*Bomoa bomoa kuwakumba
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Alphayo Kidata (kulia) bakitoa tathmini ya zoezi la bomoa bomoa awamu ya tatu linaloendelea katika Manispaa ya Kinondoni jana jijini la Dar es salaam. Kulia ni Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni, Baraka Mkuya. Baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Bw. Alphayo Kidata (hayupo pichani) alipokuwa akitoa tathmini ya zoezi la bomoa bomoa kwa wananchi waliovamia maeneo yanayomilikiwa kisheria na watu wengine katika manispaa ya Kinondoni jana jijini Dar es Salaam.
Moja ya ukuta uliojengwa kinyume cha sheria katika eneo lisiloruhusiwa eneo la Tegeta ukibomolewa jana.
Baadhi ya wananchi katika manispaa ya Kinondoni wakiondoa bidhaa zo katika maduka eneo la Tegeta Machakani kupisha zoezi la bomoa bomoa kufuatia maduka hayo kujengwa eneo lisiloruhusiwa, jana jijini Dar es Salaam. Fundi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), akiendelea na zoezi la kukata umeme eneo la Mikocheni B kufuatia zoezi la bomoa bomoa lililokuwa likiendeshwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Manispaa ya Kinondoni, jana jijini Dar es Salaam.
Askari wa Jeshi la Polisi wakiwa wameimarisha ulinzi wakati wa zoezi la bomoa bomoa maeneo ya wazi na yale yaliyochukuliwa kinyume cha sheria kutoka kwa wananchi wanaoyamiliki kihalali eneo la Mikocheni na Tegeta jijini Dar es Salaam.
Na Aron Msigwa –MAELEZO, Dar es salaam.
Dar es Salaam.
28/2/2015.
WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imesema kuwa itaendelea na zoezi la kuvunja nyumba zilizojengwa katika maeneo ya wazi na yale yaliyochukuliwa kwa nguvu kinyume cha sheria kutoka kwa wananchi wanaoyamiliki kihalali katika maeneo mbalimbali nchini.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es salaam na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Alphayo Kidata alipokuwa akitoa tathmini ya zoezi la bomoa bomoa awamu ya tatu linaloendelea katika Manispaa ya Kinondoni jijini la Dar es salaam.
Alisema kuwa wizara imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi ambao maeneo yao yamevamiwa na watu wengine kinyume cha sheria ambayo wao wanayoyamiliki kihalali.
Alieleza kuwa kutumia kanuni na taratibu zinazosimamia umiliki na matumizi ya ardhi nchini wizara hiyo itaendelea kuchukua hatua na kuyabaini maeneo yote yenye migogoro inayosababishwa na baadhi ya wananchi wasio na nyaraka halali za umiliki kisheria kuingia kwenye viwanja vya wananchi.
“Sisi kama wizara tumekubaliana kuwa zoezi hili litakuwa endelevu, wale wote waliovamia maeneo ambayo sio yao yakiwemo maeneo ya wajane na kujenga majengo yao Serikali itayabomoa kwa nguvu hata kama wamejenga maghorofa na Hoteli” Amesisitiza.
Alisema kwa muda mrefu pamekuwa na wimbi kubwa la migogoro ya ardhi inayosababishwa na tabia ya wananchi wasio na nyaraka kisheria kuingia kwenye viwanja vya watu wengine wenye hati za kumiliki ardhi kihalali na kuviendeleza kiuvamizi pasipokuwa na vibali vyovyote vya ujenzi.
Bw. Kidata alibainisha kuwa vitendo wanavyofanya wananchi hao ni kosa la jinai na kinyume cha sheria ya ardhi namba 4 ya mwaka 1999 kifungu namba 175(1) kinachozuia mwananchi yeyote kuingia na kuendeleza kwenye ardhi asiyoimiliki kisheria.
Alisisitiza kuwa hakuna raia yeyote wa Tanzania aliye juu ya sheria hivyo watanzania bila kujali hali walizo nazo wanao wajibu wa kutii na kufuata sheria za nchi zinazosimamia sekta ya ardhi na kuongeza kuwa Serikali haitamvumilia yeyote atakayeendesha vitendo vya kuhujumu maeneo ya wazi, kujenga kuta katika maeneo yasiyoruhusiwa na kuvamia maeneo ya hidhadhi ya Bahari.
Kwa upande wake Muhandisi wa Manispaa ya Kinondoni, Baraka Mkuya ambaye zoezi hilo lilifanyika katika manispaa anayoisimamia ameeleza kuwa awamu ya tatu ya zoezi la bomoa bomoa katika manispaa hiyo limehusisha ubomoaji wa kuta, majengo na maduka katika maeneo ya tofauti ya kata Mikocheni B na Tegeta.
Aliongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maenedeleo kwa kushirikiana na manispaa ya Kinondoni na vyombo vya ulinzi na usalama itaendelea na zoezi hilo ili kusimamia sheria za nchi kutokana na baadhi ya wananchi kwa makusudi kuendesha vitendo vya hujuma na vurugu miongoni mwa jamii.
“Kwa upande wetu kama manispaa ya Kinondoni kwa kushirikiana na Wizara na vyombo vya ulinzi na usalama, tutalifanya zoezi hili kuwa endelevu ili tuweze kuondoa kabisa migogoro ya ardhi katika manispaa yetu” Alisisitiza.








No comments:
Post a Comment