RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
amewataka watumishi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi kuifahamu vyema dhana ya utawala bora ili wawe mfano wa kuigwa
katika kuitekeleza dhana hiyo kwa vitendo.
Akizungumza
katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Mpangokazi wa Ofisi hiyo
kwa kipindi cha Julai 2013 na Machi 2014 jana, Dk. Shein alieleza kuwa
utawala bora ni dhana pana na ni suala mtambuka hivyo watumishi wa Ofisi
hiyo hawana budi kuielewa na kuitekeleza ipasavyo katika utendaji wa
shughuli zao za kila siku.
Alisisitiza
kuwa suala la utawala bora linagusa kila eneo la utendaji na utoaji
huduma katika serikali hivyo watumishi wote serikalini hawana budi
kuzingatia misingi ya utawala bora katika utendaji wao.
Aliongeza
kuwa utawala bora ni suala muhimu katika uendeshaji wa shughuli za
Serikali na ndio maana uongozi wa Awamu ya Saba ulipoingia madarakani
umekuwa ukiimarisha jitihada zilizoanzishwa na uongpzi wa Awamu ya Sita
kwa kuunda na kuimarisha taasisi zinazosimamia masuala ya utawala bora
nchini.
Kuhusu
bajeti ya mwaka 2014/2015 ya Ofisi ya Rais na Mawenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Shein amewataka viongozi na watendaji wa Ofisi hiyo
kutumia uzoefu wa Mpangokazi wao ili waweze kuandaa bajeti halisi kwa
kupanga malengo yanayopomika kwa kuzingatia vipaumbele na matumizi bora
ya rasilimali zilizopo.
Alibainisha
kuwa ni vyema kupanga vipaumbele vichache ambavyo bajeti itaweza
kuvigharamia ili hatimae kupata matokeo mazuri na kusisitiza kuwa kwa
kufanya hivyo Ofisi hiyo itakuwa imekwenda sambamba na mfumo wa bajeti
unaozingatia matokeo ambao serikali inaufuata.
Katika
maelezo yake ya awali Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Dk.
Mwinyihaji Makame alikiambia kikao hicho kuwa katika kipindi cha miezi
tisa iliyopita Ofisi imeweza kutekeleza majukumu yake kwa mafanikio
makubwa kwa kuweza kutekeleza malengo yaliyopangwa.
Alieleza
kuwa utekelezaji wa malengo hayo yalizingatia mipango ya mikuu ya
maendeleo ya nchi ukiwemo Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza
Umasikini-MKUZA II, Dira ya Maendeleo 2020, Malengo ya Milenia pamoja na
Ilani ya Uchaguzi wa CCM mwaka 2010/2015.
Alibainisha
kuwa pamoja na mafanikio hayo, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi inaendelea kutekeleza jumla ya programu na miradi 14 ikiwemo
Mradi wa kuimarisha Mawasiliano Ikulu, Mpango wa Ufuatiliaji na Tathmini
Yenye Kuleta Matokeo ya MKUZA II na Kujenga Uwezo wa Utekelezaji wa Taasisi za Serikali.
Miradi
mingine ni pamoja na Mradi wa Utafiti wa Hali ya Utumishi Nchini, Mradi
wa Uimarishaji Sekta ya Takwimu, Mradi wa Kuimarisha Juhudi za Kuzuia
Rushwa Zanzibar na Mradi wa Kuoanisha Masuala ya Idadi ya Watu, Afya ya
Uzazi, Jinsia na Umasikini.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Katibu
Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alirejea wito wake wa kuzitaka
Wizara na Idara za Serikali kuongeza umakini katika kupanga malengo
ambayo hatimae yanaweza kupimika.
Alisisitiza
kuwa ni lazima kuwe na uwiano kati ya malengo na shughuli za kufikia
malengo hayo ili kupata matokeo yaliyopangwa vinginevyo kasoro katika
upangaji malengo zinasababisha Wizara na Idara za Serikali kushindwa
kufikia matokeo hayo yanayotarajiwa.
Katika
kikao hicho alizikumbusha Wizara na Idara za Serikali kuwa malengo ya
Wizara na Idara makao makuu hayawezi kuwa tofauti na malengo ya Ofisi
kuu za Pemba hivyo katika upangaji wa malengo pamoja na bajeti suala
hilo halina budi kuzingatiwa.
Alifafanua
kuwa Ofisi za Pemba ni sehemu ya Makao Makuu ya wizara na Idara hivyo
malengo yao hayawezi kutofautiana ingawa kwa kiasi fulani shughuli
zinaweza kutofautiana katika kuyafikia malengo hayo kutokana na
mazingira yaliyopo.
No comments:
Post a Comment