Katibu Mkuu
Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw.
Jumanne Sagini akitoa wito kwa wananchi kujitokeza kupiga kura hapo kesho
wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kuchagua viongozi watakaosaidia
katika kuwaletea maendeleo, Pia aliwataka Wananchi kuepuka vitendo vya uvunjifu
wa Amani kwani hatua kali zitachukuliwa kwa wale wote watakaojaribu kuvuruga
Amani katika vituo vya kupigia kura.kushoto ni mratibu wa uchaguzi huo Bw. Denis
Bandisa. (Picha zote na Mpigapicha wetu)
Na Frank Mvungi-MAELEZO
Serikali imewataka wananchi wote waliojiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za
Mitaa kushiriki kwa wingi ili waweze
kuwachagua viongozi wao katika maeneo yao.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri
Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Jumanne Sagini wakati
wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam .
Akifafanua Sagini amesema wapiga kura wazingatie
kuwa kila mpiga kura anatakiwa kupiga kura moja tu na apige kwenye kitongoji au
mtaa anaoishi na si vinginevyo.
Pia Sagini alitoa wito kwa viongozi wa vyama vya
siasa, Asasi zisizo za Kiserikali kuwahamasisha wapiga kura kujitokeza kwa
wingi hapo kesho kuchagua viongozi wao.
Akiwatahadharisha wananchi kuhusu kupiga kura Zaidi
ya mara moja au kutaka kupiga kura wakati
si mkazi wa eneo hilo Sagini
alisema hatua kali za kisheria
zitachukuliwa kwa wale wote watakaojaribu kukiuka sheria, Kanuni na taratibu za
uchaguzi huo.
Katika uchaguzi huo sagini alibainisha kuwa
utaratibu utakaotumika ni kupiga kura,kuhesabu na kutangaza matokeo ambapo
taratibu zote zimefafanuliwa katika Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa za
mwaka 2014 na katika mwongozo wa uchaguzi huo.
Wapiga kura wote wametakiwa kufika katika maeneo ya
kupigia kura wakiwa na kitambulisho cha mpiga kura cha Uchaguzi Mkuu, Kitambulisho
cha kazi,Hati ya kusafiria,Kadi ya benki,Kadi ya Bima ya Afya,Kitambulisho cha
shule au chuo,Leseni ya Udereva au Kitambulisho cha uraia kwa ajili ya
kuwatambulisha.
Uchaguzi wa Serikali za mitaa katika ngazi za
vijiji,Mitaa na vitongoji utafanyika siku ya jumapili ya tarehe 14 Desemba,2014
ambapo katika uchaguzi huo watachaguliwa wenyeviti wa vijiji na wajumbe wa
Halmashauri za Vijiji,Wenyeviti wa Mitaa na wajumbe wa Kamati za mitaa na wajumbe
wa kamati za Mitaa na wenyeviti wa vitongoji.

No comments:
Post a Comment