TANGAZO


Monday, November 3, 2014

Waziri Nyalandu atoa wito kwa viongozi wa Dini kuhusu kukemea ujangili nchini

 
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu
 
Na Anitha Jonas – Maelezo.
03 Novemba, 2014.
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Lazaro Nyalandu ametoa wito kwa Viongozi wa dini wote nchini kupaza sauti kwa pamoja kukemea vitendo vya Ujangili pamoja na Uharibifu wa mazingira nchini.
Wito huo ameutoa leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua mkutano wa viongozi wa dini unaolenga kuwaelimisha viongozi hao kutoa elimu kwa waumini wao juu ya kupinga suala la ujangili na kuwasihi juu ya utunzaji wa mazingira.

Mhe. Nyalando alisema kuwa, vitendo vya ujangili vikiendelea vinaweza kuleta athari kubwa nchini ikiwa ni pamoja na uharibifu wa mazingira na kuharibu sekta ya utalii kwa Mbuga za wanyama.
“Serikali imeamua  kwamba,  mtu yoyote anayefanya vitendo vya kijangili akijisalimisha na kukabidhi silaha yake atasamehewa,” Alisema Mhe. Nyalando
Aliwasihi akina mama wanaojua waume zao wanaojihusisha na vitendo vya ujangili kuacha na kujisalimisha Wizarani.

Naye Sheikh Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Sheikh Alhaj Mussa Salum ameonyesha ushirikiano na kuunga mkono utoaji wa elimu hiyo kwa waumini kwani hata Quran Tukufu  inahubiri juu ya haki za wanyama, hivyo ukatili juu ya wanyama sio jambo zuri mbele za Mungu.

“Dhuluma inayofanyika kwa wanyama ni dhambi kwani Quran inasema fanyeni wema kwani mwenyezi Mungu anapenda wema” Alisema Sheikh Mussa.
Kwa upande wake Askofu wa Jimbo la Iringa Baraza ka Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa  alisema kuwa rasilimali zote zilizopo nchini ni Baraka, hivyo zinapaswa kutunzwa na kuepuka suala la ubinafsi kwa kutaka kuzitumia zote kwa haraka na kuzimaliza.
“Tufikirie na kizazi kijacho kitahitaji kunufaika na rasilimali asilia hizi, mfano miti inayochukua muda mrefu kuota pamoja wanyama wa porini”,alisema Askofu Ngalalekumtwa.

Naye mdau wa maendeleo nchini Dkt. Regnald Mengi alisema kwamba, viongozi wa dini wana nguvu kubwa katika jamii, kwani chochote wanachokisema kwa waumini wao ni rahisi kwa waumini hao kukifuata kwani wanaamini chochote kinachosemwa nao ni maagizo ya Mungu.
Mkutano huo ulihusisha viuongozi mbalimbali wa kidini wakiwemo Maaskofu, Masheikh pamoja, Wadau wa maendeleo wa UNDP pamoja na Mashirika mbalinmbali ya Wanyamapori yakiwemo TANAPA, TAWIRI, FZC, AWF, WWF, ICCF ambao wenyeji wa mkutano huo.

No comments:

Post a Comment