Balozi Seif akimkabidhi Fundi Mkuu wa Wadogo Gereji Bwana Hussein Moh’d Said Zana za Ufundi akitekeleza ahadi aliyowapa wanachama wa kikundi hicho cha ufundi zitakazowasaidia katikia harakati zao za kujitafutia mapato. (Picha zote na Hassan Issa–OMPR – ZNZ)
Na Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
26/3/2015.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema licha ya Serikali kujitahidi kutafua mbinu za kukabiliana na tatizo la ajira lakini wananchi wenyewe hasa Vijana waliomaliza masomo yao wana fursa na wajibu wa kuunda vikundi vya ujasiri amali vitakavyoweza kusaidia kukabiliana na tatizo hilo.
Alisema suala la ajira hivi sasa limekuwa changamoto kubwa inayoikabili Dunia ambapo hata Mataifa yaliyoendelea kiuchumi yanaguswa na changamoto hiyo inayoweza kupungua iwapo jitihada kati ya Serikali ya taasisi Binafsi zitashirikiana katika kuunganisha nguvu za pamoja.
Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akikabidhi zana za Kiufundi { Tools Box } kwa Kikundi cha Vijana wajasiri amali cha Wadogo Garage hapo Hoteli ya Hifadhi Tibirinzi Mjini Chake chake kufuatia ziara yake ya hivi karibuni aliyoifanya Kisiwani Pemba.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikuwa akitekeleza ahadi aliyowapa Vijana hao wenye mastakimu yao katika Mtaa wa Wete mkabala ya Jengo la Posta ambao wanaojishughulisha na shughuli za ufundi wa Magari, Vespa, Piki piki pamoja na Mashine zinazotumia umeme.
Alisema juhudi mbali mbali zitachukuliwa na Serikali Kuu katika kuona vijana hao wanapata zana kamili zitakazokidhi mahitaji yao ya kiufundi na kuwataka kuhakikisha kwamba wateja wanaowahudumia wanalipa fedha za matengenezo kutokana na vyombo wanavyopeleka ili fedha zinazokusanya zisasaidie kuendesha maisha yao ya kila siku.
Aliwapongeza vijana hao wa Kikundi cha ufundi cha Wadogo Gereji kwa uamuzi wao wa kujikusanya pamoja na kuanzisha miradi itakayotowa mwanga katika kukabiliana na ukali wa maisha hapo baadaye.
Balozi Seif amekuwa akisisitiza kwamba Serikali imeanzisha mfuko wa Uwezeshaji kupitia Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana Wanawake na Watoto ambao umelenga kuwasaidia wananchi waliojikusanya pamoja kwa kupatiwa mikopo ya kuendesha miradi yao ya Kiuchumi.
Nao Vijana hao wa Wadogo Gereji Wete Pemba walimshukuru na kumpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa jitihada zake anazoendelea kuzichukuwa kila kukicha katika kujaribu kusaidia kuunga mkono jitihada za wananachi mbali mbali walioamua kujiletea maendeleo kupitia vikundi vya wajasiri amali.
Walisema juhudi za Balozi Seif ziko wazi na kushuhudiwa na Wananchi waliowengi Nchini na zinapaswa kuungwa mkono sambamba na kuigwa na Viongozi wengine wa Taasisi za umma na hata zile za kiraia zinazotoa huduma za maendeleo na kiuchumi hjapa Nchini.
Wakizungumzia changamoto wanazopambana nazo vijana hao wa Wadogo Gereji walisema kuwa ni pamoja na ukosefu wa sehemu maalum ya kufanyia shughuli zao za kiufundi, umuhali walionao kwa wateja wao pamoja na ukosefu wa fursa za masomo kwa nia ya kuongeza ujuzi waliokuwa nao.
Kikundi cha wajasiri amali cha Wadogo Gereji kilichoanzishwa miaka kadhaa iliyopita Chini ya Fundi Mkuu Nd. Hussein Moh’d Said kikiwa na wanachama 29 hivi sasa tayari kimeshafungua Tawi jengine la Kiufundi katika Kijiji cha Tumbe.
No comments:
Post a Comment