Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, HAB Mkwizu (kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), mapema hii leo, jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma yanayotarajiwa kuanza Juni 16. Katikati ni Mkurugenzi Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu wa ofisi hiyo, Bi. Roxana Kijazi na kulia ni Mkrugenzi Msaidizi Idara ya Uchumi na Ushauri Kazi, Bw. Hassan Kitenge.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza kwa
makini Naibu Katibu Mkuu toka Ofisi ya
Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. HAB Mkwizu (hayupo pichani) wakati wa
mkutano na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma
yanayotarajiwa kuanza Juni 16 jijini Dar es Salaam.
Na Eliphace Marwa -MAELEZO
ZAIDI ya Taasisi 30 za Serikali hapa nchini
zinatarajiwa kushiriki katika maonesho ya wiki moja ya utumishi wa Umma
yanayotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 16 hadi 23 Juni katika viwanja vya
Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa leo, jijini Dar es Salaam na Naibu
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. HAB Mkwizu wakati
akizungumza na waandishi wa habari juu ya kukamilika kwa maandalizi hayo.
Mkwizu alisema maadhimisho hayo ambayo huratibiwa na ofisi
yake yatafunguliwa rasmi na Waziri wa
Nchi ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mhe. Hawa Ghasia na
kuambatana na uoneshaji wa kazi
mbalimbali za Taasisi za Serikali wanazozifanya kila mwaka kwa lengo la
kutathmini kazi zinazofanywa na sekta hiyo katika kuleta maendeleo ya kiuchumi
na kijamii.
“Kuadhimisha
siku hii kutakuwa na kongamano la siku mbili litakalojadili miaka hamsini ya Muungano
katika Utumishi wa Umma ambalo litafanyika kuanzia tarehe 19 hadi 20 Juni katika Kituo cha Mikutano cha kimataifa cha Mwalimu Nyerere
jijini Dar es Salaam na kusimamiwa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue”,
alisema Bw. Mkwizu
Aidha Bw. Mkwizu pia alitoa wito kwa wananchi kujitokeza
kwa wingi katika viwanja vya Mnazi mmoja ili kupata huduma na kutoa maoni juu
ya kazi mbalimbali zinazofanywa na Taasisi za Serikali.
Kauli mbiu ya Maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni ‶Mkataba wa Msingi na Kanuni za
Utumishi wa Umma Barani Afrika ni Chachu ya kuimarisha utawala bora na
Uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa Uwazi″
Kilele cha Maadhimisho hayo hufanyika kila mwaka
tarehe 23 Juni kama ilivyokubaliwa na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU)
mwaka 1994 katika mkutano wa Mawaziri wa Utumishi wa Umma barani Afrika uliofanyika
nchini Morroco.

No comments:
Post a Comment