Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi, akizungumza kuhusu tahadhari hiyo kwa matapeli wa ajira za Serikali.
Katibu wa
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi.
Na Kassim
Nyaki
SEKRETARIETI ya Ajira
inapenda kutoa tahadhari kwa waombaji wote wa nafasi za kazi kupitia chombo
hiki kuwa kumezuka kundi la watu wanaojifanya ni watumishi wa Sekretarieti ya
Ajira ambao kwa makusudi wamekuwa wakiwapigia simu kwa lengo la kuwalaghai
baadhi ya waombaji wa nafasi za kazi Serikali wakidai wapewe fedha ili waweze kuwasaidia kupata kazi Serikalini
kwa urahisi mara baada ya kufanya
usaili.
Katibu wa
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bw. Xavier Daudi amefikia hatua
ya kutoa tamko hili kutokana na baadhi ya waombaji wa nafasi za kazi Serikalini
kukumbwa na kadhia hiyo na kutoa taarifa. Amesema Ofisi yake haina utaratibu wa
kuwapigia simu waombaji wa fursa za ajira Serikalini na kuwadai fedha ili
kuweza kuwapatia nafasi ya ajira.
Hivyo, endapo kuna msailiwa yeyote
atakayepigiwa simu ajue hao watu ni matapeli na ni vyema akawapuuza kw
akutokuwapa ushirikiano na badala yake kuwaripoti katika vyombo vya dola ili
waweze kuwachukulia hatua stahiki.
Daudi
amesema kuwa ni vyema kila mwombaji wa nafasi za kazi Serikalini kutambua kuwa
Sekretarieti ya Ajira inaendesha mchakato wa ajira kwa mujibu wa Sheria, Kanuni
na Taratibu na si vinginevyo. Aidha, ni kosa kosa kwa mtu au Taasisi yeyote ile
kutoa ama kupokea rushwa ili katika kutoa huduma au kutekeleza jambo lingine
lolote.
Katibu anawataka watu wote wanaowapigia waombaji wa
fursa za ajira simu na kuwalaghai kuacha kufanya hivyo mara moja na Serikali
inaendelea kuyafanyia kazi malalamiko ambayo yamewasilishwa katika ofisi yake
na pindi inatakapowabaini wahusika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria za
nchi.
Aliongeza
kuwa mtu yeyote anayepata kazi kupitia chombo hiki ajue ameipata kutokana na
kuwa na sifa na kutimiza vigezo vyote baada ya kupitia mchakato mzima hadi kupangiwa
kituo cha kazi lakini sio kwamba amepata kazi kutokana na rushwa au kumjua mtu,
hivyo, hakuna sababu yoyote ya kuhadaika na watu wasiopenda kufanya kazi za
halali na badala yake kutumia njia za mkato kujipatia fedha kirahisi bila hata
ya kujali madhara anayomsababishia mwingine au yanayoweza kumkuta pindi
atakapobainika kufanya hivyo.
Ni
vyema wananchi wote wakafahamu kuwa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa
Umma ndio chombo pekee kilichoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma
Na. 8 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa na
Sheria Na. 18 ya mwaka 2007 kifungu 29 (1), pamoja na marekebisho yaliyofanyika
katika Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 1998 toleo
Na. 2 la mwaka 2008 ambapo katika Vifungu Na. 4.6 na 6.6. vya Sera hiyo
vimetamka kuwepo kwa chombo maalum cha kushughulikia mchakato wa masuala ya
ajira katika Utumishi wa Umma na si mtu au kikundi cha watu kinachotaka
kupotosha uma kwa kujua au kutokujua wanaweza kumpa mwombaji kazi ajira
Serikalini kwa njia za mkato.
Aidha,
amewasisitizia wadau wote wa Sekretarieti ya Ajira wanaotafuta kazi pindi
wanapopigiwa simu au kuona matangazo yanayohusu ajira Serikalini katika Vyombo
mbalimbali vya Habari ambavyo wanamashaka navyo, ikiwemo mitandao ya kijamii
wajaribu kujiridhisha kwa kuthibitisha taarifa hizo kama ni za kweli kwa
kutembelea tovuti ya Sekretarieti ya Ajira ambayo ni www.ajira.go.tz
kwa taarifa sahihi zihusianazo na ajira katika Utumishi wa Umma au kupiga simu
namba 255-687624975 kuanzia saa 1:30 asubuhi
hadi saa 9:30 jioni kila siku ya Jumatatu hadi Ijumaa ili kupata ufafanuzi
zaidi.
Amesema,
Sekretarieti ya Ajira haiwajibiki na wala haitawajibika kwa mtu au watu
watakaopigiwa simu na kutoa fedha kwa matapeli hao kwani ni kosa kutoa au
kupokea rushwa kwa mujibu wa Sheria za nchi.

No comments:
Post a Comment