TANGAZO


Sunday, March 1, 2015

Simba yawasili Zanzibar kujiandaa kwa mchezo na mtani wake wa jadi Yanga utakaopigwa Jumapili Machi 8

Kikosi cha Simba SC, kilichowasili mjini Zanzibar leo.

Na Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar
KLABU ya Simba ya jijini imewasili visiwani Zanzibar tayari kwa maandalizu ya mchezo wake na Yanga unaotarajiwa kufanyika jumapili ijayo katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salam.

Kikosi cha watu 28, wakiwemo viongozi, madaktari na wajumbe wa dawati la ufundi kimeiwasili visiwani Zanzibar, majira ya saa 8.35 mchana bila ya Kocha Mkuu timu hiyo, msaidizi wake Suleiman Matola na Simon Sserenkuma, ambao wataungana na kikosi hicho mara baada ya kumalizika kwa matatizo binafsi wanayokabiliana nayo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mjumbe wa Kamati Tendaji ya klabu hiyo, aliyepo Zanzibar Abdul Mshangama, amesema kuwa Matola amebakia jijini Dar es Salama kutokana na kukabiliwa na matatizo ya kifamilia sawa na Sserenkuma aliyepo nchini kwao, Uganda na kwamba wawili hao wangelijiunga pamoja na kocha mkuu wa timu, Goran kopunovic ambao wangewasili usiku wa leo au kesho asubuhi.
Mshangama alisema mbali ya kuwa ni kawaida ya klabu hiyo kupiga kambi visiwani humo kila inapokuwa na mechi kubwa kama ya Jumapili, kambi hiyo ya siku 7, itakuwa maalum kutokana na ukubwa wa mechi inayowakabili.

Alisema ingawa mchezo huo ni wa kawaida kama ilivyo michezo mingine ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara, mchezo huo unapewa umuhimu mkubwa baada ya timu hiyo kuibuka na ushindi wa magoli 5 – 0 dhidi ya Prison ya Mbeya.

“Tunashukuru timu imewasili salama na kufika katika kambi yetu ya kawaida na wachezaji wote isipokuwa SIMON (Sserenkuma) ambaye atawasili Dar es salam kesho jioni na ataungana na  wenzake usiku au keshokutwa asubuhi”, alisema Mshangama.

Mjumbe huyo alisema mazoezi ya timu hiyo yanayotarajiwa kufanyika katika Kiwanja cha Chuo cha Kiislamu Chukwani na Uwanja wa Amaan yataendelea hadi Jumamosi na katika kipindi hicho, timu hiyo inatarajia kucheza mechi mbili za majaribio kabla ya timu hiyo haijarudi jijini Dar es Salam siku inayofuata moja kwa moja hadi uwanjani kwa ajili ya mchezo huo.
“Mipango ya timu ni kubakia hapa hadi siku moja kabla ya mchezo au siku ya mchezo na baadaye kurudi jijini na kufikia Uwanjani”, aliongeza mshangama aliyekuwa ameambatana na baadhi ya wadau wa timu hiyo huku wachezaji na walimu wakianza safari ilipo kambi ya timu hiyo.

No comments:

Post a Comment