TANGAZO


Wednesday, March 11, 2015

Serikali yaahidi kutoa Milioni 50 kuboresha mradi wa Jaribu Mpakani

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Amos Makalla akisaini kitabu cha wageni kwenye ofisi za Mradi wa Maji wa Kibiti bada ya kuwasili kukagua mradi huo.
Baadhi ya watendaji wa mradi na wilaya ya Rufiji na wawakilishi wa wananchi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Amos Makalla (hayupo pichani) wakati alipozungumza nao. 
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Amos Makalla, akizungumza na watendaji wa wilaya ya Rufiji, watendaji wa mradi wa maji wa Kibiti na wawakilishi wa wananchi kuhusu mradi wa Kibiti. 
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Amos Makalla akiondoka kwenye ofisi ya Mradi wa Maji wa Kibiti baada ya kufanya mazungumzo. 
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Amos Makalla akikagua baadhi ya miundombinu ya mradi wa Maji wa Kibiti. 
 . Mhandisi wa Maji wilaya ya Rufiji, Mhandisi Frobert Andrea (wa pili kushoto) akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Amos Makalla kuhusu mradi wa Jaribu Mpakani wakati alipotembelea mradi huo.Kushoto ni Mbunge wa Kibiti Mhe. Abdul Malombwa.
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Amos Makalla akiwa na wenyeji na watendaji wengine, akikagua tenki la maji la Mradi wa Maji wa Jaribu Mpakani baada ya kutembelea mradi huo.
Mhandisi wa Maji wilaya ya Rufiji, Mhandisi Frobert Andrea, akisoma taarifa ya Mradi wa Maji wa Jaribu Mpakani, kwenye mkutano kati ya Naibu Waziri wa Maji na wakazi wa Jaribu Mpakani. 
Baadhi ya wakazi wa Jaribu Mpakani waliohudhuria mkutano wao na Naibu Waziri, wakisikiliza taarifa ya Mradi wao, iliyowasilishwa na Mhandisi Frobert Andrea. 
Diwani wa Kata ya Mjawa ulipo mradi wa Maji wa Jaribu Mpakani, Ramadhani Mketo, akizungumza katika mkutano huo.
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Mhe. Nurdin Babu, akizungumza kwenye mkutano huo. 
Mbunge wa Kibiti, Mhe. Abdul Malombwa akimkaribisha Naibu Waziri kuzungumza na wananchi wa Jaribu Mpakani. 
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Amos Makalla akizungumza na wananchi wa Jaribu Mpakani kuhusu mradi wao.
Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Amos Makalla, akiagana na wenyeji wake kabla ya kuondoka. (Picha zote na Hussein Makame-MAELEZO)


Na Hussein Makame-MAELEZO
SERIKALI imeahidi kutoa shilingi Milioni 50 kuboresha mradi wa maji wa Jaribu Mpakani ulioko wilyani Rufiji mkoani Pwani, kufuatia mradi huo kushindwa kufanya kazi kutokana na baadhi ya miundombinu yake kushindwa kukidhi mahitaji ya wakazi wa eneo hilo.

Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Amos Makalla wakati akizungumza na wananchi wa Jaribu Mpakani baada ya kutembelea na kukagua miradi ya maji ya Kibiti na Jaribu Mpakani ambayo imekumbwa na changamoto katika uendeshaji wake.

Akieleza changamoto za mradi huo, Mhandisi wa Maji wilaya ya Rufiji Mhandisi Frobert Andrea, alisema mradi huo uliojengwa na Serikali mwaka 2005 kwa Shilingi Milioni 139,umeshindwa kufanya kazi baada ya mabomba yake kupasuka kutokana na msukumo mkubwa wa maji.

Alisema baada ya hapo, Halmashauri ya wilaya ya Rufiji ilitoa shilingi Milioni 24.4 kuchimba kisima kirefu kipya cha mita 120 na Mbunge kutoa Shilingi Milioni 15 kuboresha mradi huo, lakini juhudi hizo zilishindwa kuwapatia maji baada ya mabomba kupasuka.

Kutokana na changamoto hiyo, mradi huo ulihitaji Shilingi Milioni 50 ili kurekebishwa mabomba, tenki la maji na vituo vya kutolea maji, fedha ambazo zilishindwa kupatikana.

Akizungumzia hali hiyo, Mhe. Naibu Waziri Makalla aIiibua matumaini ya wakazi wa eneo hilo ambao walionesha kutokuwa na furaha kutokana na kutofanya kazi kwa mradi huo.

“Asubuhi tulipokutana, nikamuuliza Mkuu wa Wilaya na Mbunge sasa nyinyi mnaomba Milioni 50 wakati Serikali haina fedha nyie mnachangia kiasi gani? wakasema hatuna fedha?”

“Lakini kwa maneno niliyoyasikia kutoka kwa Katibu Mwenezi wa CCM anavyoimba hapa mpaka anataka kutoa machozi, na kwa mazungumzo niliyofanya na mbunge wa hapa na kwa sura za kina mama mbele yangu mimi naridhia kubeba mzigo huu kurudi wizarani wanipe fedha hizi” alisema Mhe. Makalla na kuongeza:

“Kwa sababu sisi tumeshatumia shilingi Milioni 139, kwa nini tuzipoteze hizi fedha, kwa hiyo hizi Milioni  50 ziwe mwendelezo wa kuboresha huu mradi ambao tulishauanza sio mpya.

“Kwa hiyo mimi hili nalibeba na hata hapa nimeshafanya maamuzi nimeshamuandikia Mkurugeni wa Maji Vijijini alipokee na alitekeleze.Nitakwenda kuongea na Waziri na zaidi Waziri wangu ni mtu mzuri ananiamini na amenipa Mamlaka.

“Mhe. Maghembe ni mtu na mwalimu mzuri na ana nia nzuri nikimueleza anasema endelea fanya kazi.Kwa hiyo uamuzi huu umeshakwisha na naamini tutaendelea kushirikiana”.

Mbali na kutoa ahadi hiyo, Mhe. Waziri Makalla alimuomba Mkuuu wa Wilaya asimamie uboreshaji huo na kuhakikisha fedha zinatumika kama zilivyokusudiwa hadi senti tano ya mwisho inayotumika.

 “Naomba ufanye hivyo ili watu wa Jaribu Mpakani wapate maji na ndio maana ya Serikali hii ni sikivu, nimeshakuja Serikali nimewasikia na nimechukua maamuzi ya haraka” alisema.

Akitoa shukrani Diwani wa Kata ya Mjawa,Ramadhani Mketo alikiri kwamba wananchi wa Jaribu Mpakani wamepata majibu tena majibu sahihi kabisa na ametaka uharakishwe ili wapate maji.

“Kwa hiyo mimi nimshukuru sana Mhe. Naibu Waziri na nimuombee watu wa Mvomero wampe kura nyingi na pia nimshukuru Mhe. Mbunge kwa juhudi zake za kuwapatia maendeleo wananchi.” alisema.

Akiwa katika Mradi wa Maji wa Kibiti, Naibu Waziri Mhe. Amos Makalla ameshauri kuundwa kwa Mamlaka ya Maji na Bodi ya Maji ya mradi wa Kibiti ili kukidhi mahitaji ya uendeshaji wa mradi huo mkubwa wa maji.

Mradi wa Maji wa Kibiti umekua ukikabiliwa na gharama kubwa za uendeshaji mbali na changamoto ya kukatika mara kwa mara kwa umeme, hali inayofanya maji kutofikia wananchi kama inavyotakiwa.

Kufuatia changamoto hizo, Mhe. Makalla aliomba mchakato uanze wa kuunda vyombo hivyo viwili kwani anaamini mradi huo ni mkubwa hivyo kamati ya maji inayouendesha inakosa nguvu ya kuuendesha.


Alisema kuna haja kwa uongozi wa juu wa Wizara ya Maji na ule wa Wizara ya Nishati na Madini kukutana ili kujadili jinsi ya kushiriiana na kuhakikisha inaokoa miradi mingi ya maji inayoshindwa kufanya kazi kwa kukosa umeme.

No comments:

Post a Comment