*Watu zaidi ya 14 wafariki
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Teule wilayani Muheza Rajabu Malamhiyo (aliyesimama), akiangalia hali ya majeruhi ambaye ni dereva wa Scania iliyopata ajali, yenye namba za usajili T645 ABJ, Benjamini Abeid.Gari la abiria aina Toyota Costa, yenye namba za usajili T 410 BJD, linalofanya safari zake kutoka Tanga kwenda Lushoto, likiwa limegongana na Scania katika kijiji cha Mkanyageni, wilayani Muheza na kusababisha vifo vya watu 14 leo. (Picha zote na Glory Machare)
Na Glory Machare Muheza,
WATU zaidi ya 14 wamefariki dunia leo na wengine kumi na tisa kujeruhiwa akiwemo Katibu Tawala wa Wilaya ya Muheza, Paul Moshi katika ajali iliyohusisha gari aina ya costa lenye namba za usajili T410 BJD maarufu kama Patashika lilokuwa likitokea Tanga kuelekea Lushoto na Lori la kubebea mizigo aina ya Scania lenye namba T645 ABJ, lililokuwa likitokea Moshi kwenda Tanga kugongana uso kwa uso katika kijiji cha Mkanyageni maarufu kama kona ya Wahindi, wilayani Muheza.
Hali ya simanzi na vilio ilitawala katika eneo la tukio mara baada ya ajali hiyo kutokea baadhi ya watu waliokuwa kijiji cha jirani waliweza kufika kwa lengo la kutoa huduma ya kwanza kwa wahanga wa ajali hiyo.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga Juma Ndaki alisema kuwa ajali hiyo ilitokea majira ya saa kumi na mbili za asubuhi ambapo ajali hiyo imesababishwa na uzembe wa madereva.
Kaimu Kamanda Ndaki alisema chanzo cha ajali hiyo ni kutokana uzembe wa dereva wa Lori kuacha njia yake na kuingia upande usio wake huku akiwa katika mwendo kasi hali iliyopelekea kuivaa costa hiyo.
Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Teule Wilayani Muheza Rajabu Malamhiyo alisema mapema leo amepokea marehemu 12 na majeruhi 25 huku wengine hali zao zikiwa siyo nzuri na hivyo kuhamishiwa katika Hospitali ya Rufaa Bombo kwa ajili ya matibabu.
Aliwataja baadhi ya marehemu waliotambulika kwa majina kuwa ni pamoja na Muddy Mohamed, Zawadi Juma, Adam Shemdoe, Salimu Hassan, na Mdimu Shomari wote wakazi wa maeneo mbalimbali Mkoani Tanga.
Kaimu Mganga Mkuu aliwataja baadhi ya majeruhi kuwa ni pamoja na Clara Rupatu, Salehe Ally, Hassan Juma, Ramadhani Athumani, John Mjema, Alex Charles, Bahati Hussein na Richard Kitara.
Hata hivyo mwandishi wa gazeti hili alifanikiwa kuonana na dereva wa Lori Benjamin Abeid (34) ambaye alijeruhiwa maeneo ya mguu ambapo alidai kuwa gari hizo zilikuwa zinaovatekiana na hivyo akashindwa kukwepa na kugongana uso kwa uso.
Ikiwa jana tarehe 26/11/2014 ilikuwa siku ya maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani kwa Mkoa wa Tanga yaliyoadhimishwa katika viwanja vya Tangamano na kuhudhuriwa na watu/viongozi mbalimbali akiwemo Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani Abdi Issango aliyewahakikishia wananchi kupungua kwa ajali hizo kutokana na elimu walizozitoa kwa madereva mbalimbali.

No comments:
Post a Comment