TANGAZO


Wednesday, February 25, 2015

Ziara ya Waziri Migiro Tume ya Haki za Binadamu

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Asha-Rose Migiro na Naibu wake, Mhe. Ummy Mwalimu wakiongea na Mwenyekiti wa THBUB, Mhe. Bahame Tom Nyanduga ofisini kwake mara baada ya kuwasili katika taasisi hiyo.
Mwenyekiti wa THBUB, Mhe. Bahame Tom Nyanduga akieleza mipango ya Tume katika kipindi kijacho wakati wa kikao hicho kabla ya kumkaribisha Mhe. Waziri kuongea na viongozi wa Tume.
Katibu Mtendaji wa THBUB, Bibi Mary Massay akitoa taarifa fupi kuhusu utekelezaji wa shughuli za Tume kwa Mhe. Waziri na ujumbe wake wakati wa kikao hicho.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Asha-Rose Migiro akiongea katika kikao chake na viongozi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), alipotembelea taasisi hiyo jana (Februari 24, 2015). Kushoto ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Ummy Mwalimu na Kulia ni Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mhe. Bahame Tom Nyanduga.
Makamu Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Iddi Ramadhani Mapuri akitoa neno la shukrani kwa Mhe. Waziri wakati wa kikao chake na viongozi wa Tume.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Asha-Rose Migiro (katikati) na Naibu wake, Mhe. Ummy Mwalimu (wa kwanza kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na makamishna wa Tume na wajumbe wa Sekretarieti ya Tume.
 Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Asha-Rose Migiro (katikati) na Naibu wake, Mhe. Ummy Mwalimu (wa kwanza kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na makamishna wa Tume na wajumbe wa Sekretarieti ya Tume.
Mwenyekiti wa THBUB, Mhe. Bahame Tom Nyanduga akimkabidhi Mhe. Ummy Mwalimu baadhi ya machapisho yaliyoandaliwa na Tume. (Picha zote na Mbaraka Kambona wa THBUB)

Na Germanus Joseph
FEBRUARI 24 mwaka, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Asha-Rose Migiro alifanya ziara fupi ya kuitembelea Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora katika ofisi zake zilizoko Mtaa wa Luthuli jijini Dar es Salaam. Katika ziara hiyo aliambatana na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Ummy Mwalimu. Lengo la ziara yao lilikuwa kufahamiana na kubadilishana mawazo na viongozi wa Tume.

Akiongea katika kikao chake na viongozi wa Tume, pamoja na mambo mengine, Mhe. Waziri aliitaka Tume kuendelea kuwahimiza wananchi, serikali na vyombo vyake kuzingatia haki za binadamu ili kudumisha amani iliyopo nchini; kuisaidia Serikali kwa kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuleta ufumbuzi wa changamoto zilizopo za haki za binadamu na utawala bora na kuongeza nguvu katika kuhakikisha kuwa haki zilizomo katika Katiba Inayopendekezwa ambazo ni nyingi kuliko zilizoko ndani ya Katiba ya sasa zinafahamika, zinalindwa, kutetewa na kutekelezwa kikamilifu.

Vilevile Mhe. Dkt. Migiro alizungumzia kuhusu taarifa za mwaka za Tume kujadiliwa bungeni. Alisema kuwa hilo ni jambo zuri kwa kuwa litasaidia siyo tu wananchi kujua utendaji wa chombo chao, bali pia taasisi nayo itapata mrejesho utakaosaidia kuboresha utendaji kazi wake. Aliahidi kulishughulikia suala hili ili taarifa hizo zipate fursa ya kujadiliwa na wabunge.

Kwa hivi sasa taarifa za mwaka za Tume zinawasilishwa bungeni lakini hakuna msukumo wa kisheria wa kuzijadili taarifa hizo.

Mhe. Waziri alitumia fursa hiyo kuwapongeza Wahe. Makamishna wapya kwa kuteuliwa kwao, pia aliipongeza Tume kwa utendaji wake licha ya kukabiliwa na changamoto nyingi.

Akiongea mapema katika kikao hicho, Mwenyekiti wa THBUB, Mhe. Bahame Tom Nyanduga alibainisha kuwa taasisi yake inakabiliwa na changamoto kadhaa katika utekelezaji wa majukumu yake. 

Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni upungufu wa rasilimali fedha, kutojadiliwa kwa taarifa za mwaka za Tume bungeni, na upungufu na uchakavu wa vitendea kazi. Zifuatazo hapa chini ni baadhi ya picha za ziara hiyo.

No comments:

Post a Comment