Kaimu Kamishna Msaidizi Kitengo cha huduma kwa familia, watoto, malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Philbert Kawemama (kulia), akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, wakati akifungua semina ya siku moja inayohusu watoto waishio katika mazingira hatarishi na kongamano la watoto hao litakalofanyika Februari 18 hadi 20 mwaka huu katika ukumbi wa Mwalimu J.K Nyerere Convention Centre. Kushoto ni Kaimu Kamishna Msaidizi Huduma kwa Wazee na Watu wenye Ulemavu, Ernest Karubi.
Kaimu Kamishna Msaidizi Huduma kwa Wazee na Watu wenye Ulemavu, Ernest Karubi akizungumza na wanahabari wakati akifunga semina hiyo.
Ofisa Ustawi wa Jamii, Johnas Tarimo akitoa mada kuhusu mahabusu za watoto.
Naibu Mkurugenzi wa Programu wa Shirika la Pact/Pamoja Tuwalee, Linda Madeleka (kushoto), akichangia mada katika semina hiyo.
Ofisa wa Ustawi wa Jamii, Vailet Mollel akifafanua mambo mbalimbali katika semina hiyo.
Maofisa kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wakiwa kwenye semina hiyo.
Wanahabari wakiwa kwenye semina hiyo.
Wanahabari wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa katika semina hiyo.
Na Dotto Mwaibale
WANAHABARI nchini wametakiwa kuandika habari za watoto kwa kuzipa kipaumbele kama wanavyofanya katika matukio mengine ili kulisaidia kundi hilo lenye changamoto kubwa.
Mwito huo umetolewa na Kaimu Kamishna Msaidizi Huduma kwa Wazee na Watu wenye Ulemavu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Ernest Karubi Dar es Salaam leo wakati akifunga semina ya siku moja inayohusu watoto waishio katika mazingira hatarishi na kongamano la watoto hao litakalofanyika Februari 18 hadi 20 mwaka huu katika ukumbi wa Mwalimu J.K Nyerere Convention Centre.
"Nyinyi wanahabari ni watu muhimu sana katika kuandika kwa undani habari zinazowahusu watoto ambao wapo katika mazingira hatarishi ili jamii izijue changamoto zao na kuwasaidi" alisema Karubi.
Alisema waandishi wa habari wamekuwa jirani zaidi na wanasiasa hivyo akawaomba pia wawageukie watoto katika kuandisha taarifa zao kwa kuzingatia maadili hasa matumizi ya picha zao.
Karubi aliwaomba wanahabri kujenga tabia ya kuzitembelea ofisi za serikali hasa za ustawi wa jamii kwa ajili ya kupata taarifa za watoto.
Kaimu Kamishna Msaidizi Kitengo cha huduma kwa familia, watoto, malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Philbert Kawemama alisema serikali imepata mafanikio makubwa baada ya kuanzisha mpango wa ulinzi na usalama kwa watoto.
Alisema halmashauri 30 nchini tayari zimefikiwa na mpango huo wa ulinzi na usalama kwa watoto jambo ambalo ni mafanikio na lengo ni mpango huo kuwa nchi nzima.
Kawemama alisema mpango wa serikali ni kushirikiana na wadau wengine ili kuwawezesha watoto hao kiuchumi badala ya kuwa tegemezi na kuweka utaratibu ambao utahakikisha shughuli zote zinazohusu watoto zinatekelezeka.
(Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com)
No comments:
Post a Comment