TANGAZO


Monday, March 9, 2015

Rais Dk. Ali Mohamed Shein akabidhi Vihori (boti ndogo) wakulima wa mwani visiwani Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akisalimiana na mwakilishi wa VSO Tanzania Jean Van Wetter wakati alipowasili katika viwanja  vya Ukimbi wa Salama Bwawani Hotel Mjini Unguja leo katika hafla ya sherehe ya kukabidhi Vihori kwa wakulima wa Mwani. (Picha zote na Ikulu)
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akifuatana na Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Bi. Zainab  Omar Mohamed  (wa pili kushoto) na Katibu wa Wizara hiyo Bi. Asha Ali Abdalla (kulia)wakati alipowasili katika viwanja  vya Ukumbi wa Salama Bwawani Hotel Mjini Unguja leo katika hafla ya sherehe ya kukabidhi Vihori kwa wakulima wa Mwani. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akiangalia bidhaa mbali mbali zilizotengenezwa kwa kutumia zao la mwani na kikundi cha Ulezi ni Kazi cha shehia ya Fujoni Jimbo la Kitope, wakati wa sherehe za kukabidhi Vihori kwa wakulima wa mwani hafla iliyofanyika leo Ukumbi wa Salama Bwawani Hotel Mjini Unguja. 
Baadhi ya Viongozi,Wananchi na wakulima wa mwani wakiwa katika sherehe za kukabidhi vihori kwa wakulima wa mwani zilizofanyika leo katika ukumbi wa Salama Bwawani Mjini Unguja ambapo mgeni rasmi akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Akinamama wakulima wa mwani kutoka sehemu tofauti za Unguja na Pemba wakiwa katika ukumbi wa Salama Bwawani Hotel Mjini Unguja katika  sherehe za kukabidhi vihori kwa wakulima wa mwani kwa Mikoa ya Unguja na Pemba leo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akimkabidhi Kihori Bi. Zainab Daudi Haji mkulima wa mwani wa Uroa Wilya ya Kati Mkoa wa Kusini  wakati wa sherehe za kukabidhi vihori kwa wakulima wa mwani zilizofanyika leo katika ukumbi wa Salama Bwawani Mjini Unguja. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akimkabidhi Kihori Bw. Kombo Salim Hamadi mkulima wa mwani wa Tumbe Magharibi Kaskazini Pemba wakati wa sherehe za kukabidhi vihori kwa wakulima wa mwani zilizofanyika leo katika ukumbi wa Salama Bwawani Mjini Unguja. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akitoa hutuba yake kwa wananchi wakati sherehe za kukabidhi Vihori kwa wakulima wa mwani katika ukumbi wa Salama Bwawani Hotel Mjini Unguja leo. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akitoa hutuba yake kwa wananchi wakati sherehe za kukabidhi Vihori kwa wakulima wa mwani katika ukumbi wa Salama Bwawani Hotel Mjini Unguja leo.

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
WIZARA ya Biashara Viwanda na Masoko, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto zimeagizwa kufanya kazi kwa karibu na wakulima wa mwani ili kuhakikisha kuwa bei wanayolipwa wakulima hao inalingana na nguvu na gharama wanazozitumia sambamba na hali halisi ya bei ya bidhaa hiyo katika soko la nje.

Rais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa agizo hilo leo huko ukumbi wa Salama, katika Hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar mara baada ya kukabidhi vihori vya kubebea mwani kwa wakulima wa mwani wa Unguja na Pemba.
Katika hotuba yake Dk. Shein alisema kuwa ni wajibu wa Serikali kuwaunga mkono wananchi kwa kuwajengea uwezo, ikiwemo kuwapatia masoko, mafunzo muhimu na fursa za mikopo pamoja na kuongeza kasi katika kutafuta masoko mapya.

Dk. Shein alisema kuwa dhamira ya Serikali ni kutaka kuona kuona kuwa wakulima wa zao la mwani wanaongeza kiwango cha uzalishaji wa mwani na uwezo wao wa ubunifu katika kutumia rasilimali zilizoizunguka Zanzibar, ili waweze kujikwamua kiuchumi na kufikia malengo la Mpango wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupambana na Umasikini Zanzibar awamu ya pili (MKUZA II).
Aidha, Dk. Shein alieleza haja ya kufanywa utaalamu uliotumika hadi bei ya karafuu ikaongezeka kufanywa pia, kwa upande wa bei ya zao la mwani huku akieleza kuwa Serikali itaendeleza jitrihada zake za kuwanga mkono wakulima wa mazao mbali mbali na kuhakikisha kuwa bei wanazolipwa kwa mazao yao inalingana na jitihada zao.
Dk. Shein alihimiza kuwepo kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH) kwa ajili ya kufanya utafiti juu ya njia bora za kuzalisha zao hilo ikiwa nji pamoja na kuwatafutia wakulima mbegu bora.
Pia, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa nasaha zake kwa wale wote waliobahatika kupewa vihori hivyo kuvifanyia kazi ipasavyo na kuvitunza huku akiahidi Serikali kuendelea kutafuta njia zaidi za kuwasaidia wakulima wa mwani hapa nchini.

“ Vihori hivi vya kisasa vitawapa nafuu wakulima wa mwani, hasa wanawake.. nafahamu jitihada za kina mama katika uzalishjaji wa zao hili..matarajio yangu ni kuwa vihori hivi vitasaidia kuondoa tatizo la ubebaji na vitatoa msukumo katika kuongeza kiwango cha uzalishaji na hatimae muongeza kipato cha wakulima’,alisema Dk. Shein.
Kwa upande wa utunzaji wa mazingira, Dk. Shein aliwataka wakulima wa mwani kukumbuka kuwa wakidharau umuhimu wa kuyatunza mazingira wataweza kuathiri shughuli za uvuvi na hata za utalii na kusisitiza kuwa kuweka safi mazingira ni jambo muhimu sana.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza azma ya serikali katika kuimarisha sekta ya uvuvi ambayo hapo siku za nyuma ilikuwa na mafanikio makubwa na hivi karibuni kukabiliwa na changamoto na kusisitiza kuwa Serikali imeandaa Sera ya Mkifugo na Uvuvi, ina mpango wa kuanzisha Kampuni ya uvuvi, kununua boti za maaluma na za kisasa za uvuvi na kuanzisha kiwanda cha kusindika samaki hapa nchini.

Alisema kuwa tayari Serikali imeshafanya mazungumzo na mwekezaji kutoka nje kwa ajili ya kuwekeza  kwenye sekta ya uvuvi kwa kuanzia na rasilimali ziliopo nchini.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali itasimamia ipasavyo mambo yote ya msingi katika masuala yua uwezeshaji, ili kuona wakulima wa zao la mwani na mazao mengine wanakua na kuondokana na changamoto zinazowakabili na kukuza kipato chao.

Kabla ya hotuba yake Dk. Shein alikabidhi vihori hivyo kwa vikundi vya Unguja na Pemba kwa niaba ambapo mapema katika vuiwanja vya ukumbi huo alikagua maonyesho maalum yaliohusisha bidhaa mbali mbali zilizotengenezwa kwa kutumia mwani zikiwemo mafuta, sabubi za kukogea na kufulia pamoja na vyakula mbali mbali vinavyopikwa kwa kutumia mwani na mazao mengine ya bahari.
Naye Waziri wa Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Bi Zainab Omar Mohammed, alieleza mikakati iliyowekwa na Wizara yake katika kuhakikisha zao hilo linapata mafanikio.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Bi  Asha Ali Abdalla alisema kuwa moja ya majukumu ya Wizara ni kusaidia uanzishwaji wa  makongano ya biashara, kama miongoni mwa mikakati ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Alisema kuwa wazo la upatikanaji wa vihori hivyo linatokana na utafiti mdogo uliofanywa na mfanyakazi  wa kujitolea kutoka Shirika la Kimataifa la Huduma za Kujitlea Bwana Hossein Chehrzade kwa kushirikiana na wafanyakazi wa Idara ya Uratibu na Uendeshaji wa Programu za Uwezeshaji Wananachi Kiuchumi, pamoja na Dk. Flower Msuya wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Bahari Tanzania.

Katibu Asha alisema kuwa jumla ya vihori 100 vimenunuliwa kwa kuazia na vitagawiwa Unguja na Pemba kwa uwiano wa 30 kwa Unguja na 70 kwa Pemba ambapo jumla ya vikundi vidogo vidogo 63 vya wakulima wa mwani na wakulima mmoja mmoja 14 watanufaika na vihori hivyo.

Aidha, alisema kuwa wanufaikaji wote wa mradi huo ni 448, kati ya hao 313 ni kutoka Pemba na 135 Unguja, wakiwemo wanawake 364 na wanaume 84 na kusisitiza kuwa vihori hivyo vina uwezo wa  kubeba kilo mia nne za mwani mbichi kwa mara moja.

Alisema kuwa kwa kutumia vihori hivi, uwezo wa wakulima wa kubeba mwani kupeleka ufukweni utaongezeka kutoka kilo 50 hadi kilo 400, sawa na ongezeko la asilimia 87.5, ongezeko ambalo linatarajiwa kuongeza uzalishaji wa mwani hapa Zanzibar sambamba na kuongeza kipato kwa wakulima wa zao hilo.

Nao wakulima wa zao la mwani katika risala yao walieleza kuwa kutokana na upatikanaji wa vihori hivyo wataweza kuongeza uzalishaji, kuokoa mwani mwingi ambao hubururwa na maji na kukuza soko la mwani hapa Zanzibar.

Wakulima hao wa mwani waliiomba Serikali kufanya kila liwezekanalo kuwapatia mambo yote ya msingi yatakayopelekea kuimarika na kudumu kwa shughuli zao za mwani ikiwemo kupandishiwa bei kwa zao hilo.

Sambamba na hayo waliahidi kuvitunza vihori hivyo na kufuata masharti yote ambayo wamepewa ili vihori hivyo viweze kudumu kwa muda mrefu na kuongeza uzalishaji wa mwani hapa nchini.

Nao Wawakilishi kutoka COSTECH pamoja na kutoka Shirika la Kimataifa la Huduma za Kujitolea VSO, waliahidi kuendelea kuwaunga mkono wakulima wa zao hilo mwani hapa Zanzibar ili liendelee kutoa ajira na kuongeza kipato cha wakulima na Taifa kwa jumla.
Katika hafla hiyo viongozi mbali mbali walihudhuria wakiwemo Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, viongozi wa Serikali na wananchi mbali mbali wakiwemo wakulima wa mwani kutoka Unguja na Pemba ambapo pia, shughuli hiyo ilipmbwa kwa ngoma ya Kibatim utenzi.

No comments:

Post a Comment