TANGAZO


Sunday, February 15, 2015

Maandalizi Sensa ya Viwanda yakamilika

*Serikali yawataka wadau kutoa ushirikiano
 Makamu Mkuu wa chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika Dkt. Tumaini Katunzi akizungumza na wasimamizi na wadadisi wa Sensa ya Viwanda itakayofanyika nchi nzima kuanzia Februari 23 mwaka huu jana jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga mafunzo ya wadadisi hao. (Picha zote na Veronica Kazimoto)
 Baadhi ya wadadisi wa Sensa ya Viwanda wakifuatilia hafla ya ufungaji wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kukusanya takwimu za Sensa ya Viwanda ya mwaka 2013 iliyofanyika jana katika Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika eneo la Changanyikeni jijini Dar es Salaam.
 Kamishna wa Viapo ambaye pia ni Mwanasheria wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Oscar Mangula akitoa ufafanuzi kwa wasimamizi na wadadisi wa Sensa ya Viwanda (hawapo pichani) kuhusu Sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia Sensa ya Viwanda ya mwaka 2013 inayotarajia kufanyika nchi nzima kuanzia Februari 23, 2015.
Baadhi ya wadadisi wa Sensa ya Viwanda wakisaini fomu za viapo vyao mbele ya Kamishna wa Viapo Bw. Oscar Mangula (hayupo pichani) jana jijini Dar es Salaam mara baada ya kuhitimu mafunzo  ukusanyaji wa takwimu  za Sensa ya Viwanda 2013 itakayofanyika Februari 23 mwaka huu. 
Wadadisi wa Sensa ya Viwanda 2013 wakiapa mbele ya Kamishna wa Viapo  Bw. Oscar Mangula (hayupo pichani) jana jijini Dar es salaam mara baada ya kuhitimu mafunzo ya siku 14 ya kuwajengea uwezo wa ukusanyaji wa takwimu  za Sensa ya Viwanda 2013 itakayofanyika nchi nzima kuanzia Februari 23 mwaka huu. 
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa  akifunga rasmi mafunzo ya siku 14 ya wasimamizi na wadadisi wa Sensa ya viwanda 2013 itakayofanyika nchini nzima kuanzia Februari 23,2015. Hafla ya kufunga mafunzo hayo ilifanyika jana eneo la  Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika jijini Dar es salaam. 
Wadadisi wa Sensa ya Viwanda 2013 wakiapa mbele ya Kamishna wa Viapo  Bw. Oscar Mangula (hayupo pichani) jana jijini Dar es salaam mara baada ya kuhitimu mafunzo ya siku 14 ya kuwajengea uwezo wa ukusanyaji wa takwimu  za Sensa ya Viwanda 2013 itakayofanyika nchi nzima kuanzia Februari 23 mwaka huu.
Na Aron Msigwa – MAELEZO.
15/2/2015, Dar es salaam.
SERIKALI imesema kuwa maandalizi ya Sensa ya Viwanda ya mwaka 2013 itakayofanyika nchi nzima kuanzia Februari 23 mwaka huu yamekamilika na  kuwataka wamiliki wa viwanda na wadau mbalimbali kutoa ushirikiano kwa wadadisi watakaopita katika maeneo yao kukusanya takwimu wakati wa Sensa hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mafunzo na kuwaapisha wasimamizi na wadadisi wa Sensa ya Viwanda ya mwaka 2013 iliyofanyika katika Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika jana jijini Dar es Salaam ,  Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa alisema kuwa maandalizi ya awali ya Sensa hiyo yamekamilika yakihusisha uhamasishaji wa ushiriki wa wenye viwanda kwenye Sensa hiyo, utoaji wa elimu kwa wadadisi na wasimamizi watakaoendesha zoezi hilo.

Alisema kuwa kutokana na umuhimu wa Sensa hiyo  wamiliki wa viwanda katika maeneo mbalimbali watashiriki kutoa takwimu zitakazojazwa katika madodoso maalum yaliyoandaliwa  ili kuliwezesha taifa kuweka Sera na mipango ya maendeleo inayotokana na takwimu sahihi za viwanda vilivyopo nchini.  
Aliongeza kuwa mafanikio ya Sensa hiyo yatatokana na wamiliki wa viwanda kutambua na kuithamini Sensa hiyo kwa kutoa ushirikiano wa kuwapatia  takwimu sahihi wadadisi watakaopita katika maeneo yao kukusanya taarifa zinazohusu masuala mbalimbali yakiwemo ya uzalishaji wa bidhaa na masuala ya ajira.
Dkt. Chuwa alibainisha kuwa upatikanaji wa takwimu sahihi kuhusu Sekta ya Viwanda nchini Tanzania utaiwezesha Serikali kutambua mchango wa viwanda katika ajira, uzalishaji na pato la taifa hivyo kuweka Sera na mipango endelevu ya maendeleo itakayoliwezesha taifa na sekta hiyo  kupiga hatua kimaendeleo.

“Sensa hii ya viwanda ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu, na mafanikio yake yatatokana na wenye viwanda kutupa ushirikiano maana bila  wao kutoa takwimu sahihi mipango ya maendeleo kuhusu viwanda haitatekelezeka kwa sababu ya kukosa takwimu sahihi” Amesisitiza Dkt. Chuwa.

Kuhusu wasimamizi na wadadisi  watakaoendesha zoezi hilo  litakalofanyika kwa muda wa miezi 3, Dkt. Chuwa aliwataka wafuate  sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa  ili kuwezesha upatikanaji wa takwimu bora.

Naye Mkurugenzi wa shughuli za Takwimu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Aldegunda Komba akizungumza na wadadisi hao alisema kuwa wadadisi hao wamepewa dhamana kubwa ya kutimiza lengo liliowekwa na Serikali la kuwa na takwimu sahihi kuhusu mchango wa viwanda katika maendeleo ya taifa.
“Mafunzo tuliyowapatia  kwa vitendo na nadharia yamewajengea uwezo wa kukusanya takwimu bora, tunaomba zoezi hili mlifanye vizuri tunatarajia mtaitumia vizuri elimu mliyoipata kwa kufanya kazi kwa umakini mkubwa kwa manufaa ya taifa letu”. Amesisitiza Bi. Komba.

Aidha, alibainisha kuwa kukamilika kwa Sensa hiyo kutaliwezesha taifa kutambaua mchango wa Sekta ya Viwanda katika uchumi na pato la taifa.

Kwa upande wake Kamishna wa Viapo ambaye pia ni Mwanasheria wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Oscar Mangula akizungumza na wasimamizi na wadadisi wa Sensa hiyo aliwataka kuzingatia  Sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia zoezi.
Alisema kuwa zoezi hilo litapata mafanikio makubwa kufuatia wadadisi na wasimamizi hao kuzingatia mafunzo na taratibu walizoelezwa huku akibainisha kuwa sheria  itachukua mkondo wake kwa wote watakaoshiriki kwa namna yoyote ile kuvuruga zoezi hilo.

“Napenda niwaeleze kwamba zoezi hili ni muhimu sana kwa uchumi wa taifa,nawaomba mzingatie yote mliyoambiwa mtakapokuwa mnakusanya takwimu, zingatieni uadilifu na utunzaji wa takwimu mtakazopata kwa kuhakikisha mnaziwasilisha kwa wahusika kwa mujibu wa sheria na si vinginevyo” Alisisitiza.

No comments:

Post a Comment