh Noman Thabit Jongo akisisiza kwa viongozi wa Dini kuisoma na kuielewa Katiba Inayopendekezwa ili kuepuka chuki zinazosambazwa kuhusu katiba hiyo ili baadae waweze kufanya uamuzi sahihi utakaopelekea uwepo wa amani nchini.
Katibu wa Kamati ya Amani na utulivu Tanzania Padri. Damas Mfoi akiongea katika mkutano wa Kamati ya Amani na Viongozi wa Dini mbalimbali Zanzibar na kuwaasa kusambaza ujumbe wa Amani na kuepuka mambo yoyote yatakayoashiria uvunjifu wa amani hasa katika kipindi hiki Taifa likielekea katika Mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu.
Baadhi ya Viongozi mbalimbali wa Dini Zanzibar wakifuatilia Mada zilizokuwa zikiwasilishwa katika Mkutano huo.
Mmoja ya Mjumbe wa Mkutano akifanya rejea katika Katiba Inayopendekezwa wakati wa uwasilishwaji wa Mada katika Mkutano huo. (Picha zote na Hassan Silayo)
Na Hassan Silayo
VIONGOZI wa Dini nchini wameaswa
kuhubiri suala amani na utulivu nchini hasa katika kipindi hiki taifa
likielekea upatikanaji wa Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa wilaya ya
Mjini Magharibi Bw. Ayoub Mohamed Mahmoud wakati wa mkutano wa Kamati ya amani
Tanzania na Viongozi wa Dini Mbalimbali leo Zanzibar
Bw. Ayoub alisema kuwa suala la amani
na utulivu linamhusu kila mtu kwenye jamii na Taifa kwa ujumla hivyo ni budi
kuepuka vishawishi vya uvunjifu wa amani hasa katika wakati huu wa kuelekea
upatikanaji wa Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu.
“ Kama tunavyofahamu sasa taifa
linaelekea katika mambo makubwa mawili ya upatikaji wa Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu hivyo ninyi kama
viongozi wa Dini hamna budi kuhubiri Amani na Utulivu ili Taifa kwa ujumla
liweze kufikia dhamira na malengo yaliyowekwa” Alisema Ayoub.
Aidha Bw. Ayoub aliongeza kuwa nchi
yetu ina sheria, kanuni na taratibu zinazotuongoza hivyo wananchi hawana sababu
ya kugombana hasa kwenye mambo yanayolenga kuliletea taifa maendeleo kwani
hatuna pengine pa kwenda pindi machafuko yanapotokea.
Akizungumzia kuhusu mchakato wa
Katiba Inayopendekezwa Bw. Ayoub alisema kuwa wananchi hawana budi kujitokeza
katika kuipigia kura ya maoni Katiba Inayopendekezwa kwani katiba hii imegusa
makundi yote katika jamii.
Pia Bw. Ayoub aliwaasa viongozi wa
dini kuisoma katiba hii kifungu kwa kifungu, ibara kwa ibara ili kwenda kutoa
elimu kwa waumini wao ili kuepuka upotoshaji unaofanywa na baadhi ya watu
wasioitakia mema nchi yetu.
Naye Mbunge wa WAWI kupitia tiketi ya
Chama cha Wananchi (CUF) Mh. Hamad Rashid Mohamed alisema kuwa amekuwa
akishangazwa na baadhi ya watu wanaopita mitaani na kutoa upotoshaji wa baadhi
ya vipengele vilivyo katika Katiba Inayopendekezwa bila kuangalia madai yaliyopelekea
kuanzishwa kwa mchakato wa upatikaji wa Katiba
Mpya.
Mh. Rashid alisema kuwa maaandamano
mengi yaliyokuwa yakifanyika kudai upatinaji wa Katiba Mpya yalitaka uwepo wa
Tume huru ya uchaguzi,Mgombea huru na
matokeo ya Tume kuhojiwa mahakamani na si suala la Serikali tatu au
Serikali ya Mkataba jambo ambalo limejumuishwa vyema katika Katiba Inayopendekezwa na kutoa fursa pana zaidi ya kile walichokuwa wakidai.
Alieleza kuwa wananchi hawana budi
kusoma na kuelewa maudhui yaliyomo Katiba Inayopendekezwa ili kuona fursa
zinazopatikana na jinsi gani Katiba hiyo imegusa maisha ya kila kundi katika
Jamii ikiwemo watoto, wavuvi, walemavu, vijana, wanawake na wazee.
Pia Mh. Rashid alisema kuwa viongozi
wa dini hawana budi kuhubiri amani hasa katika kipindi hiki cha upatinaji wa
Katiba Mpya na kuwaepuka wale wote wanaotaka kulipeleka taifa katika hali
uvunjifu wa amani kwa kuhubiri chuki hasa juu ya Katiba Inayopendekezwa.
Akizungumzia kuhusu suala la amani na
utulivu katika mchakato huu wa Upatikanji wa Katiba Mpya Mwenyekiti wa Kamati
ya Amani na Utulivu Tanzania Sheikh Noman Thabiti Jongo alisema kuwa njia pekee
ya kuepuka uvunjifu wa amani ni kwa kuisoma na kuielewa Katiba Inayopendekezwa
na kuacha kusikiliza chuki zinazoenezwa na baadhi ya watu kuhusu mchakato huu.
Naye Katibu wa Kamati ya amani na
Utulivu Padri Damas Mfoi aliwataka viongozi wote wa dini katika nafasi zao
kuhubiri amani na utulivu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea upatikanaji wa
Katiba Mpya na Uchaguzi mkuu.
No comments:
Post a Comment