TANGAZO


Thursday, May 22, 2014

TFDA watakiwa kufanya ukaguzi wa ghafla katika maduka ya vipodozi na dawa nchini

Wanahabari  kutoka  mkoa  wa Iringa  wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi  wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), jana wakati wa warsha ya  siku moja ya  wahariri na  waandishi wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini iliyoandaliwa na TFDA  kwa lengo la kuwaelimisha juu ya bidhaa feki. (Picha na Mwandishiwetublog)
 
MAMLAKA ya  chakula na dawa nchini  (TFDA) imetakiwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa  wafanyabiashara  wanaouza  bidhaa mbali mbali zikiwemo za vyakula  na dawa  na  vipodozi  ili kuyafungia kama njia ya  kusaidia  kulinda afya  za  watumiaji.

Ushauri  huo  umetolewa  jana jijini Mbeya na kaimu katibu  tawala  wa mkoa  wa Mbeya Bw  Leonard Magacha  wakati  wa  kufungua  warsha  ya  siku  moja iliyoandaliwa na TFD kwa  waadhishi wa  habari na  wahariri  wa  mikoa ya nyanda  za juu kusini iliyohusisha mkoa  wa Iringa, Ruvuma, Njombe, Katavi Rukwa na wenyeji  Mbeya.
 
Magacha  alisema  kuwa ukaguzi  wa mara kwa mara  utasaidia  kunusuru afya  za  watumiaji wa  bidhaa hizo ambazo zilizo nyingi  zipo sokoni  na  wananchi  wameendelea  kuzitumia kutokana na kutokuwa na uelewa  wa  kutosha.

Hivyo  alisema ukaguzi  wa mara kwa mara  utapelekea  wafanyabiashara  kuuza bidhaa salama  na zenye  ubora zaidi.

Magacha  alisema   pia jukumu jingine  ni  kudhibiti matangazo ya bidhaa za  chakula,dawa ,vipodozi na vifaa tiba ili kuzuia matangazo yenye  nia ya  kupotosha umma kwa  lengo la kibiashara

"Napenda  kuwaeleza  kuwa  suala la kudhibiti matangazo  ni la kisheria na katika kuhakikisha  utekelezaji wake ,zipo kanuni  za  udhibiti wa matangazo ya  vyakula ,dawa na vipodozi zilizoandaliwa chini ya sheria namba 1 ya 2003 na zilianza kutumika tangu mwaka 2010" alisema Magacha

Kuwa kati ya  changamoto kubwa zaidi ambazo mamalaka imekuwa ikikabiliana nazo  toka kuanzishwa kwake ni zaidi ya miaka kumi  sasa iliyopita  ni kushuhudia kutolewa  kwa matangazo ya  bidhaa inazozidhibiti kupitia vyombo  mbali mbali vya habari bila kibali  cha TFDA kinyume na matakwa ya sheria na kanuni na hivyo kuchangia kupotosha jamii.

"Pamoja na  upungufu   huu kwa vyombo  vya habari  napenda nitambue ushirikiano ambao umeendelea kutolewa na baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vikiwaelekeza watu wenye nia ya kutoa matangazo au kununua vipindi katika vyombo  vya habari kuzungumzia usalama na ubora  wa  chakula ,dawa ,vipodozi na vifaa tiba kuhakikisha kuwa  wanapata  vibali kutoka TFDA" 

Pia  alitaka  TFDA  kuendelea  kufanya mazungumzo na mamlaka  za  udhibiti wa vyakula na dawa za nchi za jirani ambazo sheria  zao  zinapingana na sheria  za Tanzania  na  hivyo  kufanya nchi  hizo  kuendelea  kuzalisha  bidhaa hizo ambazo kwa sheria  ya Tanzania  zinaonekana kuwa ni bandia.

Kwa  upande  wake mkurugenzi  mkuu wa TFDA Bi Charys Ugullum  alisema  kuwa TFDA ni wakala  wa serikali na kuwa mamlaka  hiyo  ilianzishwa chini ya kifungu namba 4(1) cha sheria  namba 1 ya chakula,dawa na  vipodozi sura 219 iliyoanza  kutumika rasmi Julai mosi 2003

Bi Ugullum alisema mafunzo hayo kwa  wanahabari  yamelenga zaidi  kuelimisha jamii inayozunguka  mikoa  hiyo na Tanzania kwa  ujumla ili  kuweza  kuwa na uelewa wa kutosha  juu ya bidhaa wanazotumia kama  zina ubora ama hazina ubora waweze  kutoa taarifa kwa TFDA.

No comments:

Post a Comment