Mgeni rasmi katika Uzinduzi huo, Balozi Antilla akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Mfumo wa Mtandao wa Upatikanaji Taarifa za Ardhi Zanzibar.
Meneja wa mradi wa ZALIS, Nd. Moh’d Zahran (kushoto), akitoa maelezo ya kitaalamu kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nd. Ali Khalid Mirza (kulia) na Mgeni rasmi Balozi Antilla wa Finland inchini Tanzania.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Zanzibar, Nd. Ali Khalid Mirza, akiwa katika Mkutano na Vyombo vya Habari mara baada ya kumalizika kwa uzinduzi huo.
Na Abdulla Ali
Maelezo-Zanzibar 18/02/2015
BALOZI wa Finland nchini
Tanzania Bi Sinnika Antilla amesema Zanzibar itaondokana na umasikini pindipo itakua
na utekelezaji juu ya Sera ya Utunzaji na
Utumiaji mzuri wa Ardhi.
Hayo ameyaeleza katika
ukumbi wa Idara ya Ardhi iliyoko Forodhani Mjini Zanzibar wakati wa Uzinduzi wa
Mfumo wa Mtandao wa Upatikanaji Taarifa za Ardhi Zanzibar unaojulikana kama
(Zanzibar Land Information Service) (ZALIS).
Amesema huo utakuwa na
lengo la kushughulikia changamoto za Ardhi na kuwa chachu ya maendeleo ya
kiuchumi kwa kuweka sera nzuri za mazingira nchini Zanzibar.
Aidha amefahamisha kuwa
ZALIS ina lengo la kuhakikisha kuwa Ardhi inatumika vizuri pamoja na kuwepo
uongozi ulio bora wa Ardhi nchini Zanzibar ili ije iwe ni urithi mzuri na wenye
manufaa kwa vizazi vijavyo.
Balozi Antilla ameipongeza
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuanzisha Mtandao wa Serikali (E-Government)
uliorahisisha kufanikiwa kwa mradi huo pamoja na kuushukuru uongozi wa Idara ya
Ardhi kwa ushirikiano wao katika kufanikisha mradi huo wenye malengo makubwa ya
kijamii na kiuchumi kwa nchi hizo mbili.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara
ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Zanzibar Nd. Ali Khalid Mirza amesema mradi
wa ZALIS umepelekea kuwepo kwa matumizi mazuri ya maliasili hususan Ardhi na Misitu
ambapo hadi sasa zaidi ya 40% ya Ardhi ya Zanzibar imefanyiwa usajili na
asilimia zaidi ya 30% ya Ardhi hiyo inatumika kwa ajili ya kilimo jambo ambalo
limeimarisha kilimo na kupelekea kukua kwa kiasi kikubwa uchumi wa wananchi wa
Zanzibar.
Amefahamisha kuwa mradi
wa mtandao huo utasaidia kutunza kumbukumbu kwa njia iliyo salama ya mtandao na
kuepusha kupotea kwa taarifa za wateja pamoja na kuwataka watendaji wa Idara hiyo
kuwapa elimu wananchi wasio na uelewa juu ya matumizi na umuhimu wa mtandao
huo.
Ametanabahisha kuwa
kuna changamoto nyingi zinazoikabili idara hiyo wakati wa usajili ikiwemo
baadhi ya wananchi kutokuwa na vyeti vya kuzaliwa pamoja na baadhi ya Ardhi kuwa
na migogoro ya mirathi hivyo kushindwa kuzifanyia usajili kwa wakati.
Amesema usajili wa Ardhi
ulianza mnamo mwaka 2013 ukianzia na Mji Mkongwe, Mikoroshoni, Miembeni na
maeneo mengine mbalimbali Unguja na Pemba na hadi sasa bado unaendelea hivyo
amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo ili kuzifanya Ardhi zao
kuwa katika hali ya usalama kutokana na Dhulma na Wizi jambo ambalo kwa sasa limekithiri
kwa kiasi kikubwa nchini.
No comments:
Post a Comment