TANGAZO


Tuesday, July 8, 2014

Mamia wajitokeza kushuhudia na kupata ukweli kuhusu mchanga wa dhahabu


Watumishi wa TMAA wakiwa tayari kuwaelimisha na kuwahudumia wananchi waliotembelea Banda lao kwenye Viwanja vya Saba Saba. (Picha zote na Saidi Mkabakuli)
Baadhi ya wananchi waliotembelea Banda la TMAA wakishuhudia mchanga wa dhahabu uliokuwa ukioneshwa banda hapo.


Baadhi ya wananchi waliotembelea Banda la TMAA wakishuhudia mchanga wa dhahabu uliokuwa ukioneshwa bandani hapo.
Wananchi wakiuangalia mchanga huo katika banda hilo, la TMAA wakishuhudia mchanga wa dhahabu

Na Saidi Mkabakuli
Mamia ya wakazi ya jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake, wamejitokeza kujionea mchanga wa dhahabu unaoneshwa kwenye banda la Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), lililopo katika Viwanja vya Maonesho ya Biashara ya Kimataifa vya Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam leo.

Mmoja wa wakazi hao, Bw. Shabaan Charahani, amesema ameshawishika kuja kujionea mchanga huo na kupata ukweli juu ya kutoroshwa kwa mchanga huo kama inavyovumishwa na watu wengi nchini.

“Nimekuja kujifunza masuala ya ukaguzi wa madini na kujua ukweli juu ya mchanga wa dhahabu unaozalishwa hapa nchini,” alisema Bw. Charahani.

Akitoa maelezo kwa wananchi hao waliojitokeza bandani hapo, Afisa Habari wa Wakala huo, Mhandisi Yisambi Shiwa alisema kuwa mchanga wa dhahabu ni zao lenye madini ya shaba na fedha lipatikanalo mara baada ya kuchenjua mawe yenye dhahabu kwenye mtambo wa kuchenjulia mawe hayo uliopo kwenye migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi.

Aliongeza kuwa kuna mkanganyiko wa matumizi sahihi ya neno mchanga wa dhahabu, ambapo kiusahihi mchanga wa dhahabu ni makinikia ya shaba (copper concentrate).

“Kutokana na madini ya shaba kuwa mengi kwenye huu ‘mchanga wa dhahabu’ kuliko madini mengine, jina rasmi linalotumika na kutambulisha zao hili ni makinikia ya shaba,” alifafanua.

Kwa mujibu wa Mhandisi Shiwa, kwa sasa, uzalishaji wa makinikia ya shaba unafanyika katika migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi tu. Akiitaja sababu ya kuwepo na aina ya mashapo ya dhahabu ya migodi hiyo kuwa na sifa tofauti na migodi mingine mikubwa ya dhahabu hapa nchini.

Akitaja sababu za kusafirishwa nje ya nchi mchanga huo, Mhandisi Shiwa kwamba kutokuwepo kwa teknolojia ya kutenganisha madini hayo, pamoja na gharama kubwa za kuendeshea mtambo wa kufanya kazi hiyo.

“Gharama za mtambo wa kuchenjulia madini hayo ni wastani wa dola za kimarekani milioni 500. Gharama hizi ni kubwa ukilinganisha na hali halisi ya mapato ya migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi yatokanayo na ‘mchanga wa dhahabu’,” alisema Mhandisi Shiwa.

Mhandisi Shiwa aliongeza, “kutokuwepo na umeme wa uhakika na uzalishaji duni wa makinikia hayo ndo sababu kuu za kutofanyika kwa kazi hiyo hapa nchini,” aliongeza.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo kiasi cha makinikia kinachozalishwa hapa nchini ni wastani wa tani 45,000 ilhal kiasi kinachotakiwa ni wastani wa tani 150,000 za makinikia ya shaba.

TMAA ni Wakala wa Serikali ulioanzishwa tarehe 2 Novemba, 2009 chini ya Sheria ya Wakala wa Serikali, Sura ya 245. 
Tamko la Waziri la kuanzisha Wakala lilichapishwa kwenye Gazeti la Serikali Namba 362 la tarehe 6 Novemba, 2009. 
Lengo la Wakala ni kuhakikisha kwamba, Serikali inapata mapato stahiki kutoka kwenye shughuli za uzalishaji na biashara ya madini nchini kupitia usimamizi na ukaguzi makini wa shughuli za uchimbaji, na kuhakikisha kuwa shughuli hizo zinafanyika kwa kuzingatia uhifadhi na utunzaji thabiti wa mazingira katika maeneo ya migodi.

No comments:

Post a Comment