Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akifuatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheir wakati alipowasili katika Hoteli ya Sea Cliff kufunguasemina ya siku tatu ya Viongozi wa Juu Mikoa na Wilaya za Zanzibar.
Baadhi ya wakuu wa Mikoa na Wilaya wakiwa katika ufunguzi wa semina ya siku tatu iliyowashirikisha Makatibu Tawala wa Mikoa ya Zanzibar na baadhi ya Tanzania Bara iliyoanza leo katika ukumbi wa Sea Cliff nje kidogo ya Mji Zanzibar.
Washiriki wa katika semina ya Viongozi wa juu wa Mikoa na Wilaya za zanzibar na Baadhi kutoka Bara wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alipotoa hutuba yake ya ufunguzi wa semina hiyo leo katika Hoteli ya Sea Cliff Kama nje ya Mji wa Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein alipokuwa akitoa hutuba yake ya ufunguzi wa semina ya Viongozi wa juu wa Mikoa na Wilaya za Zanzibar na Baadhi kutoka Bara inayohusu Mahusiano na mwingiliano katika siasa na utendaji kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Makatibu Tawala wa Mikoa ya Zanzibar na baadhi Tanzania Bara leo katika Hoteli ya Sea Cliff Kama nje ya Mji wa Zanzibar.
Na Mwinyi Sadala, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza umuhimu wa viongozi katika nyanja za siasa na utawala kufahamu mipaka ya majukumu yao, kujenga ushirikiano na kuwa na mawasiliano mazuri ili kuimarisha utawala bora na kufanikisha utendaji wa shughuli za Serikali.
Dk.Shein amesema
hayo leo, wakati akifungua Warsha ya Siku Tatu kuhusu Mahusiano na Mwingiliano kati ya Siasa na Utendaji kwa
Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Makatibu Tawala wa Mikoa ya Zanzibar na baadhi
ya Tanzania Bara inayofanyika katika hoteli ya Sea Cliff nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Aliwaambia washiriki
wa warsha hiyo kuwa viongozi na watendaji kushindwa kuelewa majukumu na mipaka
yao wakati mwingine kunasababisha
baadhi yao kuyumba na kuingia katika malumbano na hatimae huathiri utendaji wao
wa kazi.
“kuelewa majukumu yako
na mipaka yake na kuyatekeleza majukumu hayo kwa mujibu wa Katiba na Sheria pamoja
na kuwashirikisha walio chini yako ni sehemu ya uimarishaji wa utawala bora
kitu ambacho Serikali zetu zimedhamiria kukijenga” Dk. Shein aliwaeleza.
Alisema litakuwa ni
jambo la kushangaza kwa Mkuu wa Mkoa kushindwa kupata mafanikio katika utekelezaji
wa majukumu yake wakati kuna mfumo mzima wa uongozi ambao anauongoza kuanzia
mkoani hadi katika ngazi ya shehia.
Katika mkutano huo
uliohudhuriwa pia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI Hawa Ghasia,
Dk. Shein alitoa wito wa kuwepo kwa ushirikiano wa karibu na mawasiliano kati
ya viongozi wa siasa na utendaji kwa kuwa ni mambo muhimu katika kufanikisha kutekeleza
mipango mbalimbali ya maendeleo ya nchini.
Dk. Shein aliwaeleza washiriki
hao ambao baadhi yao ni kutoka Tanzania Bara kuwa ipo changamoto kubwa ya
ukosefu wa usimamizi ulio makini wa shughuli za serikali katika ngazi ya mikoa
na wilaya jambo ambalo linarejesha nyuma ufanisi wa utoaji wa huduma kwa
wananchi.
Kwa hivyo aliwataka
kukumbuka kuwa wao ni sehemu ya uongozi hivyo hawana budi kuchukua hatua
madhubuti kukabiliana na hali hiyo ili Serikali ziweze kufikia malengo yake
kama yalivyoainishwa katika mipango mbalimbali ya maendeleo pamoja na Ilani ya Uchaguzi
ya Chama Tawala.
“Tekelezeni Katiba,
Sera zetu, MKUZA, MKUKUTA, Mipango mingine ya Maendeleo pamoja na Ilani yetu ya
Uchaguzi ili wananchi wazidi kujenga imani kwa serikali zao” Dk. Shein alisema.
Katika hotuba yake
hiyo ambayo alielezea pia historia na jitihada za serikali kujenga utawala wa
wananchi baada ya uhuru, Dk. Shein aliwahimiza wakuu hao wa mikoa na wilaya kuendelea
kushauriana, kuwasiliana na kutembeleana ili kubadilishana uzoefu na kuongeza
ujuzi katika kuwatumikia wananchi.
Kwa upande mwingine
aliwataka kuhakikisha kuwa fedha zinazopelekwa katika mikoa, wilaya na halmashauri
zinatumika kulingana na matumizi yaliyopangwa na pia amewataka kusimamia
ukusanyaji wa mapato ili kuongeza mapato ya serikali.
Akizungumza
kumkaribisha mgeni Rasmi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara
Maalum za SMZ Haji Omar Kheri alieleza kuwa katika kuimarisha Utawala katika
ngazi za Mikoa na Wilaya, Baraza la Wawakilishi hivi karibuni lilipitisha Sheria
mpya ya Tawala za Mikoa.
Kwa hivyo alisema,
kufanyika kwa Warsha hiyo kumekuja wakati unaofaa kwa kuwa maudhui yake yanakwenda
sambamba na jitihada hizo za Serikali kuimarisha Serikali za Mitaa.
Mapema akitoa maelezo
kuhusu warsha hiyo, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Profesa Joseph Semboja
ambayo ndio iliyoandaa warsha hiyo, alieleza kuwa lengo la warsha hiyo ni kutoa
fursa kwa washiriki kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu mpya kuongeza maarifa
katika kutekeleza majukumu yao ili kuongeza ufanisi katika utendaji.
Alifafanua kuwa warsha
hiyo imezingatia umuhimu wa maingiliano kati siasa na utendaji katika kuleta maendeleo
ya nchi na kubainisha kuwa ni muhimu maelewano hayo yakawa mazuri na yenye ushirikiano
ambapo katika hali hiyo huwa ni chachu ya maendeleo na kinyume chake kuwepo kwa
migongano kunadhoofisha jitihada za kuleta maendeleo ya nchi.
Wakuu wa mikoa kutoka
Tanzania Bara wanaohudhuria warsha hiyo ni pamoja na walioteuliwa hivi karibuni
ambao ni Dk. Ibrahim Msengi (Katavi), Halima Dendegu (Mtwara), Amina Masenza (Iringa)
na John Mongela (Kagera). Wa zamani ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit
Mwambugu na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Ludovick Mwananzila ambaye kabla ya
mabadiliko alikuwa mkoa wa Lindi.
No comments:
Post a Comment