Mwenyekiti
wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Lipumba, akiongozana na Katibu Mkuu wa Chama
hicho Maalim Seif Sharif Hamad, kuelekea ukumbi wa mikutano katika
ofisi kuu za Chama hicho, Buguruni Dar es Salaam.
Baadhi
ya wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi CUF Taifa, wakifuatilia kikao hicho
kinachofanyika Ofisi Kuu za CUF Buguruni Dar es Salaam.
Mwenyekiti
wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Lipumba, akifungua kikao cha siku tatu cha
Baraza Kuu la Uongozi CUF Taifa, katika ofisi kuu za Chama hicho,
Buguruni Dar es Salaam. (Picha zote na Salmin Said, OMKR)
Na: Hassan Hamad (OMKR).
Mwenyekiti
wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Haruna Lipumba ameweka bayana kuwa Chama
chake pamoja na washirika wenzao wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(UKAWA), hawatorejea kwenye Bunge maalum la katiba mpaka wahakikishe
kuwa kinachojadiliwa ni rasimu ya katiba inayotokana na mawazo ya
wananchi ambayo roho yake ni sura ya sita inayoelezea muundo wa Muungano
wa Serikali tatu.
Amesema
kamwe hawatokuwa sehemu ya kujadili na kupitisha rasimu inayokiuka
misingi ya mawazo ya wananchi na kufuata matakwa ya Chama Cha Mapinduzi
ambacho kimeigeuza rasimu hiyo kuwa ya kwao.
Prof.
Lipumba ametoa kauli hiyo wakati akifungua kikao cha kawaida cha siku
tatu cha Baraza Kuu la Uongozi la CUF, kinachofanyika Ofisi kuu za Chama
hicho Buguruni Dar es Salaam.
Amefahamisha
kuwa mpango wa kulivuruga Bunge hilo Maalum la Katiba ulianza zamani
baada Mwenyekiti wa Bunge hilo Samuel Sita kuanza kupindisha kanuni kwa
kumruhusu Rais Jakaya Kikwete kuzindua bunge hilo mwisho, sambamba na
njama za kutaka kumpa Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba Jaji Joseph Warioba muda mfupi wa kuwasilisha Rasimu ya Tume
hiyo.
Ameelezea
kusikitishwa na kitendo cha kubezwa kwa rasimu ya katiba iliyowahusisha
watu wazito ambao wengi wao ni kutoka Chama cha Mapinduzi na kuhoji
hali ingekuwaje kama yeye ndio angekuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo.
“Ni
jambo la kusikitisha kweli kuona mapendekezo ya Tume ya Katiba
yanapuuzwa wakati tume hii ilikuwa na watu wazito wanaoaminika sana
wakiwemo Jaji Mstaafu Warioba, Mhe. Salim Ahmed Salim, Augostino
Ramadhan na wangine wazito kutoka CCM, sijui kama Mwenyekiti ningekuwa
mimi Prof. Lipumba kutoka upinzani hali ingekuwaje?’ alihoji Lipumba.
Prof. Lipumba ametumia fursa hiyo pia kutoa ufafanuzi kuwa vitendo vilivyofanywa na kundi la “Interahamwe”
vilianzia na lugha za kibaguzi na uchochezi ambazo hazikukemewa, na
hatimaye kusababisha mauwaji ya halaiki nchini Rwanda.
“Inakuwaje
leo kiongozi wa nchi anakuwa mstari wa mbele kuhamasisha lugha za
kibaguzi na uchochezi, huku viongozi wengine wakifurahia jambo hilo,
tunaelekea wapi?” aliendelea kuhoji Prof. Lipumba.
Aidha
ameelezea hatua ya Serikali ya kuifunga Tovuti ya iliyokuwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, na kukiita kitendo hicho kuwa ni cha ‘kihuni’,
kwani wananchi wengi walikuwa wakipata taarifa za tume kupitia tovuti
hiyo.
Amewaasa wajumbe wa kikao hicho kuwa wana kazi kubwa ya kutathmini hali ya kisiasa na kuweka mikakati imara ya kukabiliana na kile anachokiita “Ombwe” la uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi.
Mapema
akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif
Hamad, amesema malengo makuu ya kikao hicho ni pamoja na kufanya uteuzi
wa mwisho kwa wagombea wa nafasi za ukatibu na uwenyeviti katika ngazi
za Wilaya, pamoja na kuandaa na kupitisha Mkutano Mkuu wa Taifa.
“Kikao
hiki kilikuwa ni cha siku mbili, lakini kutokana na uzito wa ajenda
hizi imetubidi tukifanye kwa siku tatu ili kuweka mambo sawa”,
alifahamisha Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar.
No comments:
Post a Comment