TANGAZO


Wednesday, September 24, 2014

Serikali yapambana kumkomboa mwanamke na mateso ya kiuchumi

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe. Amina Masenza, akimsikiliza mmoja wa wanawake wajasiliamali waliojitokeza wakati wa ufunguzi wa kampeni ya Mwanamke na Uchumi inayoendeshwa na Angels Moment, ambayo imelenga kuwapatia wanawake uwezo na ujuzi wa kusimamia fedha ili kuwainua kiuchumi, kibiashara na familia zao jijini Mwanza. Kushoto kwake ni Bi. Naima Malima, Mkurungezi Mkuu wa Angels Moment.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe. Amina Masenza, akihutubia wageni na wananchi mbalimbali, wakati wa ufunguzi wa kampeni ya Mwanamke na Uchumi inayoendeshwa na Angels Moment, ambayo imelenga kuwapatia wanawake uwezo na ujuzi wa kusimamia fedha ili kuwainua kiuchumi, kibiashara na familia zao jijini Mwanza.



HAYO yalisemwa na Mhe. Amina Masenza, Mkuu wa Wilaya wa Ilemela, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Mhandisi Evarist Ndikilo wakati wa ufunguzi wa kampeni ya Mwanamke na Uchumi inayoendeshwa na Angels Moment, ambayo imelenga kuwapatia wanawake uwezo na ujuzi wa kusimamia fedha ili kuwainua kiuchumi, kibiashara na familia zao.
Mhe. Ilemela alisema kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau mbali mbali imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mwanamke wa Taifa hili anakuwa huru kutoka katika mateso ya kiuchumi, ukosefu wa ajira, kuibua fursa za biashara na ujasiriamali na pia kutoa udhamini kwa wajasiriamali kupitia taasisi zake na kuwajengea uwezo wa kiuongozi katika kuongoza na kusimamia miradi yao.

Kuna fursa nyingi katika mkoa huu ambazo kama zitatumiwa vizuri kupitia kampeni hii basi wanawake wajasiriamali watajikomboa na kufanya biashara kwa uhakika zaidi na hivyo kuongeza kipato cha wanawake wa mkoa wa mwanza na taifa kwa ujumla,” alisema Mhe. Masenza.

Aliendelea kwa kusema, “Mkoa wa Mwanza kwa msiofahamu ni mkoa uliojaa fursa nyingi ambazo mwanamke kama atashiriki kikamilifu basi zitatumika ipasavyo. Hapa kuna fursa za biashara za samaki na bidhaa zake, madini, bustani za mboga mboga kwani kuna maji ya kutosha nakadhalika.”

Mkuu huyo wa wilaya alichukua fursa hiyo kuwasihi wanawake watakaoshikiri katika kampeni hii wawe chachu ya maendeleo kwa kufanya biashara endelevu yenye tija kwa kujiwekea akiba na pia kutumia faida ya biashara zao kuongeza mitaji. Pia aliwatahadharisha ni jambo la muhimu kwa akinamama kuangalia afya zao na za familia zao mara kwa mara, kwani afya bora ni chanzo cha uchumi imara.

“Kwa moyo huu wa kizalendo uliooneshwa na waandaaji wa kampeni hii, Angels Moment, nawaasa wanawake wa mkoa huu kuitumia fursa hii ili muwe waelimishaji sio kwa akina mama wengine bali kwa jamii nzima. Kama kauli mbiu ya kampeni hii inavyosema kuwa ukimuelimisha mwanamke umeelimisha jamii nzima,” alihitimisha

Naye kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Angels Moment, Bi Naima Malima amebainisha kuwa kumekuwepo na juhudi nyingi za kumkomboa mwanamke wa Tanzania ambaye ndiye nguzo ya uchumi, na jamii kwa ujumla. Lakini pamoja na juhudi hizo bado mwanamke mjasiriamali ameendelea kukumbana na changamoto mbalimbali zikiwemo za kukuza mitaji, kutambua fursa ,matumizi ya fedha, mikopo na mengineyo.

“Hali hii imepelekea mwanamke huyu kushindwa kufikia malengo yake na matokeo yake wengi kuogopa kuingia katika ujasiriamali na biashara kwa kuhofia hasara na changamoto zilizotajwa hapo juu.” Alisema Bi Malima na kuongezea, “kwa kushirikiana na wizara ya Maendeleo ya jamii, jinsia na watoto pamoja na taasisi ya WAMA tumeandaa kampeni hii ya MWANAMKE NA UCHUMI kwa kuziba changamoto hizo.”

Akifafanua elimu itakayokuwa ikitolewa na kampeni hiyo kwa wanawake katika maeneo yatakayofikiwa, alisema kuwa, “Kampeni hii itatoa elimu katika Nyanja kuu tatu ambazo ni pamoja na; Ujasiriamali na fursa zilizopo, Usimamizi binafsi wa fedha na uwekaji akiba na Afya bora na Uchumi.”

Kwa kumalizia Bi Malima aliwataka wanawake watakaofikiwa na kampeni hiyo kuitumia fursa hiyo ipasavyo kufanikisha malengo yao na kuwa mfano wa kuigwa katika jamii zao. Kwani ni kwa kipindi kirefu wanaume wamekuwa wakishikilia mfumo mzima wa uchumi ingali wao wakubaki pembeni wakitazama huku wakiwa na uwezo wa kufanya mabadiliko.

Kampeni hiyo imeanza mwezi huu wa Septemba na inatarajiwa kuzunguka katika mikoa saba iliyoteuliwa ambayo ni Mwanza, Tanga, Lindi, Pwani, Kigoma, Ruvuma na Dodoma ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

No comments:

Post a Comment