Askofu Amos Muhagachi akitoa tamko juu ya tuhuma mbalimbali
dhidi ya kundi la 201 la wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba leo 03 Septemba,
2014 katika Ukumbi wa Spika, Mjini Dodoma.
Mwenyekiti wa kundi la 201 ya Bunge Maalum la Katiba, Mhe.
Dkt. Francis Michael akikanusha kuhusu madai ya wajumbe wa kundi hilo kupewa
rushwa kuhusu mchakato wa Katiba Mpya.
Sheikh Hamid Jongo akiviasa vyombo vya habari kutoa
ushirikiano ili kuhakikisha kuwa mchakato wa kupata Katiba Mpya unafanikiwa
kwakuwa hata wao (vyombo vya habari) unawahusu pia.
Askofu Donald Mtetemela akichangia mada wakati wa mkutano wa
kutoa tamko kuhusiana na tuhuma mbalimbali dhidi ya kundi la 201.Baadhi ya wajumbe wa kundi la 201 pamoja na waandishi wa habari wakifuatilia tamko hilo leo 03 Septemba, 2014 katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Spika Bungeni mjini Dodoma.
Baadhi ya wajumbe wa kundi la 201 pamoja na waandishi wa habari wakifuatilia tamko hilo leo 03 Septemba, 2014 katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Spika Bungeni mjini Dodoma.
Baadhi ya wajumbe wa kundi la 201 pamoja na waandishi wa
habari wakifuatilia tamko hilo leo 03 Septemba, 2014 katika mkutano uliofanyika
ukumbi wa Spika Bungeni mjini Dodoma. (Picha zote na Benedict
Liwenga, Maelezo-Dodoma)
Na Benedict Liwenga,
Maelezo-Dodoma.
03/09/2014.
WAWAKILISHI wa Taasisi za dini wa Bunge Maalum la Katiba toka
wajumbe 201 wametoa tamko lao dhidi ya tuhuma mbalimbali zinazoendelea katika
kulichafua Bunge hilo ikiwemo baadhi ya wajumbe wa kundi hilo wakituhumiwa
kudaiwa kupewa rushwa.
Tamko hilo limetolewa leo 03 Septemba, 2014 na viongozi wa
kiroho akiwemo Askofu wa Kikristo Amos Joseph Muhagachi pamoja na Sheikh Hamid
Masoud Jongo wakiwa wameongozana na Mwenyekiti wa kundi hilo la 201, Mhe. Dkt.
Francis Michael na wajumbe wengine wa kundi hilo, wakati walipofanya mkutano na
waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Spika uliopo Bungeni mjini Dodoma.
Akisoma tamko hilo, Askofu Amos Muhagachi ambaye pia ni
Mjumbe wa kundi hilo amesema kuwa kama ilivyoelezwa hapo awali kabla ya kuanza
kwa shughuli za Bunge hilo, kila mjumbe alikula kiapo cha kuwa mwaminifu na
mtiifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa kadiri ya uwezo wake na
ufahamu wake, kufanya kazi zinazomhusu bila upendeleo.
Askofu Muhagachi ameendelea kusema kuwa wameshangazwa na
kusikitishwa kuona kwamba mchakato wa
kutayarisha Katiba itakayopendekezwa na Bunge hilo kwa wananchi unachafuliwa
taswira yake, Bunge Maalum la Katiba linachafuliwa, shughuli zake kuingiliwa na
kupotoshwa na wajumbe wenzao walioko nje ya Bunge hilo, makundi, taasisi na
vyombo mbalimbali vya habari, uhalali na ukweli wa shughuli za Bunge hilo
unapotoshwa na wananchi wanaaminishwa mambo yasiyo na ukweli.
“Upotoshwaji huu umezua mijadala mbalimbali katika jamii ya Watanzania bado unaendelezwa”, alisema Muhagachi.
Aidha, Muhagachi amezitaja baadhi ya tuhuma zinazotolewa na
wajumbe wenzao dhidi ya Bunge hilo na wajumbe wa kundi hilo zikiwemo.
“Bunge Maalum la
Katiba halina uhalali kwa kuwa hao wajumbe wenzetu walioondoka wameliondolea
uhalali wake kwa vile hawapo, kwamba Kanuni za Bunge Maalum la Katiba
zinavunjwa ovyo ovyo, Kwamba kinachojadiliwa sasa katika Bunge hili ni Waraka
mwingine na si Rasimu iliyotayarishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Inadaiwa
na watu pamoja na Taasisi mbalimbali kwamba viongozi wa dini, wajumbe wa Bunge
hilo na wajumbe wa kundi la 201 kwamba wanapewa rushwa baadhi ya Vyombo vya
Habari vimeandika tuhuma hizi, pia madai mengine ni kwamba wajumbe waliomo
katika Bunge hili ni wachache ikilinganishwa na hao waliopo nje ya Bunge na
tuhuma ya nyingine ni ile ya kwamba Bunge hili lazima lisitishwe au livunjwe na
Mhe. Rais.
“Tunapenda kuwafahamisha Watanzania wenzetu kwamba mchakato
wa Katiba una hatua tatu kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na mpaka
hivi sasa ni hatua moja iliyokamilika, aidha hatua ya pili ndiyo inayoendelea
na hatua ya tatu bado haijaanza”, alisema Muhagachi.
Akitoa tamko hilo, Askofu Muhagachi amesema kuwa wao kama wawakilishi
wa Taasisi za Dini, ambao kuuhubiri, kuutangaza na kuusimamia ukweli ni moja ya
majukumu yao katika jamii, hivyo wameskitishwa na taarifa potofu zinazosambazwa
kwa makusudi na makundi, taasisi na baadhi ya vyombo vya habari.
“Tukiwa kama wajumbe wa Bunge hili ambao tunafahamu kwa kina
na tunaridhika na kila hatua ya mchakato huu, tuna wajibu wa kusahihisha
upotofu huu unaoendeshwa kwa makusudi na hivi kuwaeleza Watanzania ukweli na
hali halisi inayojiri hapa Bungeni, Watanzania msifadhaishwe na wala
msibabaishwe, hali ni shwari, mchakato unaendelea kwa amani na utulivu”,
alisisitiza Muhagachi.
Naye Sheikh Hamid Masoud Jongo ameviasa vyombo vya habari
kutilia mkazo katika kutoa taarifa zilizosahihi ili mchakato wa Katiba uendelee
kwa amani kwani nao ni moja ya kundi la watu inayowahusu.
“Vyombo vya habari vina nguvu ya kuhabarisha umma juu ya
mambo mengi yanayoendelea nchini, ni vema tukishirikiana sote kwa pamoja ili
kuhakikisha kuwa tunapata Katiba yetu kwani hata nyie Katiba hii inawahusu hasa
katika kudai haki na uhuru wa vyombo vya habari”, alisema Sheikh Jongo.
Aidha, Mwenyekiti wa wajumbe wa Kundi hilo la 201, Mhe. Dkt.
Francis Michael ameongezea kwa kukanusha suala la rushwa kwa wajumbe wake huku
akisisitiza kuwa wajumbe wake katika kundi hilo ni watu wenye heshima zao hivyo
madai hayo hayana ukweli wowote ule.
No comments:
Post a Comment