TANGAZO


Sunday, September 14, 2014

Mtambo wa mfano wa kuchakata dhahabu wazinduliwa Geita



·   *Ni mtambo wa kwanza kutumiwa na wachimbaji wadogo wa madini Afrika
·    *Serikali, Benki ya Dunia na wamiliki wa migodi mikubwa ya Madini ya Geita na Barrick washirikiana kuwezesha

Wataalamu wa kufunga mitambo katika maeneo ya machimbo wakiongozwa na supplier aliyejulikana kwa jina moja la Simon mwenye kofia wakifunga na kuujaribu mtambo huo ikiwa ni maandalizi ya uzinduzi huo.

Wataalamu wakiunganisha mitambo na wanakijiji katika kijiji cha Lwamgasa wakifuatilia kwa ukaribu shughuli inayofanyika katika kijiji chao huku wakiwa na ndoto za mafanikio.
Baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini wakiwa katika eneo lao la kazi wakifanya kazi kwa kutumia dhana duni ikiwemo na madini ya Mercury ambayo ni hatari kwa afya huku wakitarajia kunufaika na mradi na mitambo iliyofikishwa kijijini kwao kwa ukombozi wao.
Mkuu wa Wilaya ya Geita akimkaribisha mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa mradi wa mfano wa uchimbaji mdogo wa madini katika kijiji cha Lwamgasa hivi karibuni.


Naibu Naziri wa Nishati na Madini, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Bw. Stephen Masele, Mtendaji Mkuu wa Mgodi wa madini wa Geita Bw. Michael Vananen (kulia), akifuatiwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyamgusu kushoto kwa Mhe. Masele ni Mkuu wa Wilaya ya Geita, Bw. Omary Mazie Magochie, wakiwa wameshika utepe tayari kwa mgeni rasmi kukata utepe, ikiwa ni ishara ya uzinduzi.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Bw. Stephen Masele akifunua kitambaa ili kuweka wazi maelezo ya mradi uliozinduliwa katika eneo la kazi Kijijini Lwamgasa  nyuma yake ni Mkuu wa Wilaya ya Geita.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Bw. Stephen Masele, akiweka mchanga katika mtambo unaozinduliwa ikiwa ni ishara ya kuwa mtambo wanaoletewa wananchi wa kijiji hicho ni mzuri na unafanya kazi kama ilivyokusudiwa.


Wataalamu wakisafisha mchanga huo ikiwa ni hatua za awali za kupata dhahabu.
·     
 SERIKALI kwa kushirikiana na Benki ya Dunia na wachimbaji wakubwa wa madini nchini imezindua mradi wa kwanza Afrika wa mfano wa kuchakata dhahabu kwa wachimbaji wadogo wa madini katika kijiji cha LWAMGASA wilayani Geita.
Mradi huo umezinduliwa mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Madini) Mhe. Stephen Masele aliyekuwa mgeni rasmi katika sherehe za uzinduzi wa mradi huo ulioanza kujadiliwa mwishoni mwa mwaka jana.
Wizara ya Nishati na Madini kwa kugundua umuhimu na mchango wa wachimbaji wadogo wa madini katika uchumi wa nchi ulibuni mradi huu na kuwashirikisha wadau wengine wa maendeleo wakiwemo Benki ya Dunia, Migodi mikubwa ya dhahabu na Chama cha wachimbaji wadogo na kusaini mkataba wa makubaliano mnamo mwaka 2009.
Kwa upande wake mwakilishi toka Benki ya Dunia Mr. Mamadou Barry alizungumzia utekelezaji wa mradi huo kuwa ni matokeo ya utendaji mzuri wa Serikali ya Tanzania hususan Wizara ya Nishati na Madini katika kutekeleza miradi inayofadhiliwa na benki hiyo hivyo kuifanya benki hiyo kuwa na imani na watendaji wake.
Aidha Mamadou ameeleza kuwa kwa kutambua mchango wa sekta ya madini kwa maendeleo ya Tanzania na kuwa na nafasi kubwa ya kutoa ajira kwa takribani watanzania milioni moja, ikiwa ni ajira  za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, Benki ya Dunia imeona ni vema kuwaendeleza wachimbaji wadogo ili kuwasaidia katika kukuza uchumi wao binafsi na kuinua kipato cha taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo mjini Geita Mr. Christopher  Tadeo alizungumzia kuwa uchimbaj mdogo  wa madini wilayani Geita ulianza kushamiri mwaka 1986. Aidha amebainisha changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo katika uzalishaji wa madini kuwa ni pamoja na uhaba wa mtaji, technolojia duni, elimu duni, kutokuwa na maeneo ya kutosha kukidhi haja na kiu ya wachimbaji wadogo.
Aidha Bw. Tadeo ameiomba serikali kutekeleza kwa haraka ahadi walizozitoa kwa wachimbaji wadogo wa madini ikiwa ni pamoja na  kuwanunulia vifaa kwa ajili ya wachimbaji wadogo, kuwagawia maeneo yanayorudishwa na wachimbaji wakubwa wa madini, kuwafikishia huduma ya nishati ya umeme katika maeneo ya machimbo.
Hata hivyo Bw. Tadeo amethibitisha kuwa mradi uliozinduliwa ni kielelezo tosha cha kutambua mchango wa serikali hususani uongozi wa wizara kw kutambua uhitaji wa wachimbaji wadogo wa madini.
Kwa upande wao wachimbaji wadogo mkoani Geita waliohojiwa na mwandishi wa habari hizi kwa pamoja walikiri kuupokea mradi huo kwa mikono miwili na kuishukuru serikali kwa kuwakumbuka na kutafuta njia za kuwasaidia, aidha walisisitiza umuhimu wa wao kupatiwa elimu juu ya kuvitumia mitambo hiyo kutokana na ukweli kwamba walizoea njia duni na kwamba hawana elimu na ujuzi wa kuweza kutumia vifaa hivyo vya kisasa.
“Sisi hatujasoma sasa wanasema hiyo mitambo inaendeshwa na wasomi inamaana sisi tutazidi kuwa masikini”Bi Jenipher Hagai alizungumza kwa huzuni na kuongeza kuwa wanaiomba serikali ifikilie kuwapa elimu juu ya uendeshaji wa mitambo hiyo jambo ambalo limekwishakufanyiwa kazi na tayari mpango wa kuwaelimisha wachimbaji hao upo na kwamba hawatakabidhiwa mitambo hiyo kuiendesha wenyewe mpaka pale watakapopata mafunzo na kufaulu  kutumia vifaa hivyo. Hayo yalibainishwa na mshauri mwelekezi Bw.John-Bosco Tindebwa
Mkuu wa Wilaya ya Geita Bw.Omary Magochie aliusifu uongozi wa kijiji cha Lwamgasa kwa utayari waliokuwa nao baada ya kuoneshwa fursa hii muhimu katika kuinua uchumi wao. Amebainisha kuwa hatua ya uzinduzi iliyofikiwa ni matunda ya utayari wao.
Ameeleza kwamba awali mradi huo ulipangwa kutekelezwa katika kijiji cha Nyamgusu ambao waligoma kuupokea mradi huo kwa sababu zao mbalimbali.
Aidha ameisifu kasi ya wizara na wadau walioshiriki katika mchakato huu kwa kufanikisha kufikia hitimisho la mradi huo na kueleza kuwa majadiliano ya uanzishwaji wa mradi yalianza mwezi oktoba na kabla ya mwaka kwisha tayari matokeo yake yamekwishapatikana.
Huu ni mwendelezo wa mipango ya Wizara ya Nishati na Madini katika kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini, awali wamewawezesha kupata mikopo kupitia Benki ya Uwekezaji (TIB) na sasa imewawezesha kwa kuwanunulia mtambo wa kuchakata dhahabu ambao utatumika kama model ya kuendeleza maeneo mengine shughuli za uchimbaji madini zinakoendelea.

No comments:

Post a Comment